Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Dunia inataka kurejea tulikokuwa zamani

15152 Fredy Macha TanzaniaWeb

Sun, 2 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Juma lililopita tulitaja baadhi ya maajabu yanayoisibu dunia yetu leo. Kama watu kujibadili kuwa siyo wanaume au siyo wanawake. Haya ndiyo huchangia kutufanya baadhi yetu wanadamu kuongelea ETI “mwisho wa dunia.” Wapo wanaopitisha kila nukta kuhubiri dhana hii. Nimewasikia miaka yangu yote 63 niliyoishi.

Ndiyo, maendeleo ya teknolojia yamerahisisha maisha na pia yametudondoshea wazimu.

Wimbi la kubatilisha vyakula asilia linaloendelea kulikabili Bara la Afrika ni moja ya ulaghai unaonezwa na wafanyabiashara walafi.

Huku Majuu, Wazungu wameshazinduliwa na kilimo hiki cha kugeuza uasilia wa mifugo na mimea uitwao GMO. Baadhi ya wafanyabiashara wamerejea mazao na nyama asilia na upinzani dhidi ya GMO ni mkubwa sana. Baadhi ya madhara ya GMO (Genetically Modified Organisms) yanafahamika, mengine bado. Kwetu Tanzania athari za kula kuku waliofugwa majuma machache zinaanza kuonekana. Maradhi ya ajabuajabu yanaendelea kustawi. Wengi bado hatujaamka.

Tunadhani ni USASA...

Hapa London baadhi ya maduka yanalazimisha kuuza Unga wa Iwisa toka Afrika Kusini ambao ni GMO. Waafrika wengi hata wanaoishi Uzunguni bado hawajui tatizo wanaUSHABIKIA. Ukizunguka London utakuta unga wa dona usiotumia GMO. Lakini si wengi tunaojali. Sayari yetu ina kila kitu kizuri.

Wapo wanadamu wanaozungumzia umuhimu wa kujali tunakula nini na kuthamini afya zetu kimwili na kiroho. Si vizuri tukainua mikono juu tukijisabilia kwa Muumba Wetu kuwa yeye tu ndiye mwamuzi wa kila kadhia. Kazi kuu ya Mungu ni kutubariki na kutulinda. Ila sisi wenyewe twahitaji kuamka na kuchapa kazi.

Mkondo mojawapo wa kiafya unazungumziwa na Mhindi ambaye ni mwalimu wa Yoga kutoka India, Sathguru.

Anadai uhai umegawanyika sehemu mbili. Usiku na mchana. Hapana na Ndiyo. Juu na chini. Kukataa na kukubali. Njaa na shibe. Mwanaume na Mwanamke. Kuwepo kadhia hizi pacha, anadai mwalimu huyu wa Yoga, Sathguru ndiko kunakotukumbusha maana ya kuishi.

Mvutano wake ndiyo unaotusumbua na kutujenga. Uhai ulipoanza mivutano hii ilikaa pamoja. Sathguru mwenye umri wa miaka 60, anatukumbusha tuwatazame ndege wakiruka. Anadai huwa wawili wawili. Na hawasemi tukafanye ngono.

Ila sisi tukiona mwanamke na mwanaume tunafikiria ngono. Umaana wa ndege hawa wawili ni uhai; kuruka pamoja, kuwepo pamoja na matokeo yake kulala pamoja ili kuwepo uwezekano wa kutaga mayai, kucheza, kujenga viota, kuimba, kupigana na kadhalika. Anasema tukiwa vijana homoni zinafukuta, joto linatupanda na tunachofikiria ni kimoja tu, ngono. Tukishakua huwaza zaidi mapenzi. Tukizeeka tunatafuta umaana wa maisha na uwezekano wa kukutana na utakatifu na Mungu.

Kifupi basi mikondo inayoanza kuchipuka ni kurejea tulivyokuwa zamani. Kabla ya biashara na uroho wa kampuni kubwa za ulafi na fedha. Hapa basi yapo matumaini kuwa teknolojia, uroho na biashara havitautokomezea ulimwengu wetu. Si kweli eti mwisho wa dunia umefika. Waovu wanaotuangamiza ndiyo watakaofikia ukingoni mwa maisha.

Columnist: mwananchi.co.tz