Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

ELIMU NA MALEZI: Jinsi ya kukuza udadisi wa mtoto mchanga

50076 MTOTO+PIC

Wed, 3 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kila mzazi angependa mtoto wake awe na ufahamu mzuri. Hapa tunaongelea uwezo wa mtoto kudadisi mambo anayokutana nayo, kuchakata taarifa anazoziona kwenye mazingira yake na kufanya maamuzi yenye tija katika kukabiliana na changamoto za kila siku. Uwezo huu unakuzwa tangu mtoto akiwa mchanga. Kuna mambo mzazi asipoyaelewa na kuyafanya mwanae anakuwa kwenye hatari ya kushindwa kufikia kiwango chake halisi cha ufahamu. Tena, wakati mwingine, ufahamu wa watoto waliolelewa na wazazi wasioelewa nini cha kufanya kuwajenga kiakili hujikuta wakisuasua katika ukuaji wa ufahamu wako n ahata kudumaa kiakili.

Kwa mujibu wa Jean Piaget, ukuaji wa ufahamu wa mtoto unategemea mambo mawili makubwa. Kwanza ni kile ambacho milango ya fahamu ya mtoto inakipokea. Macho, masikio, ngozi, ulimi, pua hivi vyote vinajaza ufahamu wa mtoto na taarifa ambazo zinapopokelewa zinamwezesha mtoto kujenga tajiriba (experience) itakayotumika katika kuchakata taarifa anazokutana nazo vizuri. Mlango unaofanya kazi vizuri zaidi tangu mtoto anapozaliwa ni mguso. Unapowagusa watoto kwa kuwakumbatia unawasaidia kuimarisha mfumo wao wa fahamu.

Lakini pia namna ya pili ya kukuza uwezo wa mtoto kuelewa mambo ni kupitia vitendo anavyovifanya. Piaget anasema tabia ya kichanga inategemea vile anavyoweza kuvifanya kwa kutumia viungo vya mwili wake. Maana yake ni kwamba mtoto mchangamfu, anayeshughulika zaidi, ndiye anayekuwa kwenye nafasi kubwa ya kuwa na ufahamu mzuri kuliko mtoto aliyepooza, asiyeona haja ya kushughulika.

Unaweza kujiuliza kuna uhusiano gani kati ya vitendo anavyovifanya mtoto na ufahamu wake? Inakuwaje, kwa mfano, mtoto kujaribu kufikia mdoli wake kumsaidie kukuza ufahamu? Jibu ni kwamba kila anachokifanya mtoto mchanga kinalenga kutatua changamoto fulani kwenye mazingira yake au kufurahia kile kinachomvutia. Tukumbuke kuwa kadri mtoto anavyokua, hukutana na vitu vingi vinavyomshangaza na hivyo kumfanya adadisi kwa kujiuliza maswali. Mfano wa vitu vinavyoweza kumfanya ajiulize maswali ni pale anapoona kitu chenye rangi iliyong’aa. Udadisi utamfanya anapojaribu kufikia. Pia udadisi unaweza kuchochewa na sauti anayoitoa bila kujua, ambayo inaweza kumfanya aone inakuwaje akiirudia rudia. Vitu kama hivi vinamfanya awe mdadisi. Kadri anavyoshangazwa na mazingira yake ndivyo anavyofikiri vizuri zaidi.

Ushauri kwa wazazi ni kuhakikisha mtoto anazungukwa na vitu vinavyoongeza udadisi wake. Udadisi unaongezeka kadri unavyomkutanisha na vitu asivyovitarajia. Mwekee vitu vinavyotoa sauti ya kuvutia vinapoguswa. Mahali anapolala pawekewe vitu vinavyomfanya ajaribu kuvifikia. Hivi vinaweza kuwa vitu vinavyosogea, vitu vinavyotoa harufu nzuri, vitu vyenye rangi ya kuvutia. Unapomwekea vitu kama hivi unamfanya ajaribu kufanya kitu aone matokeo ya kile anachokifanya. Kama sio kunyoosha mkono, atatumia vidole, atajaribu kutambaa, atatamani asimame, atembelee muradi tu aone hicho kinachomvutia kinafananaje.



Columnist: mwananchi.co.tz