Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Edward Lowassa ‘hajawahi’ kuwa CCM wala Chadema

44718 Pic+edo Edward Lowassa ‘hajawahi’ kuwa CCM wala Chadema

Tue, 5 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Edward Ngoyai Lowassa. Bado ni mtu shujaa tofauti na unavyoweza kumchukulia. Amejipima, amejichekecha, amejitathimini, amejielewa. Amenyoosha mikono juu. Kama kuna mtu alitumwa kwenda kumwambia arudi CCM nadhani alimwambia ukweli.

Wakati mwingine huwa najiambia ukweli kama ambao inawezekana Edward mwenzangu alijiambia. Lowassa hajawahi kuwa CCM wala hajawahi kuwa Chadema. Lowassa amewahi kuwa mgombea urais tu katika nafsi yake kuanzia mwaka 1995.

Utashi wake wa kuupata urais nadhani ni mkubwa kuliko mapenzi kwa vyama vya siasa. Alivitumikia kwa ajili ya kupata urais kwa sababu jicho lake lilikuwa linaona mbali kuliko baadhi ya wanasiasa, ndio maana alijua namna ya kujijenga zaidi.

Nafsi yake imemtuma kuwa rais kwa muda mrefu. Ameishi na ndoto hiyo. Ameipigania ndoto yake. kuna wakati alipanga kubadilishana urais na rafiki ambaye alianza zamu ya kuwa rais baadaye wakatofautiana. Akaendelea kuitumia ndoto yake ndani ya CCM. Iliposhindikana akaamua kuitumikia ndoto yake Chadema.

Ndoto yake ndani ya Chadema haikutimia pia. Bahati mbaya mwelekeo wa ndoto kwa sasa umebakia kuwa ndoto. Nadhani mtu aliyetumwa kwake kumshawishi arudi CCM alifanya vyema, hata yeye mwenyewe amefanya vyema kuukubali ukweli huu.

Ukweli huu unatiwa nguvu na hali halisi kwamba kwa sasa Namba Moja ni mtu imara. Mtaani huwa wanamuita ‘chuma’. Nguvu ya nafasi yake katika kiti chake cha juu zaidi nchini imekuwa kubwa kuliko watu wanne waliowahi kukalia kiti chake. Lowassa mwenyewe amekubali ukweli huu. Nafasi ya 2020 kwake haipo.

Ameamua kustaafu kuwania nafasi hiyo kimya kimya na ameona bora aendeleze siku zake za ustaafu kwa amani. Amefanya kitu ambacho binafsi nilikuwa nakifikiria kwa niaba yake.

Mtu shujaa ni yule anayejisikiliza na kujiambia ukweli. Amenifundisha kitu. Kupambana kwa unachokiamini mpaka pale utakapouona mwisho. Ni kweli ameuona mwisho. Jinsi alivyodiriki kuhama CCM na kwenda Chadema aliwaacha watu wengi midomo wazi, lakini ukweli ni kwamba wakati mwingine dhamira yake ilikuwa kubwa kuliko mapenzi kwa vyama hivi vikubwa. Usijidanganye kwamba amewahi kuvipenda sana vyama hivi kuliko dhamira yake, kwamba alienda Chadema kwa sababu aliipenda na siamini kwamba amerudi CCM kwa sababu anaipenda. Siamini.



Columnist: mwananchi.co.tz