Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Diamond; ujana, mafanikio na matatizo ni pacha

Sat, 22 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Anaitafuta miaka 30 sasa. Ni umri mdogo sana kwa Afrika. Ana kila kitu anachoota kumiliki kijana. Ndinga kama zote. Mijengo kama ugomvi. Anapasua anga kuzunguka dunia kila siku. Ana lundo la warembo wazuri. Ni maarufu sana na zaidi ana wafuasi wanaompenda.

Shetani ni maarufu lakini hapendwi. Ndivyo ilivyo kwa Hitler na wendawazimu wengine kama Idd Amin. Umaarufu bila kupendwa hauna maana. Kuwa kijana mdogo mwenye ukwasi, maarufu na unapendwa ni jambo moja. Kudhibiti hulka na mihemko ya ujana na kiburi cha pesa ni jambo lingine.

Narudia tena ogopa sana kijana mdogo maarufu anayependwa. Chochote anachofanya au kusema kinageuka dhahabu. Kina Michael Jackson wakaishia kujibadili rangi na sura kutaka kufanana na mwanadada Diana Rose. Kule ni kushindwa hudhibiti mihemko ya ujana, ‘ustaa’ na utajiri chekwa.

Kina Mike Tyson wakaishia kufilisika kindezindezi tu. Walishindwa kudhibiti ujana wenye umaarufu na mafanikio makubwa. Ni wachache sana wanaopata mafanikio ujanani wakazeeka katika utulivu ule ule. Waheshimu watu kama ‘brazameni’ Will Smith. Usimchukulie poa ‘bishoo’ kama David Beckham. Ni kazi ngumu kuishi katika utulivu ule walionao toka ujanani.

Unashangaa Diamond kwa alichofanya kwa wale ‘stafu’ wa ATCL pale Mwanza? Mimi ningekuwa katika daraja la mafanikio ya Diamond, huenda ningewatandika makofi. Niko na ‘baunsa’ walio tayari kufa kwa ajili yangu. ‘Stafu’ wa airport utaniambia nini? Makofi ‘mkurabita’ yenye ‘mkukuta’ yangewahusu.

Nimechelewa kuripoti airport ya Mwanza? Kwa nini nisichelewa pale Heathrow airport, London town nikipita zangu kwenda JF Kennedy airport, New York City? Usinitanie wewe. Kila siku nadondoka Oliver Thambo airport, kuwatembelea wanangu Tiffah na Nillan, itakuwa Mwanza hapa? Acheni kunitania.

Wazee waliokula bata hata kabla ya vita vya Idd Amin, wakipata kiinua mgongo leo wanawehuka. Itakuwa mtoto wa kitaa mwenye makuzi ya Tandale? Miaka michache nyuma nikiwaonea wivu wanaoishi Sinza. Leo namiliki mjengo ‘Sauzi’ utaniambia nini? Tusilaumu sana, pesa inaleta ugonjwa wa kujiamini.

Pamoja na yote Chibu ana tofauti. Ameweza kwa kiasi kikubwa kudhibiti mihemko ya ‘ustaa’ na mafanikio ya ujanani. Tusiongelee kama kijana mpenda ‘vicheche’ tukisahau kabisa milioni 68 aliyoacha Sumbawanga huko kwa ajili ya ujenzi wa shule. ‘Vicheche’ vinalazimika kumpenda msela kwa sababu ya mkwanja mrefu.

Usawa huu kuacha 68 milioni sehemu ambayo huna hata ndugu wala mchepuko. Ni zaidi utajiri aiseee. Bali ni moyo wa kutoa. Siyo kila mtu mwenye uwezo ana moyo huo wa kutoa. Lakini watu wanachukulia poa poa huku wakidhani kuwa ni ‘kiki’ kama ‘kiki’ zingine. Kizazi cha nyoka hiki.

Tusikariri anavyobadili totoz na vituko vyake mitandaoni. Huku tukijifanya viziwi wenye upofu wa kutoona na kusikia alichomfanyia yule dada (Hawa), aliyeimba naye wimbo wa Nitarejea. Kumuokoa na kifo kwa kumsafirisha mpaka India kutibiwa.

Hakumpeleka Muhimbili hapo. Milioni zaidi ya 50 mchizi aliipangua kiroho safi kwenye akaunti yake. Hawa akapaa na mwewe mpaka India. Akalipia usafiri. Malazi. Matibabu na kila kitu kwa mgonjwa na walioongozana naye. Milioni 50 kiasi hicho hicho kinalipwa kimafungu mwaka mzima kwa mshindi wa Bongo Star Search mwaka huu.

