Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Duniani kote thamani ya msanii huonekana baada ya kifo

9363 Pic+duniani TZW

Mon, 18 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanzoni mwa wiki hii jioni moja nikiwa mitaa ya Kurasini baada ya shibe ya mwaliko wa futari kwenye mkeka mujarabu nimelaza mbavu zangu kilofalofa huku nikiperuzi simu yangu.

Ubora wa futari ambayo ilikuwa na mchanganyiko wa vitu vyote vinavyotakiwa. Wakati naperuzi simu yangu nikaingia kwenye ukurasa wa staa mmoja wa kike wa muziki. Ametundika maneno mtandaoni yaliyonifanya nivute kumbukumbu nyingi nyuma. Hebu tuachane naye kwanza.

Mshikaji mmoja hivi sanaa ya muziki ilimtambua kama Sam wa Ukweli ameaga dunia wiki iliyopita. Huyu ni miongoni mwa wanamuziki waliokuja kwenye kizazi cha kina Diamond Platinumz na wenzake.

Ujio wake ulikwenda sambamba na akina Ommy Dimpoz, Belle 9, Ben Pol, Barnaba, Amin, Mwasiti, Linnah na wengineo wengi tu ambao kwa kiasi kikubwa walipindua mambo.

Waliua mizuka ya madogo kuchana mistari. Baada ya kuona washikaji wa kuimba (akiwemo yeye Sam wa Ukweli) wanapasua anga fasta kuliko wapenda ngumu kwa ‘biti’ zile za kubum kabam. Hapo kabla wachanaji walitamba zaidi.

Kinachoshangaza ni kwamba, kifo chake kimezua mijadala kiasi cha kuacha kumuongelea kwa mazuri yake. Na watu baadhi ya wanamuziki wenzake kuanza maneno mitaani na mitandaoni.

Siyo mijadala mipya ni ileile kama iliyokuwepo wakati wa msiba wa Ngwair. Kwamba nyimbo za wanamuziki zinapigwa sana au kuongelewa kwa wema baada ya kufariki dunia tofauti na wanapokuwa hai.

Hili suala linanikata stimu sana. Linakera na sitashangaa siku mwanamuziki akafariki na nyimbo zake tukafanya kuzitafuta mitaani baada ya kutozisikia redioni na runingani.

Kwa sababu lawama hizi zimekuwa kubwa na sasa zimehama kwa mashabiki na kwenda kwa wanamuziki wenyewe. Kifo cha Sam kimewaibua wasanii kadhaa waliolalamika mitandaoni.

Kwamba redio na runinga zinatwanga sasa nyimbo za Sam wa Ukweli baada ya kuaga dunia. Hizi pia ni lawama ambazo zina baraka ya kiibilisi ndani yake. Sidhani kama wanawatendea haki jamaa wa redio na runinga.

Hebu kwanza tujiulize wenyewe, siku chache kabla ya mwili wa Sam wa Ukweli kuachana na roho yake, ni wimbo au nyimbo gani alizotoa ambazo leo tunaweza kulaumu redio na runinga kuwa hazikuutendea au kuzitendea haki mpaka alipofariki?

Sam wa Ukweli taarifa ya msiba wake ilikuja na mshituko wa aina tatu. Wapo walioshangaa kifo chake, hao nd’o wengi sana. Wapo baadhi kifo chake kimewakumbusha uwepo wake na wapo ambao walishangaa kusikia kulikuwa na mwanamuziki huyo.

Nyakati hizi za akina Harmonize alikuwa na kasi ya konokono kwenye gemu. Hakuweza kwenda na kasi ya muziki wa kiki kabla na baada ya kuachia ngoma. Ubora wa muziki wa saa ni ukubwa wa kiki.

Pia, wanamuziki wengi vifo vimewakuta wakiwa kwenye hali tofauti na ukubwa wa majina yao. Wakiwa hawana kazi mpya au kazi bora kama zile za awali wakati wakipambana kutengeneza majina.

Ndivyo ilivyokuwa kwa Ngwair, siku chache kabla ya umauti kumtenganisha na ulimwengu huu hakuwa Ngwair yule wa enzi za Mikasi na Getho Langu. Alikuwa Ngwair sawa lakini siyo Ngwair aliyevuruga akili za masela na masista duu kitaani. Alikuwa na nyimbo mpya kama ‘Bifu’, ambao haukuwa daraja moja na ‘Mikasi’. ‘She Got Gwan’ wala ‘Mtoto wa Jah Kaya’. Hakuwa yule Ngwair ambaye mitaa ya Uswahilini kama Tandika walimpenda na maeneo ya ushuani kama Oysterbay walimtii.

Siku za mwisho wa uhai wake alikuwa Ngwair anayepambana kurudi kwenye ubora wake akiwa na hasira na pesa kuliko wakati wote. Ni wakati ambao hakuwa anatafuta jina, bali anatufata pesa. Na siyo pesa tu bali pesa nyingi.

Haikuwa ajabu kifo kumtokea nje ya mipaka ya Taifa lake. Zilikuwa mbio za kusaka pesa na siyo za kuandika mistari. Ukubwa wa mazishi yake ni kutokana na ubora wa msingi wake tangu anatoka kimuziki.

