Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Bustani ya mboga ,matunda inalipa mshahara kila mwezi

Thu, 4 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Achana na maneno ya kukatisha tamaa, ukikifanya kwa maarifa, kilimo kinalipa na kinaweza kukupa fedha nyingi kukidhi mahitaji yako.

Wapo vijana wengi wa mfano ambao wamejikita kwenye kilimo na wanafanya mambo makubwa tofauti na imani ya baadhi yao hasa wahitimu ya vyuo vikuu wanaodhani kilimo na shughuli zake si ajili yao. Zamani ilizoeleka kuwa kilimoni kwa ajili ya watu waishio kijijini lakini kwa siku za karibuni mambo yamebadilika na baadhi ya watu wanahama mjini kwenda kulima.

Hili linadhihirishwa na David Msaki (73), ofisa maendeleo aliyeamua kuipa kisogo taaluma yake na kujikita kwenye kilimo huko wilayani Serengeti.

Tofauti na watumishi wengi ambao muda mfupi baada ya kustaafu huhangaika kutafuta kazi kwenye kampuni binafsi waweze kujikimu licha ya kupoteza sifa za kuajirika, yeye anafanya kilimo kwa namna tofauti.

Mzee Msaki anaamini kazi ya mkono yake inalipa zaidi kuliko kuajiriwa mahali popote licha ya faida nyingine za kujiajiri. “Nilianza kilimo tangu nikiwa kazini na kwa sehemu kubwa kilibeba gharama za masomo ya wanangu, mapato yalikuwa makubwa kuliko mshahara niliokuwa napata,” anasema mzee Msaki.

Astaafu kwa hiyari

Kutokana na mafanikio aliyokuwa anayapata kwenye kilimo, anasema mwaka 1995 aliomba kustaafu na kuelekeza nguvu zake huko akijikita kwenye kilimo cha bustani mchanganyiko ambacho kinamwezesha kupata fedha kila wakati.

“Nilistaafu nikiwa napata mshahara wa Sh75,000 kwa mwezi, kiasi ambacho ni kidogo kikilinganishwa na nilichokuwa napata kutoka kwenye kilimo. Kwa ujumla niliona kama napoteza muda mwingi kuendelea na utumishi, niliomba kupumzika,” anasema.

Alistaafu akiwa na miaka 50 uamuzi ambao anasema ulimsaidia kuboresha shamba lake la hekta tano kwa kulima mazao mchanganyiko ikiwemo miti ya aina mbalimbali inayowavutia watu wengi kwenda kujifunza.

Bustani maridhawa

Zaidi ya nusu ya maisha yake, anasema ameelekeza nguvu kwenye kilimo ambacho licha ya kumuwezesha kusomesha watoto watano alionao bila wasiwasi, zimempa uhakika wa kipato kwa ajili ya mambo mengine.

Mpaka sasa mzee huyo anasema uwekezaji alioufanya ni mkubwa ambao kama ataamua kuiuza bustani yake basi anaweza akaingiza karibu Sh1 bilioni kwani ameigeuza kuwa ofisi yake na kila kukicha hufikiri kuongeza kitu kipya na cha kipekee.

“Sijawahi kutembelewa na wataalam wa kilimo kunipa ushauri badala yake wengi wanakuja kujifunza kwangu kutaka kujua aina ya matunda na miti niliyopanda, nilivyofanikiwa kuiboresha na kuiongezea thamani,” anabainisha.

Ndani ya bustani yam zee Msaki kuna matunda ya aina nyingi, mboga za majani, nafaka kama mahindi, viazi, mihogo na miti ya mbao, kuni, mapambo na kivuli.

Ubunifu na uvumbuzi

Kutotembelewa na wataalamu wa kilimo kumpa ushauri hakucheleweshi safari yake kwani kilakukicha anawaza anavyoweza kufanya kitu kipya. Analima hata mazao ambayo wakulima wengine mkoani Mara hawayapandi.

Baada ya kuona kuna mahitaji makubwa la tende hasa kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, aliagiza mbegu ambazo amezipanda.

“Najitahidi mara kwa mara kufuatilia mahitaji ya watu hasa vitu wanavyoagiza kutoka nje nami hujielekeza huko. Baada ya muda nitakuwa nazalisha tende hapahapa badala ya kuagiza kutoka Dubai na kwingineko,” anasema.

Sio tende pekee, mzee huyo ameanzisha kilimo cha chikichi lengo lake likiwa kuleta mageuzi kwa jamii wilayani humo ambayo kwa kiasi kikubwa imejikita kwenye kilimo cha mahindi, mtama, ulezi, pamba na tumbaku kutambua fursa zilizopo kwenye mazao mengine.

