Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Diplomasia ya uchumi itakuacha huru na 666

Mon, 20 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni Jumapili nyingine yenye baraka katika mwaka huu. Naendelea kukuombea uwe mwaka wa mafanikio tele kwa sababu tunakaribia kufikia nusu mwaka.

Neno la Mungu leo litaongozwa na kichwa cha habari kinachosema Diplomasia ya Uchumi.

Biblia katika kitabu cha Ufunuo wa Yohana 13:16-18 inaandika: “Naye awafanya wote wadogo kwa wakubwa, matajiri kwa maskini, walio huru kwa watumwa ili wote watiwe alama kwenye mkono wao wa kulia au kwenye paji la uso wao, na ili yeyote asiweze kununua au kuuza isipokuwa mtu aliye na ile alama, jina la yule mnyama wa mwituni au namba ya jina lake. Hapa ndipo hekima inapohitajiwa:

“Yule aliye na ufahamu na afanye hesabu ya namba ya yule mnyama wa mwituni, kwa maana ni namba ya mwanadamu, na namba yake ni 666.”

Unaposoma maandiko haya katika kitabu hiki cha ufunuo na unapohusianisha na kichwa cha mahubiri ya leo ya Diplomasia ya Uchumi unaweza kujikuta ukijiuliza maswali mengi.

Mfano wa maswali utakayojiuliza ni kama hili. Je, nani anaitawala dunia hii? Ni Mungu, Mwanadamu au shetani? Na baada ya hili swali unaweza kukosa jibu au ukapata jibu lisilo sahihi.

Pia Soma

Ukiwa kama Mwanadamu ambaye umeumbwa na Mungu unapaswa kutafakari kwa kina jambo hili ili umjue ni nani hasa anayetawala ulimwengu huu tunaoishi.

Inashangaza sana kuona kwamba kuna mambo yanayotendeka katika ulimwengu huu huku watoto wa Mungu wakiwa wametiwa upofu, hawaoni wala hawatambui namna akili zao zinavyovurugwa na shetani na kukosa ufahamu juu ya mamlaka ya Mungu aliyoiweka kwao.

Mungu amewapa wanadamu mamlaka ya kutawala na kumiliki. Kwa maana nyingine, mwanadamu anao uwezo wa kumiliki kitu chochote kilicho duniani kisha kukitawala vinginevyo mamlaka hiyo itachukuliwa na shetani.

Mungu amempa mwanadamu maarifa na katika maisha lazima ajue namna ya kutumia maarifa aliyopewa ili shetani asije akajitwalia utukufu.

Katika kitabu cha Mathayo 4;8-11 Biblia inasema: “Tena Ibilisi akampeleka Yesu kwenye mlima mrefu sana, akamuonyesha falme zote za ulimwengu na utukufu wazo. Naye akamwambia:

“Nitakupa vitu hivi vyote ukianguka chini na kunifanyia tendo la ibada.”

Ndipo Yesu akamwambia: “Nenda zako, shetani! Kwa maana imeandikwa: “‘Yehova’ Mungu wako ndiye unayepaswa kumwabudu, na yeye peke yake ndiye unayepaswa kumtolea utumishi mtakatifu.” Ndipo Ibilisi akamwacha, na tazama! malaika wakaja na kuanza kumhudumia.

Baada ya kuwekwa katika huduma yake ya umasihi Yesu alijaribiwa na shetani. Nia ya shetani ilikuwa kutaka Yesu atumie mamlaka yake vibaya, ukweli ni kwamba shetani hana chochote anachomiliki.

Hii jeuri aliyoipata ya kumuamrisha Yesu kuwa atampa miliki ya vitu vilivyo duniani anaitoa wapi?

Kumbuka katika kitabu cha Mwanzo mwanadamu ndiye aliyepewa kumiliki na kutawala, lakini shetani alipomdanganya Adam na Hawa ndiyo akapora ile mamlaka. Kwenye kitabu hiki cha ufunuo mnyama hapa anawakilisha matendo yatendwayo na adui shetani.

Roho wa nabii wa uongo siku zote yupo duniani kwa sababu ya falsafa ikaenea hadi Rumi, ikawa taasisi, ikaenea Ulaya ikawa utamaduni na ikafika Amerika ikawa shughuli kama biashara vile.

Ukweli ni kwamba Ukristo si biashara, ajenda iliyopo duniani leo hii na inayoendeshwa kwa siri ni kutumia alama hizi za kishetani kumtawala Mwanadamu kiuchumi.

Kazi hii inafanyika kupitia alama kama fedha na hata siasa. Taasisi kubwa za za kidunia hutumika pia zikitawala nchi changa.

Leo Mungu ameamua kukupatia ufahamu huu kupitia neno lake.

Neno la Mungu linasema ikiwa watu wangu walioitwa kwa jina langu watajinyenyekeza na kuomba na kunitafuta uso na kuziacha njia zao mbaya, basi nitasikia kutoka mbinguni na kuwasamehe dhambi zao na kuiponya nchi. 2 Nyakati 7:14. Tunapaswa kunyenyekea kwake na kuutafuta uso wake kwa bidii ili atuponye na mambo yote maovu yanayojitokeza duniani.

Basi Mungu atusaidie katika suala hili la diplomasia ya uchumi ili tusikumbwe na namba hii ya kishetani yaani 666. Nakuombea baraka za Mungu ziwe nawe na akuepushe na matumizi ya namba hiyo ya kishetani

Mungu anaweza kukufanikisha kwenye kila jambo unalofanya ikiwa utaziacha njia zako mbaya nawe utarejea kwake na kuomba msamaha na kutubu kweli kwamba umekosa. Mungu yupo upande wako siku zote.

Columnist: mwananchi.co.tz