Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Dalili za watu wanaotaka kujiua

11443 Kujiua+pic TanzaniaWeb

Sun, 15 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jambo kubwa ambalo limeshtua na kuwashangaza watu ni kuona polisi watatu nchini wakijiua kwa kujipiga risasi ndani ya saa 48.

Huo ni mfululizo wa matukio ya aina hiyo ambayo yamekuwa yakitokea nchini na duniani kwa ujumla, lakini kwa ujumla idadi ya watu kujiua imekuwa ikiongezeka siku hadi siku.

Shirika la Afya Duniani (WHO), limetoa ripoti inayoonyesha kuwa kila mwaka zaidi ya watu 800,000 hujiua duniani huku wengi wakifanya jaribio hilo.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa kitendo cha watu kujiua hutokea katika rika zote bila kujali umri na kwamba mwaka 2015 tu, kujiua kulishika nafasi ya pili kwa vifo vyote duniani hasa kwa vijana wa miaka 15-29.

Ripoti hiyo ambayo inataja kitendo cha watu kujiua kama janga linalohitaji kushughulikiwa haraka, inaonyesha kuwa vitendo hivyo hutokea katika mataifa karibu yote duniani bila kujali kipato, lakini asilimia 78 ya vifo vya aina hiyo hutokea zaidi katika nchi zenye uchumi wa chini na uchumi wa kati.

Mojawapo ya madhara ya watu kujiua ni kuacha matatizo katika familia kwa sababu vifo hivi huwa ni vya ghafla kwa hiyo huiacha familia bila kujiandaa na wakati mwingine hata taifa hupoteza nguvu kazi.

Ni mara ngapi, tumesikia matukio ya watu kujiua au kuua watu wengine. Je, zinaweza kupita saa 24 bila mtu kujiua popote duniani, haiwezekani.

Huenda sababu za watu kujiua zimeelezwa mara kwa mara, lakini je, unawezaje kumtambua mtu anayetaka kujiua. Wanasaikolojia na wanasosholojia wanasema kuna mambo ambayo ukiyaona kwa mtu akiyafanya mara kwa mara huenda ikawa ni dalili ya mtu kutaka kujiua, hivyo inakuwa rahisi kumpa msaada.

Mwanasosholojia, Dk Abunuas Mwami anasema kwa ujumla msongo wa mawazo ni sababu kubwa ya watu kufikia kujiua, lakini analaumu ubepari ambao umewafanya watu wafarakanishwe na jamii zao.

“Kabla ya ukoloni, jamii za Afrika zilikuwa pamoja, lakini sasa ubepari umefanya thamani ya mtu iwe katika vitu. Kama huna kitu thamani yako inapotea na hilo binadamu ameshindwa kulidhibiti kiasi kwamba watu wengi wanajiona wapowapo tu, hawana mamlaka na hilo limewafanya binadamu waonekane kama chombo cha kutumikisha zaidi,” anasema mstaafu huyo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Upweke

Mwanasaikolojia Modesta Kimonga anasema miongoni mwa dalili za watu wanaotaka kujiua ni upweke. “Mara nyingi watu wanaofikiria kujiua huwa wanakwepa muingiliano na watu wengine, hupenda kuwa wenyewe wakitafakari, wanapima uamuzi wanaotaka kuuchukua kama ni sahihi au si sahihi,” anasema Modesta.

Kukataa tamaa

Miongoni mwa dalili kubwa ya mtu anayetaka kujiua ni kukata tamaa. Hii si tu kuwa huwa ni dalili, bali pia ni sababu ya watu wengi kujiua kwa kudhani wametengwa na jamii zao au dunia kwa ujumla. Watu wanaoonekana wamekata tamaa hawatakiwi kuachwa wenyewe, kwani wapo kwenye hatari ya kujiua.

Dk Mwami anasema ubepari ambao umesababisha mtu kufarakanishwa na jamii yake umewafanya watu wengi kujiona hawana thamani na hivyo kukata tamaa ya maisha. “Mtu wa namna hii akipata tatizo dogo tu huamua kujiua kwa kudhani hana thamani.”

Mwanasaikolojia wa zamani wa Ufaransa, Emile Durkheim katika tafiti zake aligundua kuwa watu wanapodhani wametengwa kutokana na mabadiliko ya ghafla ama ya kijamii, kisiasa au kiuchumi huchanganyikiwa na kukataa tamaa hivyo kujiua.

Kuahirisha mambo

Watu wanaofikiria kujiua huwa hawataki kufikiria mambo ya mbele, hata kwa mambo ambayo tayari waliyapanga huwa wanaahirisha bila sababu ya msingi na wengine huwa wanaahirisha hata safari muhimu.

