Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

ELIMU NA MALEZI: ‘Home work’ zinawasaidia watoto kujifunza?

Tue, 19 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Imekuwa kawaida watoto kurudi nyumbani wakiwa na kazi za shule wanazotakiwa kuzikamilisha wanapokuwa nyumbani. Kazi hizi zinazofahamika kama ‘homework’, mara nyingi hulenga kujenga daraja zuri kati ya kile mtoto alichojifunza shuleni na mazingira ya nyumbani anakoishi baada ya saa za shule. Inatarajiwa, kwa mfano, kuwa kazi hizi za nyumbani zitamsaidia mtoto kutenga muda fulani kwa ajili ya kurejea kile alichojifunza shuleni, na hivyo kujikuta akijijenga utamaduni wa nidhamu ya muda hata anapokuwa nyumbani.

Aidha, ili kukamilisha kazi hizi, mtoto pia hulazimika kupata msaada wa watu wengine zaidi ya mwalimu wake rasmi wa darasani. Mtoto, kwa mfano, atahitaji msaada wa mzazi wake, dada yake, kaka yake au mtu mwingine yeyote anayepatikana nyumbani mwenye utayari wa kumpa msaada anaouhitaji. Msaada kama huu kutoka kwa ‘walimu’ wanaopatikana kwenye mazingira ya nyumbani unamsaidia kukazia maarifa aliyoanza kuyapata akiwa shuleni.

Kwa kuzingatia uhusiano huo kati ya shule na nyumbani anakoishi mtoto, kazi hizi za nyumbani zinatarajiwa kumsaidia mtoto kuendeleza maarifa aliyoyapata shuleni kwa kuyahusisha na maisha yake ya kila siku anapokuwa nyumbani. Kwa mfano, mtoto aliyefundishwa kutambua vyombo muhimu vinavyotumika kuandalia chakula, anaweza kupewa kazi ya nyumbani inayomfanya aende jikoni kuona vyombo ambavyo mama yake huvitumia kuandalia chakula. Kazi kama hii inamwezesha kuona uhusiano wa moja kwa moja kati ya kile alichokisikia shuleni na maisha halisi anayoyaona nyumbani.

Lakini je, walimu wanapowapa watoto wetu kazi hizi za nyumbani wanazingatia kuweka mazingira ya kujenga daraja kati yao na ‘walimu’ wanaoishi na mtoto? Wazazi wameanza kuzitazama kazi hizi kwa jicho la mashaka kidogo na hivyo kuhoji mantiki ya kazi hizi zinazoonekana kuwa mzigo mzito kwa watoto. Mashaka yanaanza pale ambapo mwalimu anatoa kazi ambazo kimsingi zingeweza kukamilika ndani ya muda wa kipindi. Matokeo yake, maswali ambayo mtoto hulazimika kwenda nayo nyumbani mbali na kumnyima muda wa kubadili shughuli anaporudi nyumbani, yanamjengea msongo wa shughuli ambao hatimaye humnyima nafasi muhimu ya kucheza.

Lakini pia, kuna ukweli kuwa kazi hizi wakati mwingine zinadai uelewa mkubwa kuliko uwezo halisi alionao mtoto. Matokeo yake, ili mtoto aweze kuzikamilisha anahitaji msaada uliopita kiasi kutoka kwa watu wengine. Tunafahamu, mathalani, wazazi wengi hujikuta wao wenyewe wakizifanya kwa niaba ya watoto wao au kugombana na watoto wanaposhindwa kuzifanya. Katika mazingira kama haya ya kusaidiwa au kufokewa, mtoto hujikuta akianza kuwa na wasiwasi na uwezo wake.

Masuala kama haya yanatuleta kwenye swali muhimu la kujiuliza: Je kazi hizi za nyumbani zina tija kwa watoto? Una maoni gani?



Columnist: mwananchi.co.tz