Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Chaguo lililo jema, vyama vya upinzani vijitoe au vijitose uchaguzi mdogo

11409 Upinzani+pic TanzaniaWeb

Sat, 14 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kipenga kishapulizwa. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo wa mbunge katika jimbo la Buyungu mkoani Kigoma na madiwani katika kata 77 za Tanzania Bara.

Uchaguzi wa Buyungu utakaofanyika Agosti 12, 2018 unalenga kujaza nafasi iliyoachwa wazi baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, kwa tiketi ya Chadema, Kasuku Bilago, kilichotokea Mei 26 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Kwa upande wa madiwani, uchaguzi huo utakaohusisha halmashauri 43 katika mikoa 24 ya Tanzania Bara, unatokana na sababu mbalimbali ikiwamo kujiuzulu kwa waliokuwa wanashikilia nafasi hizo.

Hii ni mara ya tatu kwa uchaguzi mdogo kufanyika katika maeneo mbalimbali baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 uliompa ushindi Rais John Magufuli. Mara zote katika chaguzi hizo, licha ya kuwapo malalamiko upande wa pili, chama tawala CCM kilipata ushindi na kujiongezea idadi ya madiwani na wabunge.

Chaguzi hizo zililalamikiwa kwamba ziliendeshwa katika mazingira ambayo vyama vya upinzani havikutendewa haki na kusababisha kupata matokeo mabaya.

Katika chaguzi hizo, hasa kwa Jimbo la Kinondoni, lawama zilielekezwa kwa wasimamizi wa uchaguzi wakidaiwa kutotenda haki dhidi ya upinzani, huku sanduku la kura likidaiwa ‘kuibwa na baadaye’ kurejeshwa katika kituo cha uchaguzi bila hatua zozote kluchukuliwa.

Sambamba na hayo, Tume ya Uchaguzi ililaumiwa kwa kushindwa kutoa vitambulisho kwa mawakala wa upinzani, jambo lililosababisha wafuasi wa Chadema kuongozana kwenda kwa msimamizi wa uchaguzi kushinikiza kupatiwa kwa vitambulisho.

Kitendo hicho kilisababisha polisi kuingilia kati na katika mazingira hayo, mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini alipoteza maisha baada ya kupigwa na risasi iliyokatisha uhai wake na baadaye viongozi wa Chadema kufunguliwa mashtaka yanayoendelea mahakamani.

Makandokando hayo yameibua maswali miongoni mwa wadau wa siasa nchini baada NEC kutangaza uchaguzi mdogo wa sasa. Swali kuu ni je, mambo yatakuwa yaleyale au kutakuwa na mabadiliko?

Wapo wanaoona ni bora kwa vyama hivyo vikajiweka kando na kuiacha CCM ishiriki yenyewe katika uchaguzi huo kwa maelezo kwamba hata vyama hivyo vikishiriki ni sawa na kuisindikiza na mwishowe kupokwa ushindi, lakini wengine wanaona vinginevyo. Wenye mtazamo tofauti na huo wanashauri vyama vyote vishiriki katika mchakato huo ili kupaza sauti kuwaonyesha wananchi hali halisi iliyopo katika uwanja wa mapambano.

Maoni ya wachambuzi

Mwanasiasa mkongwe na waziri wa zamani, Njelu Kasaka anasema ni kweli chaguzi zina matatizo yake, lakini upinzani ni lazima ushiriki ili kuhakikisha unatimiza wajibu wake.

“Kuna suala la uwepo, usipogombea ina maana hautaonekana. Na ili siasa itimie ni pamoja na kujishughulisha na masuala ya uchaguzi,” anasisitiza Kasaka.

Kasaka anasema ni vizuri vyama vya upinzani vikashiriki uchaguzi huo pamoja na kwamba kilichotokea katika chaguzi dogo zilizopita kinafahamika, vinginevyo hawataonekana na hivyo wanaweza kupotea kabisa.

“Wananchi wanataka kuona upinzani upo na unaendelea kuwa imara kwa kushirikia masuala mbalimbali ya siasa,” anaongeza.