Wakati anatoka alikuwa kwenye uzito wa tani nyingi. Balaa alilokuja nalo ndilo lililioendelea kulinda heshima yake na kupendwa na mamilioni ya watu mpaka siku anafukiwa pale Kihonda mjini Morogoro.

Mioyo na hisia za watu kuhusu Ngwair, anahesabika kama mwanamuziki wa kizazi kipya ambaye hakuwahi kutokea na hatotokea wa aina yake. Fid Q hakuwa mjinga kurudia upya ‘vesi’ yake kwenye wimbo wa CNN.

Lakini pamoja na hayo hakuwa peke yake. Na isingewezekana kila siku tusikie nyimbo zake zilezile wakati hana ngoma mpya. Na iko wazi kuwa msanii anayetoka anakuwa na hasira nyingi kuliko aliyetoka tayari.

Mana’ake ni kwamba mizuka ya Ngwair wakati anatoka kwenye gemu ni tofauti na baada ya kupata jina. Alikuwa mkali lakini, hakukaza kama mwanzoni. Hapa stresi zinahusika sana.

Pia kibiashara redio na runinga haziwezi kupiga nyimbo hizohizo kila mwaka. 2004 wakati Mikasi ikitoka ni tofauti na 2013, wakati uhai wa Ngwair unatutoka.

Wanamuziki wengi wa Kibongo wakishapata umaarufu mkubwa kuna kitu wanapoteza. Wanaupokea umaarufu kwa mbwembwe nyingi na wanatumia kiwango kilekile katika kuupoteza na kuacha juhudi ya kazi. Wanajisahau.

Kama redio zinapiga sana nyimbo za msanii aliyefariki dunia ni suala la kushukuru kama siyo kupongeza. Ni sawa na mizinga 21 kwa mwanajeshi aliyefariki anapozikwa. Dunia nzima iko hivyo.

Siku chache kabla ya kifo cha Michael Jackson hakuna aliyemuongelea wala kusikiliza muziki wake. Hakuna mahojiano wala tuzo aliyopewa kwa muda mrefu.

Lakini baada ya kifo chake aliongelewa kuliko miaka yote aliyodumu kwenye muziki. Kila runinga, redio, magazeti na mitandaoni aliongelewa yeye.

Mauzo ya albamu zake yalianza upya. Nyimbo zake za kitambo hicho zilipigwa kila wakati kana kwamba nd’o zinatoka. Lakini hakuna aliyelalamika kama huku kwetu kuwa mbona wanapiga nyimbo zake baada ya kufa?

Hatukusikia staa wala shabiki ndani ya Marekani aliyelalamika kuwa redio na runinga zinaanza kupiga nyimbo za Michael baada ya kifo chake. Hii akili ipo mitaa hii ya Mwananyamala tu huku kwetu.

Dunia nzima staa anapofariki vyombo vya habari vitamuongelea mpaka vitakapotosheka. Huku wanasema anaanza kupigiwa nyimbo zake baada ya kufariki dunia.

Hizo nyimbo zake zenyewe zilijulikana kupitia redio na runinga hizohizo. Alipata umaarufu kwa kutajwa na mahojiano na hizo redio na runinga. Lakini huwezi kuwa unapigiwa nyimbo zako na kuongelewa wewe tu kila siku.

Ni Kanumba tu ambaye alifariki akiwa kwenye kilele cha umaarufu mkubwa. Mafanikio makubwa na kazi zake nyingi zikiwa mtaani kwa wakati huohuo.

Ngwair licha ya kutuacha ghafla hakuwa kwenye kilele cha umaarufu mkubwa. Hakuwa na kazi nyingi mtaani kwa daraja la Kanumba na filamu zake. Ngwair alibebwa na ubora wake kwa ujumla toka anaanza muziki.

Kama ilivyo kwa Ngwair naye Sam wa Ukweli amefariki kipindi ambacho hana kazi kali mtaani. Ndiyo maana hakusikika sana mwishoni mwa uhai wake kama ilivyokuwa kwa Ngwair.

Hata safari yake ya Afrika Kusini alikofia ilijulikana kwa wengi baada ya kifo. Uwezo wake kisanaa, mazingira ya kufa kwake ilikuwa lazima kifo kiwe rafiki na vyombo vya habari.

Hata Sam wa Ukweli kifo chake kimemrejesha kwenye masikio ya watu. Sasa badala ya kuongelea mambo mazuri aliyokwishafanya wao wakajikita kwenye neno ‘kubaniwa’.

Inafika wakati malalamiko yanakuwa makubwa kana kwamba ndiyo chanzo cha kifo chake. Kama ilivyokuwa kwa Ngwair ikawa kama mauti yake yametokana na kubaniwa kwa nyimbo zake.

2Pac alikuwa maarufu, lakini kifo chake kikampa umaarufu zaidi. Mauzo ya albamu zake yakapanda na kila chombo cha habari kilimuongolea yeye.

Tusishangae kifo cha staa kuongelewa, kitu cha kushangaa ni siku staa akifariki dunia bila kuongelewa na vyombo vya habari. Hicho kitakuwa kitendo cha kuhoji na kuzua mjadala.

Kila mwanadamu mara nyingi huwaza jinsi ya kuibadili dunia, lakini ni ngumu kumuona akifikiri namna ya kujibadili yeye mwenyewe. Pale unafikiri upo sawa au haupo sawa, maana yake uko sawa.

Eid Mubarak.

Columnist: mwananchi.co.tz