Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

CCM kukirimu wanaotoka upinzani, inaitendea dhambi katiba yake

13763 Ccm+pic TanzaniaWeb

Sat, 25 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mei 25, 2011, Rais wa 44 wa Marekani, Barack Obama alihutubia Bunge la Uingereza, chemba zote mbili kwa pamoja; ya chini yenye wabunge wa wananchi (House of Commons) na ya juu, iliyokutanisha malodi (House of Lords), katika ukumbi wa Westminster, London, Uingereza.

Obama katika hotuba hiyo alieleza kupewa heshima kubwa zaidi kuhutubia katika ukumbi wa Westminster akiwa mtu wa nne baada ya Papa, Malkia wa Uingereza na Nelson Mandela.

Obama alipoambiwa kwamba watu watatu wa mwisho kabla yake kuhutubia Bunge la Uingereza kuwa ni aliyekuwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki dunia, Papa Benedict XVI, Malkia Elizabeth II wa Uingereza na Mandela, aliona ama na yeye amekuwa mtu mzito sana au labda ulikuwa utani mkubwa kumlinganisha na watu hao watatu.

Maneno hayo “mwanzo wa utani wenye kuchekesha sana” ndiyo naguswa kuyatumia kufikisha maudhui kuhusu mwendo mpya wa CCM, hususan tabia mpya ya kupokea viongozi kutoka vyama vya upinzani na kuwasimamisha kugombea nafasi walizojiuzulu bila kupingwa.

Tabia hiyo ya CCM ni mwanzo wa utani mkubwa wa kisiasa, lakini zaidi ni dhambi kubwa ya kisiasa. Kwa chama ambacho kinaheshimu demokrasia na haki za wanachama wake ni lazima kitaheshimu Katiba. CCM hivi sasa inajikita zaidi kukirimu wageni kiasi kwamba inaacha misingi yake.

CCM inakuwa sawa na nyumba ambayo mgeni akiingia na utaratibu wote wa kimaisha unabadilika. Wanafamilia wanakuwa hawapati huduma, maana kipaumbele ni wageni. Matokeo yake mpaka watoto wanawachukia wageni, wanakuwa wanaomba usitokee ugeni mwingine.

Inafahamika kuwa CCM ina watu ambao walibeba gharama kubwa kuhakikisha chama chao kinashinda dola kwenye Uchaguzi Mkuu 2015. Mara haohao waliokipigania chama wanajikuta si kipaumbele tena. Mboni zao zinapokea mfululizo wa matukio yenye kuonyesha kwamba wageni wana thamani kubwa.

Huu ni utani mkubwa wa kisiasa; kuna wanasiasa ambao walikimbilia upinzani baada ya kuona nafasi zao za kupata uongozi CCM ama ni finyu au hazipo kabisa, watu hao walipofika upinzani, pengine kwa uhaba wa watu, ikawa rahisi kwao kupata nafasi ya kugombea ubunge au udiwani na kushinda.

Ajabu ya watu hao, wanapotoka upinzani wakiwa wabunge au madiwani, wanapewa mapokezi yenye hadhi kubwa. Chama kinaamua kuvuruga utaratibu wake wa kawaida, kinazuia wanachama wengine kusogelea haki zao. Huwezi kutafuta kipimo kingine cha ukandamizaji wa demokrasia halafu hicho ukakisahau.

Chama kupokea wageni ni jambo zuri sana. Hata kuwakirimu ni vizuri pia, haipendezi mgeni apokelewe kwa masimango. Hata hivyo, kipindi chama kinapokea wageni hakitakiwi kusahau mambo mawili; mosi, furaha ya ugeni isisababishe wenyeji wakose stahili zao. Pili, wageni hawatakiwi kubomoa misingi ya nyumba.

Wabunge na madiwani waliotoka upinzani na kujiunga CCM kisha kuchaguliwa katika nafasi zao, sasa hivi hawasemi wazi wakasikika, ama wananong’ona na watu wao wa karibu au wametulia nayo vifuani, lakini kwa vyovyote lazima wawe wanajiona bora kuliko waliowakuta.

Ni dhambi ya Katiba

Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln, alipata kusema: “Tusiingilie chochote ndani ya Katiba. Inatakiwa itunzwe wakati wote, kwani ndiyo pekee inayolinda usalama wa ukombozi wetu. Na si demokrasia peke yake inayonifanya nifanye ombi hili, lakini kwa wote wanaopenda hii misingi bora na ya kweli.”

Lincoln alisema Katiba ni kitu ambacho hakipaswi kuingiliwa kwa chochote. Kwamba si kwa sababu za kidemokrasia peke yake, bali kwa misingi yote ndani ya Katiba. Nitie mkazo hapa kuwa anayependa nchi lazima aipende, aiheshimu na ailinde Katiba ya nchi. Mwanachama mwenye mapenzi na chama chake, ataipenda, kuiheshimu na kuitukuza Katiba ya chama.

Hivi karibuni, Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, alifanya mkutano na waandishi wa habari, alioutumia kuwashuru wananchi kwa chama chake kuendelea kupata ushindi katika uchaguzi mdogo, vilevile kumkaribisha aliyekuwa mbunge wa Liwale (CUF), Zuberi Kuchauka aliyehamia CCM.

