Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Demokrasia sawa, lakini tutafakari gharama zake

12092 MUSA+JUMA TanzaniaWeb

Wed, 15 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tanzania ni moja ya mataifa yanayoendelea ambayo uchumi wake unaelezwa kukua kwa kasi.

Jitihada za kukuza uchumi ambazo zinafanywa na Serikali na wadau wengine zinapaswa kuungwa mkono na Watanzania wote.

Hata hivyo, naamini katika safari ya Tanzania mpya, kuna changamoto ambazo sasa zinapaswa kufanyiwa kazi, ili kutorejesha nyuma jitihada kubwa ambazo zinaendelea kufanywa.

Inawezekana kisiasa ikawa ni fursa ya kujiimarisha lakini, kiuchumi na kijamii jambo linaweza kuwa na athari hasa katika mikakati ya kushughulika na matatizo na kero za wananchi.

Hivi sasa katika taifa letu kuna wimbi na wanasiasa kuhama vyama, jambo hili lina sura kadhaa kwanza ile ya kuunga mkono serikali, kuna sura ya ushawishi na kuna sura ya uchu wa madaraka kwa wanaohama.

Ni ukweli kuwa katika mchakamchaka wa maendeleo unaoongozwa na Rais John Magufuli, wapo wanaomuunga mkono na baadhi ya wanasiasa wanahama vyama na kujiunga naye.

Lakini, kushawishiwa kwa wanasiasa na kuahidiwa fursa nyingine pia kunaweza kuchangia baadhi yao kuhama vyama vyao na kuzikimbilia fursa.

Katika hamahama hii ya wanasiasa, pia kuna taarifa kuwa baadhi yao, wameanza kuona mwaka 2020 hawawezi kutetea nafasi zao hivyo kuamua kusaka huruma ili kutetea mikate yao.

Hata hivyo, sababu zote nilizotaja ama zaidi ndio demokrasia yenyewe kwani kila mtu ana haki ya kujiunga na chama chochote cha siasa ama kuhama chama bila kubughudhiwa.

Lakini tujiulize, je, hamahama hii ina faida kiasi gani kwa wananchi masikini wa mijini na vijijini?

Je, wanaotaka kuungana na mchakamchaka wa maendeleo, hawawezi kubaki walipo na kujitangaza hadharani hawataki siasa ambazo zinapingana na maendeleo?

Hawa wanaohama hawezi, kuwa na subira hadi 2020 wakaibuka hadharani na kuepusha gharama za uchaguzi kurudiwa.

Gharama za uchaguzi wa jimbo moja ni inakaribia Sh1 bilioni na gharama ya kata moja katika uchaguzi wa diwani inakadiriwa kufikia Sh200 milioni naamini fedha hizi ni nyingi sana.

Tunashuhudia hivi sasa katika harakati za uchaguzi, viongozi wa serikali, halmashauri na vyama vya siasa, wanatumia muda mwingi kwenye kufuatilia kampeni na chaguzi.

Kama nilivyosema awali kinachotokea ndio ukomavu wa demokrasia lakini narudia tena ni muhimu kutafakari athari nyingine za kiuchumi na kijamii.

Katiba ya Tanzania inatoa uhuru wa kidemokrasia na si rahisi kufanya mabadiliko ili kuwa na mfumo mzuri wa kuruhusu hamahama bila kuturudisha nyuma, lakini jambo hili linapaswa kutoa funzo ili kupata njia mbadala ya kuruhusu hamahama bila kuathiri uchumi na maisha ya Watanzania masikini.

Katika Rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba, wananchi waliliona hili na walitoa mapendekezo kadhaa ambao sasa ni fursa ya kuyapitia na kuyafanyia kazi.

Mapendekezo ya wananchi yalilenga kupunguza gharama za michakato ya kampeni na uchaguzi lakini pia kuhusiana na sifa za wanasiasa wetu, wananchi walitoa mapendekezo hadi viwango vya elimu vinavyotakiwa.

Itoshe kutoa wito kuomba wahusika hata kama wanadhani ni haki yao kidemokrasia, lakini waangalie gharama zinazotumika ili kuwaepusha wananchi kubeba mzigo wasioustahili.

Columnist: mwananchi.co.tz