Dar es Salaam. Vyama vya upinzani nchini Tanzania vya Chadema na ACT- Wazalendo vimetoa salamu za rambirambi kwa familia ya aliyekuwa Mhariri wa gazeti la Jamhuri, Godfrey Dilunga aliyefariki usiku wa kuamkia leo Jumanne Septemba 17,2019 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam.
Dilunga ambaye amewahi kufanya kazi katika magazeti ya Raia Mwema na Mtanzania nchini Tanzania amekutwa na mauti wakati akipatiwa matibabu ya maradhi ya tumbo ‘typhoid’.
Taarifa ya Chadema iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Tumain Makene imeelezea jinsi Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe alivyoguswa na msiba huo.
Katika taarifa hiyo, imemnukuu Mbowe akisema, “Nimepokea kwa huzuni na masikitiko taarifa za msiba huu. Tumefanya kazi na Dilunga kwa ukaribu, kimsingi alikuwa mmoja wa waandishi wa habari kwenye timu ya wanahabari kutoka vyombo vya kimataifa, tuliozunguka nchi nzima kuanzia mwaka 2000.”
“Pumzika kwa amani, Chadema inatoa pole na salaam za rambirambi kwa familia ya marehemu Dilunga, ndugu, jamaa na marafiki kwa kuondokewa na mmoja ya nguzo na mpendwa wao. Mungu awafariji wote walioguswa na msiba huu,” amesema Mbowe ambaye pia Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
Katika salamu zao za pole Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano na Umma wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema chama kinatoa pole kwa familia, uongozi wa gazeti la Jamhuri, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na tasnia ya habari kwa kumpoteza Dilunga.