Alikwenda mitaa aliyokulia Tandale. Akamwaga bodaboda na bajaji kama zote kwa vijana kibao na wajane. Mpuuzi mpuuzi huko uliko unaweza kuona jambo la kawaida.

Alichangia madawati 600 kwa shule za Daslama. Haya hayaonekani wala kusikika kwenye macho na masikio ya kizazi cha nyoka. Wao wapo maalumu kwa ajili ya kusikiliza kelele za madem zake mitandaoni.

Hizi pesa anazotoa Diamond kwa matibabu, madawati na ujenzi wa shule. Miaka ile Mr Nice, Ferouz na wenzao walizihifadhi kwenye meza za baa mjini. Mastaa wa zamani wa muziki pesa zao zilituama kaunta za Billz, Kwa Macheni, Kona Baa. Na kwenye’ vigesti’ na hotel za mjini.

Ni kama kanuni tu kwamba watu watakupa utajiri kwa kununua kazi zako. Pale tu unapofanikiwa hawataki uwe kiburi wala mjivuni. Hutaka waone mnyenyekevu ‘deile’. Ni jukumu zito ambalo wengi limewashinda. Binadamu wengi kubadilika ghafla kwa umaarufu na mafanikio ni jambo la asili.

Hata kama atajificha, kile kiburi cha siri hubaki nacho. Anapoonyesha unyenyekevu ni maigizo tu. Chibu atambue hakuna mtu hapa Bongo asiyejua kuwa yeye ni staa mwenye mafanikio. Kile ambacho anaweza kukifanya au kukitamka kwa namna ya kujikweza, kitatafsiriwa kuwa sababu ni mafanikio yake.

Hii ni kwa yeyote unapokuwa na mafanikio kimaisha. Lazima uwe makini kwa vitendo na maneno yako. Chochote cha kufanya au kusema huunganishwa na mafanikio yako. Kinaweza kufanywa na mtu wa kawaida ikawa poa tu, kikifanywa na mwenye mafanikio inageuka shida mjini.

Wadau wengi wa muziki na wanamuziki hawampendi Chibu. Hakuna zaidi ya kuona anaringia mafanikio yake. Ni juu yake kuwa mwangalifu. Anaweza kutamka neno au kufanya jambo kwa nia njema. Watu kwa kutoelewa au kwa makusudi wakalazimisha iwe kama dharau. Tusi. Kebehi. Majivuno au kujikweza.

Wakati taarifa za afya ya Hawa zikisambaa mitandaoni. Baadhi walimlaumu Diamond. Kana kwamba kamtelekeza mtu aliyetoka naye mbali. Kumbe hakuwa na taarifa. Alipotangaza kumsaidia, watu wale wale kizazi cha nyoka wakaanza kusema Chibu analeta “show off’.

Leo hii dogo na dogo mwenzake Rayvanny wamefungiwa na Basata. Kutofanya muziki ndani na nje ya nchi kwa muda usiojulikana. Kwa kosa la kukiuka maamuzi ya Basata kuufungia wimbo wao wa Mwanza. Inadaiwa waliimba wimbo huo kwenye moja ya matamasha yao ya Wasafi Festival.

Kibaya zaidi hata tamasha la Wasafi Festival ambalo linajumuisha wanamuziki wengi nalo limesimamishwa kama siyo kufutwa. Hakuna neno sahihi zaidi ya ‘kukomoana’. Tamasha linahusika vipi na upuuzi wa watu wawili?

Kumzuia mwanamuziki asifanye kazi ya muziki ndani na nje ya nchi ndio nini? Basata majukumu yao yanafika mpaka Harare? Nairobi? Comoro na Lagos? Maadili yanayolindwa Ilala Sharifu Shamba, yanahusika vipi na maadili ya Shimoni Mombasa?

Basata adhabu yao ni kubwa mno hata kwa wasiohusika. Na wanaounga mkono ndo walewale ‘Kizazi cha nyoka’. Hawaoni jema lolote kwa msela wa Tandale. Na madogo ‘kupafomu’ wimbo uliopigwa marufuku na Basata ni tatizo la mihemko ya ‘ustaa’ mafanikio na kupendwa sana.



Columnist: mwananchi.co.tz