Anasema kuwa kutoshiriki au kususia uchaguzi kwa namna yoyote ile, si jawabu la kutokuwa na imani na chombo chochote cha Serikali na kwamba ni lazima wapinzani hao watimize wajibu wao,” anaongeza.

Kasaka aliyewahi kuhama CCM kwenda CUF na baadaye Chadema, anasema suala la kutokushinda ni lingine na kwamba wasiposhinda kwa sababu zozote zile za hila wananchi wanaona na kuchambua sababu hizo.

“Kama itatokea figisufigsu yoyote ile itakayosababishwa ama na wenye mamlaka, wananchi wataona na wao ndiyo wenye maamuzi, hivyo wapinzani wasiogope wala kukata tamaa,” anasisitiza.

Kwa mujibu wa Kasaka hakuna marefu yasiyo na ncha na kwamba ipo siku ukweli utabainika na haki itatendeka na kila mmoja atajua ukweli.

Hata hivyo, suala la kutoshiriki ama kushiriki kwa upande wa Chadema awali lilionekana kitendawili mpaka pale vikao vya juu vya chama hicho vilipotoa maamuzi ya kushiriki.

Chadema kushiriki uchaguzi

Naibu katibu mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salumu Mwalimu anasema, “Suala si kama tutashiriki au hatutashiriki, bali ni endapo tunashiriki au hatushiriki ni kwa nini na kwa namna gani tutashiriki.

Uamuzi wa Chadema kushiriki uchaguzi huo ulifikiwa katika kikao cha siku mbili cha Kamati Kuu kilichoketi wiki hii chini ya mwenyekiti wake, Freeman Mbowe. Na baadaye chama hicho kikatoa tamko rasmi la kushiriki uchaguzi huo kikieleza sababu mbili.

Mosi, Chadema inasema itatumia uchaguzi huo kama kipimo cha mkurugenzi mpya wa uchaguzi katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Athuman Kihamia.

Kihamia aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa Jiji la Arusha, aliteuliwa na Rais John Magufuli Julai 1 kuchukua nafasi ya Kailima Ramadhani, ambaye amehamishiwa katika Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi kuwa naibu katibu mkuu.

Chadema imewahi kumlalamikia Kailima ikidai kuwa chini yake NEC imekuwa haiwatendei haki katika chaguzi kadhaa zilizopita kiasi cha kususia baadhi ya chaguzi.

Katika uchaguzi wa madiwani kwenye kata 43 wa Novemba mwaka jana, chama hicho kiliilalamikia NEC kwa kutowatendea haki na kujitoa katika uchaguzi wa udiwani katika kata tano za Arumeru mkoani Arusha.

Kutokana na kilichotokea Novemba, Chadema pia ilisusia uchaguzi mdogo wa majimbo ya Longido, Songea Mjini na Singida Magharibi na kata kadhaa, ikidai Tume isingewatendea haki. CCM ilishiriki pamoja na vyama vingine vidogo na kunyakua nafasi zote.

Malalamiko ya Chadema dhidi ya NEC hayakukoma. Katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kinondoni na Siha, Chadema iliamua tena kushiriki kwa ilichosema kuona kama Tume hiyo imefanyia kazi malalamiko yake, lakini badili yaliibuka mengine mapya.

Safari hii ikiwamo kucheleweshewa au kunyimwa barua za kuwatambulisha na viapo vya mawakala, wakisema matokeo yake mawakala wake wengi walikataliwa katuika vituo vya kupigia kura, madai ambayo wakati wote NEC imekuwa ikiyakanusha.

Sababu ya pili ya chama hicho kikuu cha upinzani kuingia katika kinyang’anyiro hicho sasa, ni kutaka kutumia uchaguzi huo kufanya siasa za majukwaani ambazo tangu utawala wa awamu ya tano uingie madarakani zimezuiwa.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema anasema ili kufanikisha lengo hilo, chama hicho kimempitisha Elia Kanjero kuwa mgombea ubunge Buyungu na utaratibu wa kupata wagombea katika kata 79 unaendelea.