Hili la Kuchauka limo kwenye muktadha wa makala haya, lakini kwanza tulielekee swali la kikatiba ambalo Dk Bashiru aliulizwa. Kwamba kwa nini wabunge na madiwani wanaohamia CCM kutoka vyama vya upinzani, chama hicho huwa hakiendeshi kura za maoni kwenye majimbo na kata zao, badala yake husimamishwa kugombea bila kupingwa?

Dk Bashiru alijibu kuwa kuna mambo mazuri hayapo kwenye katiba na chama huyatumia wanapoona yanafaa. Akatolea mfano utaratibu wa CCM kumpitisha bila kupingwa Rais atokanaye na chama hicho, kila anapotaka kugombea muhula wake wa pili. Kwamba hiyo haipo kwenye katiba ya chama, ila ni utaratibu waliojiwekea.

Alichosema Dk Bashiru ni kweli lakini siyo sahihi. Chama chochote cha siasa huwa kina masuala yake ya kikatiba ambayo ndiyo misingi. Vilevile yapo mambo ya utamaduni. Mfano alioutoa huo ni utamaduni ambao chama hicho kimejiwekea.

Rais atokanaye na CCM ndiye anakuwa mwenyekiti wa chama. Huo ni utamaduni wa chama hicho wa kuunganisha kofia mbili za uongozi, kwamba Rais wa nchi lazima awe na mamlaka ndani ya chama. Isije kutokea chama kikamyumbisha Rais. Hili pia halipo kwenye Katiba.

Mgogoro wa kisiasa ambao aliyekuwa Rais wa Malawi, Bingu wa Mutharika alikutana nao kwenye chama cha United Democratic Front (UDF) mwaka 2005, mpaka akalazimika kuanzisha Chama cha Democratic Progressive (DPP), ni kwa sababu alikuwa Rais asiye na mamlaka kwenye chama chake.

Aliyekuwa Rais wa UDF Bakili Muluzi, alipoanza kuguswa na Mutharika kwenye Serikali, mgogoro mkubwa uliibuka. Wakaanza kuonyeshana umwamba. Mutharika na urais wa nchi, Muluzi urais wa UDF. Hivyo, CCM waliliona hili mapema, kwamba isitokee Rais akawa mnyonge kutenda kazi yake kwa sababu ya kukosa mamlaka kwenye chama.

Utamaduni mwingine ni Rais kugombea muhula wa pili bila kupingwa. Ni utamaduni wenye lengo la kulinda heshima ya Rais ambaye anakuwa mwenyekiti wa chama.

Vizuri kukumbushana

Utamaduni huo wa kumheshimu Rais aliye madarakani anapotaka kugombea muhula wa pili, upo hata kwa vyama vya Republican na Democrat, Marekani. Agosti 24, mwaka jana, mtandao wa CBS News, uliripoti kwamba Gavana wa Ohio, John Kasich, atawania tiketi ya Republican dhidi ya Rais Donald Trump ili ateuliwe kuwa mgombea urais, kipindi ambacho Trump atakuwa anawania muhula wa pili.

Hiyo ni kuonesha kwamba utamaduni wa kumpitisha Rais aliye madarakani bila kupingwa hauzidi nguvu ya Katiba. Ndiyo maana milango huwa ipo wazi kwa yeyote ndani ya chama.

CCM haijawahi kuwa na utamaduni wa kumheshimu mbunge aliye madarakani, kwamba apite bila kupingwa. Na hili la wabunge na madiwani kujiunga na CCM kisha kupewa nafasi ya kugombea bila kupingwa ni jipya. Mbaya zaidi linakandamiza demokrasia.

Upigaji kura za maoni CCM umefungwa kama haki ya kikatiba. Katiba ya CCM, sehemu ya pili inayozungumzia wanachama na viongozi, ibara ya 14 ni haki za mwanachama wa CCM kupiga kura ya maoni kwa wagombea wa nafasi za udiwani wa kata/wadi, ubunge na uwakilishi wa jimbo kwa kufuata masharti ya Kanuni za CCM.

Ieleweke kuwa jambo lolote likishatamkwa ni haki ya mtu, likiondolewa au kunyimwa, maana yake mtu husika amenyimwa haki yake. Ikishaitwa haki, maana yake ni stahili ya mtu. Sasa Katiba ya CCM imeandikwa ni haki ya mwanachama kupiga kura ya maoni. Hivyo, akinyimwa haki hiyo, inakuwa hajatendewa haki na Katiba inakuwa imevunjwa.

Dk Bashiru alipotaka kufananisha upatikanaji wa mgombea urais wa CCM na ubunge au udiwani, hapo alikosea. Kosa hilo linafanya malalamiko ya wapinzani kwamba wabunge na madiwani wananunuliwa yapate nguvu. Maana inaonekana huwa kuna makubaliano kati ya wanaohama na wanaowapokea ambayo husababisha haki ya kura ya maoni inyimwe.

Columnist: mwananchi.co.tz