Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Bila nguvu kiuchumi ushiriki wa wanawake katika siasa kitendawili

82747 Pic+wanawake Bila nguvu kiuchumi ushiriki wa wanawake katika siasa kitendawili

Mon, 4 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Takwimu zinaonyesha katika idadi ya Watanzania wote kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya 2012 wanawake ni zaidi ya asilimia 51. Hata hivyo, katika idadi hiyo, ni asilimia 30 tu ya wanawake wanaoshiriki katika uongozi wa siasa, vyama vya siasa, Serikali, Bunge na Mahakama.

Pamoja na dhamira ya Serikali ya kufikia usawa wa kijinsia katika uongozi yaani 50 kwa 50, hali halisi inaonyesha bado tungali mbali.

Katika dhamira hiyo, Tanzania imeridhia mikataba na matamko mbalimbali ya kimataifa yanayotoa haki kwa kila mtu kushiriki katika utawala wa nchi, haki za kisiasa na kiraia na mingine inayotoa miongozo ya ushiriki sawa wa kijinsia.

Kubwa zaidi ni azimio la Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) linalotaka ushiriki wa wanake na wanaume katika fursa za uongozi kuwa 50 kwa 50 ifikapo mwaka 2030.

Licha ya jitihada zote hizo, bado ushiriki wa wanawake katika siasa uko chini.

Hali hiyo inamwibua Idd Rajab, mtafiti katika eneo la sheria na sera, akibainisha vikwazo vya wanawake kushiriki siasa kadri ya matazamio ya mikataba hiyo na dhamira ya Serikali. Rajab aliyekuwa anatoa matokeo ya utafiti kuhusu ushiriki wa wanawake katika siasa katika uzinduzi wa programu ya utoaji elimu ya mpigakura Dar es Salaam hivi karibuni, anasema moja ya vikwazo kwa wanawake ni katika uteuzi wa wagombea ndani ya vyama.

“Uteuzi wa wagombea ndani ya vyama vya siasa ni mzuri kwa sababu ni wa haki, lakini hauna usawa. Wanawake wanakataliwa kugombea kwa sababu vyama vinatafuta mtu anayeuzika, mwenye fedha na mwenye nguvu ya ushawishi,” anasema.

Rajab anazungumzia utafiti ulifanyika katika wilaya tano za Kongwa (Dodoma), Urambo (Tabora), Singida Vijijini (Singida) na Bukombe (Geita), ukionyesha kuwapo idadi ndogo ya wanawake viongozi katika ngazi za Serikali

za mitaa ikilinganishwa na wanaume.

Katika wilaya hizo, utafiti umeonyesha kuna madiwani 13 wanawake dhidi ya wanaume 23. Pia kuna mwenyekiti mmoja wa kijiji wakati wanaume ni 96 na pia kuna wenyeviti wa vitongoji 13 wa kike dhidi ya 516 wanaume.

“Kwa kiasi kikubwa wanawake wanashiriki siasa kama wahamasishaji, waburudishaji, mawakala wa uchaguzi na wapiga kura lakini si kama wagombea,” anasema.

Anasema katika ngazi ya Serikali za mitaa ndiko kwenye changamoto nyingi zinazowakaza wanawake kushiriki siasa kuliko kwenye ngazi za kitaifa ambako wanawake wengi wanakuwa wameelimika.

Hata hivyo, akijadili suala hilo katika mkutano huo, Katibu mkuu wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu anasema ushiriki wa wanawake katika siasa umekuwa ukiongezeka siku za hivi karibuni.

“Kwanza namwomba mtafiti afanye utafiti zaidi aje na data za vyama vya hivi karibuni, kwa sababu hali ni tofauti. Kuna vyama ambavyo vinawapa kipaumbele wanawake tena kwa nafasi za kitaifa,” anasema Semu.

Anashauri pia uwezeshaji wa wanawake ujikite kwenye ngazi za msingi vijijini ili kupata wanawake wengi viongozi huko waliko wananchi.

“Wanawake lazima tutoke tuchukue hatua ya kushiriki na kugombea nafasi za uongozi na kuzika tuliyoaminishwa na mfumo kwamba hatuwezi au ni dhaifu katika uongozi.

“Suala la wanawake kuwa sehemu ya maamuzi ya kisiasa ni suala la nguvu, hatutapewa kirahisi tu ni lazima twende tukachukue nafasi zetu,” anasema.

