Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

ELIMU NA MALEZI : Ukali unatosha kumfundisha mtoto kuwajibika?

Wed, 17 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Frida na Andrew wanazungumza wafanyeje kumnusuru Denis ambaye ni mtoto wao wa miaka 10 anayesoma darasa la sita.

Maendeleo ya Denis shuleni sio mazuri. Mazungumzo ya leo yamechochewa zaidi na taarifa kuwa asipobadilika kwa muhula ujao, Denis atakuwa kwenye hatari ya kuondolewa shuleni kwa kushindwa kufikia wastani wa shule.

Ingawa wote wawili wanatamani Denis afanye vizuri shuleni, hivyo aendelee kusoma kwenye shule hiyo nzuri, ni dhahiri kila mmoja anafikiria mbinu tofauti.

‘Denis ana uwezo mzuri, tatizo tunamdekeza sana,’ anaeleza Andrew na kuendelea:

‘Huyu mtoto amefika mahali anaamini mafanikio yanakuja hivi hivi bila kujituma. Tuwe wakali tumuonyeshe kuwa bila kupambana hatofanikiwa. Kila siku nikirudi nyumbani nakuta mtoto kakaa anaangalia katuni. Kazi anazopewa shuleni hafanyi. Unategemea atafanikiwa?’

‘Najua ana upungufu wake,’ anajibu Frida, ‘Lakini kumbuka ndio kwanza ana miaka 10 tu. Bado ni mdogo na anahitaji kuelekezwa taratibu kuliko unavyofanya wewe. Huyu mtoto ukimkemea unamharibu.

Andrew anahisi mke wake anamlaumu. Akahoji: ‘Unataka kusema nini hapo? Unamaanisha tusimkemee tumwache afanye anavyotaka sio? Unataka ashindwe kupata wastani wa shule afukuzwe? Ninapomkemea ninataka ajifunze kuwajibika.

‘’Nilipokuwa kwenye umri wake nilikuwa na ratiba ya kusoma inayoeleweka. Nilicheza kama yeye lakini nilikuwa na muda wa kutosha kusoma. Sikufaulu kwa kukaa muda wote naangalia vitu visivyo na mchango wowote kwenye taaluma.’’

‘Nakuelewa mume wangu. Lakini ujue wewe na Denis ni watu wawili tofauti. Hulka zenu haziwezi kufanana na mmekulia kwenye nyakati tofauti. Sijui kama unaliona hilo. Denis hajiamini kama unavyojua. Ukimkemea anaumia sana na anashindwa kufanya kazi.’

‘Nini sasa hicho unachoongea? Tusimwambie kitu kwa sababu eti ataumia? Unajua tatizo lako ni hizo nadharia zako za saikolojia za Kizungu. Maisha na saikolojia ni vitu viwili tofauti. Mtoto hatokaa ajiamini mpaka aanze kufanya vizuri.

‘’Naona hilo hulielewi unaongea tu. Nilishakwambia hayo mawazo yako ndio yanamsaidia kufeli zaidi. Mtoto amekuwa kilaza kwa sababu nikiondoka hapa unamwacha.

‘‘Utakuja kunielewa akishakosa wastani wa shule,’ Andrew alishapandwa na jazba. Anaamini Frida anaacha upenyo wa Denis kucheza bila kuwajibika.

‘Naona umeanza tena mambo yako. Unamwita mtoto kilaza?’ Frida anajibu. ‘Mtoto wako mwenyewe unamwita kilaza kweli baba Debora? Sasa kama sisi wazazi wake tunamwona hana maana unafikiri atapata wapi nguvu za kujituma afanikiwe?’ ‘Nani kasema hana maana? Unakuza mambo sana. Sipendi sana hiyo tabia yako ya kuniwekea maneno mdomoni. Ninachokitaka mimi kiko wazi. Mtoto awe na nidhamu ya maisha. Denis ajifunze kuwajibika na kujituma zaidi. Hii tabia yake ya kurudi nyumbani na kukaa anaangalia katuni, ndio tatizo. Au wewe huoni?’

‘Sijui kwa nini hatueleweni mume wangu. Mimi naunga mkono mtoto kujifunza kuwajibika zaidi. Hunielewi. Tunakotofautiana mimi na wewe ni mbinu. Wewe unafikiri kumtisha na kumwadhibu kutamsaidia? Mimi napendekeza tumsaidie ajiamini zaidi ili aweze kuwajibika. Kumshambulia kwa sheria ngumu hakujamsaidia. Wewe mwenyewe shahidi. Kila ukimsema, anafeli zaidi. Hujaona?’

