Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla alitumia siku 24 kufanya ziara katika maeneo mbalimbali nchini kushughulikia masuala ya wizara yake kabla ya kupata ajali Agosti 3 mkoani Manyara.
Katika siku hizo 24, Dk Kigwangalla kwa kutumia gari, alitembea kilomita takribani 7,074 akiwa na wasaidizi wake.
Dk Kigwangalla ambaye anaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, aliambatana katika ziara hiyo na ofisa habari wa wizara yake, Hamza Temba ambaye ndiye aliyekuwa akitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya kile alichokuwa akifanya katika maeneo mbalimbali nchini.
Temba ndiye abiria pekee aliyefariki katika ajali hiyo iliyotokea Agosti 4 eneo la Vilima Vitatu wilayani Babati, walipokuwa wakitokea Arusha kuelekea Dodoma.
Mwananchi limetumia taarifa zilizokuwa zikitumwa kwa vyombo vya habari na Temba wakati uhai wake katika kuangalia umbali ambao Dk Kigwangalla alimbea tangu alipoanza ziara yake mkoani Dodoma Juni 22.
Juni 22, Temba alituma taarifa akieleza kuwa Dk Kigwangalla ametoa siku 30 kwa wananchi waliovamia Pori la Akiba Swagaswaga, Dodoma na kuendesha shughuli zao ikiwamo kilimo, makazi na ufugaji kinyume cha sheria waondoke mara moja kwa hiari yao kabla ya kuondolewa kwa nguvu.
Baada ya kutoa agizo hilo Juni 24, Dk Kigwangalla alisafiri takriban kilomita 427 (kama alipitia Kondoa) kwenda Arusha kwenye mkutano wa Itifaki ya Utalii na Usimamizi wa Wanyamapori katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC).
Taarifa ya Temba kwa vyombo vya habari ilieleza jinsi kulivyokuwa na mjadala mzito na mabishano makali katika Mkutano wa Nane wa Kisekta wa Baraza la Mawaziri wa jumuiya hiyo.
Alieleza kuwa mvutano huo ulisababishwa na hoja iliyowasilishwa na Tanzania ambayo ilitaka kuboreshwa kwa kifungu cha nne cha itifaki hiyo ambacho kinazitaka nchi wanachama kutangaza eneo lote la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kama kituo kimoja cha safari za utalii duniani.
Baada ya mkutano huo, Dk Kigwangalla alitumia kilomita hizohizo 427 kurejea Dodoma ambako Juni 26 alifungua warsha ya siku moja ya wadau wa kitaifa kupinga vitendo vya uhalifu dhidi ya wanyamapori na misitu. Akiwa Dodoma, Juni 28 alipokea taarifa ya kamati ya Suleiman Kova kuhusu mauaji ya tembo katika Ikolojia ya Ruaha Rungwa.
Julai Mosi, Dk Kigwangalla alikuwa Songwe (umbali kati ya Dodoma na Songwe ni kilomita 662) ambako Temba aliripoti kuwa waziri huyo alitoa wito kwa wadau wa utalii wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuweka juhudi za pamoja na kushirikiana na Serikali katika kuendeleza na kutangaza vivutio vya utalii vya kanda hiyo ili viweze kunufaisha zaidi wananchi na Taifa kwa ujumla.
Akiwa Songwe pia Julai 2, Dk Kigwangalla alitoa miezi mitatu kwa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri) kufanya utafiti na sensa ya mamba katika Ziwa Rukwa ili kubaini idadi yake na hatimaye kuishauri Serikali namna ya kudhibiti madhara wanayosababisha kwa wananchi.
Aliondoka Songwe na Julai 3 kwenda Chunya mkoani Mbeya (zaidi ya kilomita 140) ambako alitoa onyo kali kwa wananchi wanaojihusisha na vitendo vya uchimbaji wa mchanga wa madini ya dhahabu (makinikia) ndani Hifadhi ya Msitu wa Palamela.
Julai 4 taarifa ya Temba ilieleza kuwa Dk Kigwangalla akiendelea na ziara yake Mbeya alikagua shughuli za uhifadhi katika Pori la Akiba Mpanga Kipengere ambalo lipo katika wilaya za Mbarali (Mbeya), Makete na Wanging’ombe (Njombe).
Siku hiyohiyo alielekea wilaya ya Makete mkoani Njombe kwenye maporomoko ya Mto Kimani.
Alitoka Njombe na kuelekea Rukwa (kilomita 544)ambako Julai 5 aliagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuchangia Sh20 milioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Mponda, Sumbawanga.
Akiwa Rukwa alienda Nkasi ambako Julai 6 alitangaza kiama kwa wafugaji wanaoingiza mifugo kwenye maeneo ya hifadhi nchini na kusema kuanzia sasa yeyote atakayekamatwa, mifugo yake itataifishwa kwa mujibu wa sheria.