Chikichi ni zao maarufu mkoani Kigoma, Ruvuma, Tanga, Pwani na Mbeya. Anasema kuanza kwake kulilima zao hilo ni juhudi za kuleta mageuzi katika sekta hiyo ili wananchi wengine wachangamkie fursa za kibiashara.

Anaamini endapo kilimo cha chikichi kitachangamkiwa na wanakulima wengi kitachochea uwekezaji wa viwanda vya mfuta nchini kutokana na uhakika wa malighafi za kutosha.

Mstaafu huyo anasema kama wataalam wangetimiza wajibu wao vizuri, wilaya hiyo ingeweza kuzalisha mazao mbalimbali ya biashara kwa kuwa maeneo ya kuendelezwa yapo mengi kinachokosekana ni hamasa tu kwa wananchi.

“Wilaya ina mifugo mingi inayotoa uhakika wa mbolea, kama wataalam wangetimiza wajibu wao naamini wananchi wangeachana na kilimo cha mazao yaliyozoeleka ambayo hata hivyo hayana tija na masoko yake si ya kuaminika,” anasema.

Mafanikio

Ingekuwa ameajiriwa mahali basi ungesema ni miongoni mwa wanaolipwa mshahara wa kati kwani anasema kila mwezi ana uhakika wa kupata zaidi ya Sh500,000 kwa kuuza mazao mbalimbali aliyonayo shambani mwake.

Si kwa wafanyakazi wengi wanaolipwa chini ya kiasi hicho, anasema fedha ni nyingi hata kwa mkulima wa mazao mengine wanaovuna mar amoja kwa mwaka. “Hapa nauza miche ya miti mbalimbali ninayootesha, baadhi haipatikani maeneo zaidi ya hapa kwangu. Mingine naiboresha ili ianze kutoa mazao kwa muda mfupi,” anasema.

Anao mpango wa kuboresha zaidi kilimo chake kwani ameanza matayarisho ya kuchimba kisima kirefu kitakacho msaidia kupata maji ya kutosha kufanya umwagiliaji wa bustani yake.

Umwagiliaji huo wa mazao anayolima, anasema utasaidia kuimarisha ukijani wa bustani na kumsaidia katika ufugaji nyuki aliouanza ndani ya eneo hilo iliaanze kuvuna asali na mazao mengine ya wadudu hao yenye soko kubwa wilayani humo.

Changamoto

Kama walivyo wakulima wengine, mzee Msaki pia anakabiliana na changamoto hasa ukosefu wa soko la uhakika la matunda chanzo kikiwa kutokuwa na viwanda vya kusindika mazao hayo.

“Matunda kama machungwa, maembe, maparachichi, machenza na mengine huiva karibu kwa wakati mmoja maeneo mengi lakini wateja wetu ni wale wale hivyo bei huwa chini na wakati mwingine huozea shambani,” anasema.

Anasema kwa kipindi hicho bei huwa chini sawa na kwa bure maana kalai la mapera kwa mfano huuzwa mpaka Sh2,000 ilmradi yasiozee shambani.

Changamoto nyingine anasema ni wizi wa mazao na ukataji miti unaofanywa zaidi usiku. Kwa wanaofanya uvamizi huo bustanini kwake, anasema humpa changamoto ya kupanda upya na kusubiri muda mrefu kabla miti husika haijawa mikubwa.

Ushauri

Kuonngeza hamasa ya juhudi binafsi kwenye kilimo, anawashauri viongozi wa halmashauri nchini wakiwamo wataalam wa huduma za ugani kutambua juhudi zinazofanywa na watu binafsi badala ya kujielekeza kwenye vikundi vinavyopata mikopo.

Anasema upatikanaji wa mbegu na ushauri kutoka kwa wakulima wazoefu unaweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa wakulima wanaoanza hivyo kupunguza uwezekano wa kupata hasara.

“Hata inapotolewa mikopo kwa vikundi, fedha hizo wasipewe watu ambao hawajaanza bali wawape wenye mashamba ili waweze kuboresha na kuendeleza kazi zao,” anasema.

Kwa wataalam wa kilimo, anasema wasisubiri kuitwa na wakulima bali wanapopata taarifa waende mashambani kuwasikiliza wakulima na kutatua changaoto zao suala litakalosaidia kuongeza uzalishaji wa mazao na tija.

Columnist: mwananchi.co.tz