Kutokana na changamoto hizo, Neema Makando, mkurugenzi mtendaji wa Gender Action Tanzania (Gata), anasema ndiyo sababu wameanzisha programu ya kuhamasisha watu, hasa wanawake, kushiriki siasa hasa katika chaguzi zinazokuja – Serikali za Mitaa Novemba 2019 na uchaguzi mkuu 2020.

“Tutatoa elimu ya urais nchi nzima kupitia mitandao na vyombo vya habari vya kawaida, tutafuatilia uhakiki wa wapiga kura, usajili wa wapiga kura, matumizi ya Tehama katika uchaguzi na kushirikishana taarifa za uchaguzi kupitia mitandao ya jamii,” anasema Makando.

Hoja nyingine inayoibuliwa kuhusu ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi, ni nguvu walizonazo kiuchumi na jinsi walivyojiandaa.

Hoja hiyo inajadiliwa kwa kina katika mkutano wa kuimarisha usawa wa kijinsia ulioandaliwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) hivi karibuni jijini Dar es Salaam, ukijaribu kuangalia suluhisho vikwazo vya usawa kijinsia.

Katika mkutano huo, Ruth Zaipuna, kaimu mkurugenzi wa Benki ya NMB anasema kinachotakiwa ni wanawake wenyewe kujiandaa kuwa viongozi na kuwa na weledi wa kutosha.

“Niwe mkweli. Ninaamini hakuna mwajiri au kampuni yoyote inayoweza kukupa kazi au cheo kwa sababu wewe ni mwanamke. Ni mpaka ulete matokeo mazuri, ni mpaka uonyeshe uwezo wako,” anasema Zaipuna.

Huku akijitolewa mfano wa mafanikio yake, Zaipuna aliyewahi pia kufanya kazi katika Benki ya Standard Chartered, anawataka waajiri kuwekeza katika rasilimali watu ili kujenga nguvu ya uongozi.

Hoja ya Zaipuna inaungwa mkono na Zuhura Muro, mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Lindam Group, akisema changamoto inayowakwamisha wanawake wasiamini kama wanawaweza wanapoingia kwenye uongozi.

“Tatizo ni kujihukumu wenyewe. Mwanamke akipewa nafasi anabaki kujiuliza, kweli nitaweza? Anaanza kujitilia wasiwasi yeye mwenyewe na akipata sauti inayompa wasiwasi ndipo anashindwa kabisa,” anasema Muro.

“Wanawake wajue hawatapewa nafasi kwa sababu wao ni wanawake, lazima wajiandae. Mwanamke aangalie elimu yake na vigezo vya kitaaluma na kujituma na kujiendeleza, lazima uwe na upekuzi uangalie dunia inakwenda wapi,” aliongeza.

Kwa kutambua hilo, Sanjay Rughani, ofisa mtendaji mkuu wa benki ya Standard Chartered, wanao mkakati maalumu ya kuwawezesha wanawake kushiriki uongozi wa benki.

“Karibu asilimia 50 ya uongozi wetu unashikwa na wanawake, kwa upande wa staff (wafanyakazi) asilimia 58 ni wanawake. Tunaona umuhimu wa kuwasaidia wanawake kujiendeleza kwani ukiwaendeleza umeendeleza jamii nzima,” anasema Rughani.

Hoja kama ya Rughani inatolewa pia na Sabasaba Moshingi, mkurugenzi wa Benki ya Posta, anayesema licha ya kuongeza jitihada za kuongeza viongozi wanawake katika benki hiyo, pia wanawasaidia wateja wanawake kumiliki uchumi.

“Kwa upande wa wateja wetu ambao wengi ni wanawake, tunawawezesha kupata mitaji ili waanzishe biashara zao na tuna dirisha maalum la wanawake,” anasema Moshindi.

Yote kwa yote, lipo tatizo la msingi katika jamii kama anavyobainisha Frank Ajilore, ofisa mtendaji mkuu wa IFC kwa Tanzania na Burundi, kuwa licha ya Tanzania kuwa na uandikishaji wa wasichana wengi kujiunga na shule kuliko wavulana, ni nusu ya wanawake hao humaliza sekondari.

Hii ina maana kwamba wanafunzi wengi wa kike wanaoandikishwa shule huishia njiani kutokana na changamoto zilizomo katika jamii.

Akizungumzia suala hilo, Ajilore anasema “hii ina matokeo makubwa kwa wanawake katika kushika nafasi za juu za uongozi. Kwa mfano utafiti uliofanywa na Chama cha Waajiri (ATE), asilimia 28 ya wafanyakazi katika sekta binafsi ni wanawake.”

Columnist: mwananchi.co.tz