Modesta, ambaye ni mwalimu wa Chuo cha Elimu cha Patandi, tawi la Tanga anasema watu wanaofikiria kujiua pia huwa wanapenda kuahirisha mambo kwa sababu ya hasira ambazo zimetokana na uchungu uliosababishwa na watu, vitu au mazingira.

“Mtu anafikiria niwekeze kwa ajili ya nani, kinachomfanya kuahirisha mipango yake au uwezekaji si yeye ila ni uchungu kwa sababu anaamini kuwa jamii ndiyo imemjeruhi,” anasema Modesta.

Ukiwa na mtu wa aina hii hutakiwi kumuacha mwenyewe, badala yake unatakiwa kuwa naye karibu huku ukimpa maneno ya faraja.

Watu waliowahi kubakwa

Watu waliowahi kubakwa wasipopata ushauri wa uhakika huwa kwenye hatari kubwa ya kujiua. Sababu kubwa huwa ni kuona wamedharauliwa, wamedhalilishwa na zaidi wametengwa na kuonekana hawafai mbele ya jamii. Huwa na uwezekano wa kujiua kwa sababu ya kudhani kwa kufanya hivyo watakuwa salama zaidi.

Modesta anasema sababu nyingine ambayo huwaonyesha dalili za watu wanaotaka kujiua ni hasira na upweke na kwa mazingira yaliyopo ni rahisi watu waliowahi kubakwa kuwa na hasira na jamii na hata mara nyingi kuwa wapweke.

Kuandika wosia

Watu huandika wasia kwa sababu mbalimbali, mara nyingi katika nchi za Afrika, watu wengi (sio wote) huandika wasia wanapojua siku zao za kufa zimekaribia kutokana na uzee, ugonjwa au hatari nyingine yoyote iliyo mbele yao. Hata hivyo, wanasaikolojia wanasema watu ambao wanazungumza zaidi kuhusu kuandika wosia mara kwa mara wanapaswa kuangaliwa kwa makini kwa sababu wakati mwingine huwa ni dalili ya kutaka kujiua.

Mtu aliyewahi kutaka kujiua

Sababu za kutaka kujiua huwa haziishi kirahisi, zinachukua muda mrefu, kama sababu ni sonona huwa haitibiwi kirahisi wala kwa haraka, kwa hiyo kama kuna mtu amewahi kutaka kujiua ikashindikana kwa namna yoyote ile, huwa ni rahisi kutaka kurudia kufanya kitendo hicho kwa sababu zilezile za kwanza.

Aibu na kutoangalia usoni

Kama anavyosema Modesta kuwa watu wengi wanaotaka kujiua huwa wanataka faragha na kutotaka muingiliano na watu wengine, ni dhahiri kuwa mtu ambaye anataka kujiua huwa na aibu na hataki kuwaangalia usoni watu wengine. Wanajua kinachofuata na huwa hawapendi mtu agundue chochote.

“Watu hawa huwa wanatafakari mara kwa mara kama wanachokifanya ni kosa au si kosa, hujiona wakosaji,” anasema Modesta.

Mazungumzo ya kujiua

Kuna baadhi ya watu ambao hupenda kuzungumzia mara kwa mara kuhusu masuala ya kujiua au kuua watu wengine. Kuna baadhi huwa wanazungumza kama masihara huku wakisema wanataka kujidhulu au hawapendi kuishi duniani. Tena kuna wakati huwa wanataka ushauri na maoni kutoka kwa watu wengine kuhusu kujiua. Huwa wanajaribu kutafuta msaada, lakini huwa ni ngumu kwa watu wengine kuelewa. Wanasaikolojia wanaonya kuwa watu hawa wasichukuliwe kimasihara kwani huwa wamepania kufanya hivyo.

Wanasaikolojia kwa pamoja wanakubaliana kuwa watu wa kundi hili huwa wakipata tatizo kidogo na likachochea hasira zao, huwa wanajiua na hasa wanapoachwa pekee yao bila familia au marafiki. Inashauriwa kuwa mtu anayezungumza mara kwa mara kuhusu mauaji asiachwe mwenyewe.

Sonona na magonjwa ya akili

Maumivu yanayotokana na msongo wa mawazo au sonona na magonjwa ya akili pia ni dalili nyingine ambayo huwa kichocheo kikubwa cha watu kujiua. Ni rahisi kumjua mtu mwenye dalili kama hizo za kukata tamaa na msongo wa mawazo kutokana na vitendo vyake visivyo vya kawaida.

“Sonona ni ugonjwa unaoongoza watu kujiua, kwa hiyo mtu anapopata sonona kali, ndivyo anavyokuwa na ukaribu zaidi wa kujinyonga. Mtu anapokatishwa tamaa zaidi anakuwa hatarini zaidi kujiua,” anasema Paula Clayton, mkurugenzi wa taasisi ya Marekani ya kuzuia watu kujiua.

