Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Changamoto za uandishi katika Kiswahili

14315 Erasto+Duwe TanzaniaWeb

Tue, 28 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Uandishi ni miongoni mwa mambo ambayo hayaepukiki maishani. Uandishi unaozungumziwa katika makala haya ni uandishi rasmi unaofuata taratibu na kanuni mbalimbali.

Uandishi nyaraka mbalimbali kama vile wa barua hususan za kikazi, dokezo, ripoti, risala, hotuba; una namna zake za kuandika.

Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na tatizo kubwa katika uandishi wa nyaraka mbalimbali.

Kwa kiasi fulani tatizo hilo linachangiwa na mitazamo potofu ya baadhi ya watu wadhanio kwamba kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, hakuna tena umuhimu wa kujishughulisha na uandishi wa barua na nyaraka.

Baadhi ya watu wamekuwa wakibeza umuhimu wa barua na kusisitiza umuhimu wa mawasiliano mathalani ya simu.

Hivyo hata baadhi ya walimu shuleni hawaweki tena msisitizo katika mada zihusuzo uandishi.

Kanuni na taratibu za uandishi hususan tahajia, zimekuwa tatizo katika uandishi. Si ajabu kwa baadhi ya watu kuandika huku kazi zao zikiwa hazina alama kama nukta.

Baadhi ya watu huandika kwa kuchanganya mawazo mbalimbali wanayokusudia kuyawasilisha kwa wasomaji wao bila kuyapangilia katika vifungu stahiki kwa mantiki na uzito wa mawazo.

Changamoto nyingine katika uandishi ni ya kutumia lugha ya mazungumzo badala ya lugha ya maandishi. Kuna tofauti kubwa kati ya dhana hizo mbili. Anayeandika nyaraka rasmi, anapaswa kutumia lugha rasmi ya kimaandishi.

Katika lugha ya mazungumzo mtu yuko huru kuongea lolote aliwazalo na hata kutumia lugha isiyo rasmi na fasaha ili mradi tu aelewane na anayewasiliana naye.

Mawasiliano ya namna hiyo yanaruhusiwa pia katika uandishi wa barua za kirafiki. Lakini uandishi wa kazi nyingine rasmi kama vile barua za kikazi, ripoti, risala, hotuba, insha katika ujibuji wa mitihani shuleni na vyuoni, na uandishi mwingine rasmi hauna budi kuzingatia uakifishaji, urasmi wa lugha na muundo wa aina ya andiko linaloshughulikiwa pamoja na taratibu nyingine zinazotawala uandishi huo.

Uandishi ni taaluma kama taaluma nyingine. Kwa sababu hiyo, mwandishi yeyote hana budi kujipanga kabla ya kuandika aina ya waraka aliokusudia kuandika.

Makosa mbalimbali yajitokezayo katika uandishi kama vile ya kutozingatia kanuni za uandishi, kukiuka muundo wa waraka husika, ukosefu wa lugha fasaha na rasmi, yana athari kubwa katika kusudio la waraka unaoshughulikiwa.

Kanuni na taratibu za uandishi zisipozingatiwa ipasavyo, mwandishi anaweza kujisababishia kutoeleweka kwa ujumbe husika, kuwakera wasomaji/walengwa, na mbaya zaidi ni kutokukubaliwa ikiwa waraka huo unahitaji majibu.

Mathalani, baadhi ya watu wamekosa kazi kwa sababu ya kutozingatia taratibu stahiki za uandishi bora. Baadhi ya wanafunzi hufeli mitihani yao kwa kuwa hawazingatii uandishi rasmi hata kama wana majibu kwa maswali wanayotahiniwa.

Mpenzi msomaji, kujua kusoma na kuandika ni jambo moja, na kujua kuandika kwa usahihi na ubora ni jambo jingine. Ipo haja ya kuchukua hatua za makusudi kujikumbusha kuhusu uandishi wa aina mbalimbali za nyaraka.

Kwa kubaini umuhimu wa taaluma ya uandishi, Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita ) na baadhi ya waandishi, kwa nyakati tofauti wametoa vitabu mbalimbali kuwa miongozo kwa waandishi.

Ili kuepuka kubananga Kiswahili chetu adhimu na kuziwezesha kazi zetu kuwa zenye kiwango cha ubora, tumakinikie taratibu za uandishi bora. Tuache kuandika kwa mazoea.

Columnist: mwananchi.co.tz