‘Kwa hiyo mimi ndio nimemfanya afeli sio?’

‘Sijasema hivyo. Watoto wanahitaji tuwaelekeze nini cha kufanya kwa upole. Wanahitaji tuwawekee mazingira rafiki yanayowafanya wajisikie msukumo wa kuwajibika zaidi. Denis sasa hivi hajiamini kabisa. Kama umegundua ukiongea tu akakimbilia chumbani. Tumemjengea woga. Kila ukiongea naye umekuwa ukimwambia ni mjinga. Hayo maneno hayamsaidii.’

‘Unapenda kunilaumu sana.’

‘Nakwambia ukweli. Unapokazana kumwambia mtoto amefeli unamsaidia? Kwani hukumbuki baba yako alikufanya ukajisikiaje? Mbona unataka kufanya makosa yale yale?’

‘Baba alikuwa mkali sana. Lakini huo ukali wake ndio ulinisaidia,’ Andrew alidakia kwa kujiamini, ‘Huoni nimefika hapa nilipofika?

‘‘Mafanikio niliyonayo hayajaja kwa kubembelezwa eti nijisikie naweza hata kama siwezi. Watoto bila kuwasukuma hawawezi kuwajibika. Nikikuacha ufanye hayo unayoyataka tutavuna mabua kwa Andrew. Sitoruhusu.’’

Andrew alinyanyuka kufuata ilikokuwa Biblia. ‘Soma hapa. Mithali 22: 15. Ujinga umefungwa ndani ya moyo wa mtoto. Lakini fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali.

Sasa wewe mwenzangu na visaikolojia vyako unataka tumdekeze. Kwa biblia ipi?’ aliongea kwa kujiamini huku akirudisha biblia mahali ilikokuwa.

‘Lakini mume wangu usiishie hapo,’ alijitetea Frida. ‘Biblia hiyo hiyo inasema pia tunahitaji upendo na huruma. Umekuwa mkali kupitiliza hasa mtoto anaposhindwa kufikia matarajio yako. Unapomkemea hivi anaogopa na anajisikia hatia. Sasa atajifunzaje akiwa kwenye hali hii?’

‘Mbona Debora namkemea na anafanya vizuri?’ alijitetea Andrew.

‘Debora ni tofauti na Denis. Ukiwalinganisha unakosea. Hapa tunaangalia namna nzuri ya kumsaidia Denis kuwajibika zaidi kwa sababu ukali na adhabu hazijamsaidia.’

Andrew kusikia hivyo alitikisa kichwa, akarusha magazeti yake mezani, akainuka na kuondoka bila kuaga. Frida alibaki ameduwaa sebuleni. Hali ya hewa nyumbani ikabadilika.

Nani yuko sahihi?

Umewahi kuwa na mjadala kama huu nyumbani kwako? Unadhani nani yuko sahihi kati ya Frida na Andrew?

Jibu linaweza kuwa gumu, kwa sababu na wewe kwa kiasi fulani unaweza kuwa upande mmoja wapo.

Labda mmewahi kubishana kwa kiasi hiki kuhusu maendeleo ya mtoto wenu. Kama ilivyo kwa Frida na Andrew, huenda mnashindwa kuelewana kwa sababu kila mmoja ana mawazo tofauti na anaamini kile anachokijua ni sahihi zaidi kuliko mawazo ya mwenzake.

Lakini pia, pengine hambishani na mwenzako lakini wakati mwingine unajikuta ukibishana na mawazo yako mwenyewe.

Unajikuta wakati mwingine unakuwa mkali, lakini saa nyingine unakuwa kama Frida. Leo unamtia moyo mtoto, kesho unakuwa mbogo.

Hata hivyo, hakuna wakati utafika wazazi wote tukawa na mtazamo unaofanana.

Pengine tufikiri namna ya kuwaleta pamoja wazazi wenye mawazo kama Frida na Andrew. Wakati upi tunahitaji kumpa nafasi Andrew, na wakati upi Andrew anapaswa kunyamaza ili Frida naye afanye kazi yake?

INAENDELEA

Columnist: mwananchi.co.tz