Alitoa tamko hilo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Lyazumbi kinachopakana pori la akiba la Lwafi.
Alitoka Nkasi na kuelekea Kalambo ambako Julai 7 alimuagiza katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha Taasisi za Uhifadhi wa Wanyamapori pamoja na TFS wanashirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kutengeneza vikundi vya wananchi wa vijiji vyote vinavyopakana na Hifadhi ya Msitu wa Kalambo na Pori la Akiba Lwafi ili wawezeshwe mikopo ya mizinga ya kufugia nyuki ambayo wataipanga pembezoni mwa mashamba yao ili kuzuia tembo kuingia kwenye mashamba.
Julai 8 aliporejea Sumbawanga akiwa hapo, aliwasimamisha kazi maofisa na askari wanyamapori wote 27 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) katika Pori la Akiba Uwanda akiwamo Kaimu Meneja, Lackson Mwamezi kwa kushindwa kusimamia vizuri pori hilo na kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa.
Baada ya hapo alielekea Katavi (kilomita 309) kukagua moja ya eneo la chanzo cha maji yanayozalisha maporomoko ya Nkondwe ambayo ni kivutio cha utalii katika Wilaya ya Tanganyika. Hiyo ilikuwa Julai 10.
Alienda Wilaya ya Mlele na Julai 11 na akiwa huko aliagiza Polisi mkoani Katavi kumkamata na kumfungulia mashtaka Mkuu wa Kanda - Pori la Akiba Rukwa, Emannuel Barabara kwa madai ya uhujumu uchumi.
Dk Kigwangalla alichanja kilomita 652 kuelekea Bunda mkoani Mara kutafuta ufumbuzi wa kilio cha muda mrefu cha wananchi wa wilaya hiyo katika ukanda unaopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuhusu tembo kuvamia makazi na mashamba yao.
Pia, aliiagiza Tanapa kushirikiana na TFS kuanzisha mradi wa ufugaji nyuki kwa vijiji 10 vinavyopakana na hifadhi hiyo ili watumike kama uzio wa kudhibiti wanyamapori hao.
Alitoka Bunda kuelekea Tarime (kilomita 195) ambako Julai 17 aliagiza Polisi Wilaya ya Tarime kumkamata na kumfungulia mashtaka Katibu wa UVCCM wa wilaya hiyo, Newton Mongi na Mjumbe wa Kamati ya Siasa, Richard Tiboche kwa tuhuma za kuitukana Serikali na kuchochea mgogoro wa mpaka kati ya Hifadhi ya Serengeti na vijiji jirani.
Baada ya Tarime aliendelea na ziara yake Busega mkoani Simiyu na kuwapa siku 45 wananchi wanaoishi kinyume cha sheria ndani ya kingo (bufer zone) za Pori la Akiba Kijereshi kuondoka kwa hiari yao kabla ya kuanza operesheni ya kuwaondoa kwa nguvu.
Alipita Meatu Julai 20 na kuangalia mandhari ya Pori la Akiba Maswa lililopo Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu
Julai 22 alikuwa Tabora (akiwa ametembea wastani wa kilomita 302) na kuagiza Mfuko wa Ruzuku wa Misitu Tanzania (Taff) kwa kushirikiana na TFS kuanzisha mradi wa viwanda vidogo vya kusindika na kufungasha asali katika mikoa ya Tabora na Katavi ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kujenga uchumi wa viwanda.
Alielekea Kigoma umbali wa kilomita 412 na Julai 26 aliagiza wavamizi wote waliopo ndani ya Pori la Akiba Kigosi/Moyowosi na Hifadhi ya Msitu wa Makere mkoani humo waondoke mara moja ili maeneo hayo yaendelee kuhifadhiwa kwa mujibu wa sheria.
Aliingia Geita (kilomita 475) Julai 28 na kuiagiza kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzam 2000 iliyokuwa ikifanya utafiti wa madini ya dhahabu katika eneo la Luahika ndani ya Pori la Akiba Moyowosi/Kigosi kuondoa vifaa na mitambo yake ndani ya siku saba.
Aliondoka Geita na Julai 31 alikuwa Dar es Salaam (kilomita 1,105) ambako alisema Serikali itatumia fursa ya ujio wa mcheza Golf mashuhuri duniani, Jack William Nicklaus kutoka Marekeni kubuni viwanja vya mchezo huo karibu na maeneo ya vivutio vya utalii nchini ili kuvutia watalii wengi wa kimataifa na hivyo kukuza pato la sekta hiyo.
Hiyo ilikuwa taarifa ya mwisho ya Temba kwa vyombo vya habari kabla ya kuelekea Arusha (kilomita 624) akiwa na Dk Kigwangalla alipokuwa na mkutano na wadau wa utalii uliofanyika Agosti 3 kabla ya kupata ajali mkoani Manyara akiwa ametembea kilomita zipatazo 166.