Mtu kujiona mkosaji

Madelyn Gould, profesa wa uchunguzi wa magonjwa ya akili katika Chuo Kikuu cha Columbia Medical Center kilichopo New York, Marekani anasema hali ya kujiona mkosaji inapozidi, ambayo huwa ni dalili ya msongo wa mawazo na hofu, ni mambo yanayopaswa kuangaliwa kwa karibu na mtu akiwa na dalili hizo anapaswa asiachwe pekee yake.

“Unaanza kudhani ni mkosaji kuhusu jambo fulani, unadhani umewaangusha wenzako. Ukizungumza na mtu mwingine anakwambia hujafanya kosa kubwa, lakini huamini,” anasema Gould.

Dk Mwami anasema mtu mwenye msongo wa mawazo ambayo yametokana na kufarakanishwa na jamii yake, hujiona dhaifu na asiye na mamlaka yoyote, hivyo mtu huanza kujiona mkosaji katika jamii yake.

Unywaji pombe/dawa za kulevya

Matumizi ya dawa za kulevya na kunywa pombe kupita kiasi, mambo ambayo baadhi ya watu hutumia kama kupunguza mawazo au hasira, ni ishara za mtu anayetaka kujiua, anasema Dk Clayton. “Unaweza usiwe mnywaji wa pombe, au mtumiaji wa dawa za kulevya, lakini kama unadhani kwa kufanya hivyo unaweza kusahau matatizo au kujisikia vizuri, unakuwa katika mazingira ya kutokuwa na uamuzi sahihi wa kila jambo hivyo kuwa hatarini,” anasema.

Hofu

Ken Robbins, Profesa na daktari wa magonjwa ya akili wa Chuo Kikuu cha Wisconsin kilichopo Madison, Marekani anasema nusu ya watu wenye sonona huwa na sonona ambayo huwababisha huzuni, uchovu na kupoteza hamu ya kula.

Nusu nyingine huwaweka katika sonona ya misukosuko na usumbufu. Hii huwasabishia watu kukosa usingizi, kukosa raha na uchovu. Profesa Robbin anasema hofu kwa ujumla ni tatizo kubwa na huchangia katika watu kujiua. Ukiona mtu ana hofu ya mara kwa mara kuwa naye karibu.

Kuwa na silaha nyumbani

Miongoni mwa sababu kubwa ya watu kujiua ni kuwa na silaha nyumbani. Watu wenye silaha kama bastola au bunduki wapo kwenye hatari zaidi ya kujiua mara 10 kuliko ambao hawana. Wanaume hupenda kujiua kwa kujipiga risasi wakati wanawake hupenda kujiua kwa kunywa vidonge vingi yaani kuji-overdose.

Matatizo ya kiafya

Wengi wanadhani vijana wapo hatarini zaidi kujiua kuliko makundi mengine. Lakini ukweli ni kuwa wazee wapo katika hatari zaidi kwa sababu ya kudorora kwa afya zao. Nchini Marekani, mwaka 2015 watu wenye umri wa miaka 45 mpaka 64 walikuwa na kiwango kikubwa cha kujiua kwa asilimia 19.6 wakifuatiwa na wenye umri wa miaka 85 na zaidi ambao walikuwa asilimia 19.4 kwa mujibu wa taaisisi ya Marekani ya kuzuia kujiua.

Matumizi ya kompyuta/simu

Dalili nyingine ambayo inaweza kuonyesha kuwa mtu anataka kujiua ni matumizi makubwa ya kompyuta na simu. Ukiangalia watu wengi waliojiua ukienda kwenye kompyuta zao utagundua mara kwa mara walikuwa wakitafuta kwenye google jinsi ya kujiua,” anasema Dk Clayton huku akishauri wazazi kuwafutilia watoto wao hasa kwenye Facebook na mitandao mingine kama simu.

Dk Mwami, ambaye alikuwa mhadhiri wa UDSM anashangazwa na jinsi watu walivyofarakanishwa na jamii yao kupitia mitandao ya simu huku akisema kushabikia teknolojia hiyo ni sawa na kudumazwa nayo.

“Unashangaa unawafundisha wanafunzi, baada ya hapo unamkuta kila mtu yupo kwenye simu, mtu anapanda daladala hata hajakaa vizuri unamkuta yupo kwenye simu, hajui chochote kinachoendelea ndani au nje ya daladala kwa sababu yupo bize na simu. Hii ni dalili mbaya na inaonyesha jinsi mtu alivyotenganishwa na jamii yake,” anasema Dk Mwami.

Columnist: mwananchi.co.tz