Kanjero anatarajia kuchuana na Christopher Chiza aliyeteuliwa na CCM na wagombea wengine wa vyama vingine kama watakuwapo.

Ushirikiano wa vyama

Chadema ambayo imeanza kulalamikia baadhi ya wagombea wake kufanyiwa faulo, imesema itakuwa tayari kushirikiana na chama chochote ambacho kitakuwa tayari vikiwamo vile vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya CUF, NLD na NCCR-Mageuzi.

Hofu kwa watendaji

Akizungumzia hatua hiyo, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Iringa (UoI) Dk Gibson Sanga anasema kuna kazi kubwa ya kubadili mfumo ulipo sasa ambao umejenga hofu kubwa kwa watendaji wanaosimamia uchaguzi.

“Sasa kuna hofu kubwa na msukumo kutoka juu na endapo CCM isiposhinda watendaji wakiwamo Mkurugenzi wanaonekana hawafanyi kazi, jambo linalochangia kuvuruga uchaguzi, anasema mhadhiri huyo wa sayansi ya siasa.

Hata hivyo, Dk Sanga anasema ni vigumu kutoa ushauri kwa kuwa sasa uchaguzi umekuwa ni kama vita ndogo kati ya wananchi na vyombo vya dola na kwamba unafanyika ili kutimiza matakwa ya sheria tu na siyo kutoa nafasi sawa kwa pande zote.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Nguruma kwa mtazamo wake anasema ni muhimu kwa vyama vya upinzani kushiriki uchaguzi huo ili kama kuna matatizo yaonekane.

“Mfano, wote tumeshuhudia kilichotokea katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni, Dar es Salaam na lile la Siha mkoani Kilimanjaro, endapo vyama vya upinzani vingeacha au kususia chaguzi zile kuna mengine yasingeonekana lakini kwa kushiriki kwao imefumbua mambo mengi ya uozo na kila mmoja sasa amefahamu dhamira ni ipi hasa,” anasisitiza Ole Nguruma.

Mtetezi huyo wa haki za binadamu anasema kwa kushiriki kwao (wapinzani), wananchi wamegundua tatizo liko wapi lakini pia vyama vyenyewe vimepata funzo na hivyo hata watakavyoshiriki uchaguzi mwingine watakuwa na pa kuanzia ili kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na chama tawala.

Hata hivyo, Ole Nguruma anasema ni vyema kuwa na angalizo na kuwa na malengo mawili makuu kabla ya kuingia katika kinyang’anyiro hicho.

Kwanza, anasema wanapaswa kushiriki kwa lengo la kuhakikisha wanashinda uchaguzi huo, pili ni kuonyesha mabaya wanayofanyiwa ili wananchi watambue ili waweze kuchukua maamuzi sahihi.

Akizungumzia mabadiliko yaliyofanywa hivi karibuni na Rias Magufuli kwa Tume ya uchaguzi, anasema haoni mabadiliko hayo kama yanaweza kuleta tija yoyote katika chaguzi zinazokuja.

“Mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi, tatizo siyo viongozi, tatizo ni mfumo kwani hata waliobadilishwa wamefuata utaratibu uleule wa Rais kuwateua, hivyo kama kweli tunataka kuwa na Tume huru itakayoweza kusimamia uchaguzi kwa haki, ni lazima kubadili mfumo mzima,” anasisitiza Ole Nguruma.

Mwanaharakati huyo anasema kwa kubadili viongozi hakuna kitu kipya kitakachobadilika na upinzani utaendelea kupita katika misukosuko kama ilivyokuwa kwa vipindi vingine.

Hata hivyo, anasema jambo la msingi kwa vyama vya upinzani ni kutokata tamaa na kuhakikisha vinatafuta mbinu mbadala ili kufikia malengo yao.

Anasema huwezi kuwa mpinzani kama hufanyi siasa na uchaguzi unapima kama siasa zako zinakubalika, hivyo wasikubali kuacha nafasi hiyo iwapite, waitumie ipasavyo.

Columnist: mwananchi.co.tz