Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Bila kunikata usingekipata

Mon, 25 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Jamani jirani yangu ni sheedah. Hana simile nakwambia. Kazi yake kumtwanga mke wake tu na ole wake mke wake atoe sauti. Atatwangwa zaidi na kutwangwa eti anataka kutoa siri nje ya nyumba, kana kwamba hatusikii kelele zote za mapigo pamoja na matusi anayoyaporomosha huku akimtwanga.

Ohoo, najua nyinyi washambenga wengine utasema kwamba hatwangi bure. Lazima mke ni mkorofi tu lakini kwanza mke ni sawa na mahindi ya kupukuchuliwa? Dah! Hata angekuwa mkorofi, inatoa ruhusa ya mwanamume kuonesha ukatili wa kukithiri? Lakini ajabu ni kwamba mke wala sio mkorofi.

Akiulizia pesa za matumizi, mtwango, akihoji kwa nini hakuna pesa za madaftari za watoto wao, wakati yeye anatamba na gari la fahari, mtwango, akijaribu kumtetea mwanaye aliyesingiziwa na baba eti amekosa heshima kwake kwa sababu hakuamka haraka kumfungulia mlango au hakucheka wakati baba akatoa kichekesho kisicho kichekesho, mtwango.

Ili mradi kero tupu na sisi majirani tunashangaa uvumilivu wa yule mama. Si bora angeondoka kabla hajatiwa kovu la maisha au hata zaidi lakini mtu akithubutu kumpendekezea hivyo, anasema kwamba hawezi kuacha watoto pale, maana bila yeye kujaribu kuwatetea watateseka zaidi.

Ngoja watoto wakue waweze kujiamulia wenyewe.

Lakini, juzi huyu baba akazidi. Si tu alimtwanga, bali alichukua kisu eti anataka kumkatakata ulimi na midomo yake asiweze kuleta vimaneno maneno yake. Yule mama alivyotoa yowe, hatukuweza kuvumilia tukakimbilia pale na kulazimisha kuingia. Kwanza yule baba alitutishia na kisu chake lakini mwenzangu akamuwahi. Kisha yule mama tukataka kumkimbiza hospitali maana alivyokatwakatwa, damu ilikuwa inatoka kwa wingi. Na si unajua taratibu za huko. Ilibidi ajaze fomu ya polisi pia ili aweze kutibiwa. Bahati mbaya, yule mume wake alikuwa ameshafika polisi kabla hajaweza kujaza fomu.

Baba mwenyewe kwanza akadai kwamba mke wake alitaka kuwadhuru watoto ndiyo maana ikabidi aingilie kati kuwaokoa. Katika kufanya hivyo, mke alianguka na kujikata midomo kwenye ncha ya meza. Baada ya kusema hivyo, alimkazia macho kama vile kumtisha asiseme.

Wote tukawa kimya kuona kama mke wake atakubali uongo huo au la. Alisita kwa muda, lakini mwisho akasema kwa maumivu makali maana damu bado ilikuwa inatoka na ulimi ulikuwa umevimba sana.

‘Si kweli! Mume wangu alinipiga na kunishikia kisu eti nina mdomomdomo, hivyo alitaka kuutoa.’

Kidogo mume amkimbilie na kuanza kumtwanga tena lakini sisi tuliingilia kati huku tukishangaa kwa nini polisi hawafanyi kitu. Kisha tulihakikisha kwamba fomu iko tayari na kumkimbiza hospitali ambapo mama alilazwa. Kwa kuwa mume alikataa katakata kuja kumwona au kumlipia kushonwa kwa midomo na ulimi pamoja na dawa nyingi kutokana na kupoteza damu nyingi na maumivu yake makali, majirani tulichangishana na mke wangu aliamua kulala naye usiku ule hadi apate nafuu.

Basi alilala kule hospitali siku tatu! Baba hakuja kumwona lakini tulisikia alienda polisi na kuhakikisha kwamba hakuna kesi.

Kwa mara nyingine, tulishangaa kwa nini polisi hawataki kuchukua hatua yoyote mbele ya ukatili wa namna hii lakini mwenzetu mmoja alipojaribu kuuliza aliambiwa asiingilie kesi, wanafanya upelelezi usiku na mchana.

Alipojaribu kuuliza ulihitajika upelelezi gani tena, kidogo wambambikie kesi eti anatembea na yule mama ndiyo maana alitwangwa.

Baada ya hapo, mama alikataa kurudi nyumbani. Alihamia kwa dada yake na kudai aletewe watoto wake pia. Baba alikataa eti mama anawaharibu watoto na maneno yake. Mwisho mama ikabidi aende mahakamani. Kutokana na majeraha yake mdomoni ambayo yalikuwa yameacha makovu ya kudumu, hata waandishi wa habari walianza kufuatilia kesi na kuandika habari za ukatili huo. Baba aliona anaanza kuumbuka kwa hiyo aliitisha kikao cha pande zote mbili ili kujaribu kutafuta suluhisho.

Kwanza mama hakutaka kuhudhuria maana alijua tabia ya wakwe na shemeji zake lakini wazazi wake walimwambia watakuwa naye bega kwa bega. La muhimu ni kupata watoto wasiteseke zaidi.

Basi mama hakukosea. Wakwe na mashemeji walimtupia kila aina ya lawama. Mkorofi, malaya anayefuata mabwana wa nje, mwanamke gani anayetangaza matatizo ya nyumbani hadharani. Kimila, ni mwiko kabisa mke atoe nje matatizo ya nyumbani, kazi yake ni kuvumilia tu na kumtegemea Mungu basi. Hebu ona alivyomwaibisha mume wake hadi nchi nzima inataka kumlaumu wakati alikuwa anamwajibisha mke wake kidogo tu. Inakuwaje kwa watoto wakienda shuleni? Wanafunzi wenzao wote wanawaangalia. Wataweza kweli kusoma katika hali hii?

Kwa hiyo, huyu mama ni mbomoaji wa ndoa, ni mbomoaji wa nyumba yao, ni mbomoaji wa heshima wa mume wake aliyepewa na Mungu. Kwa namna hiyo, hawezi kupewa watoto tena. Njia pekee ni kufuta kesi warudiane ili aibu isiendelee.

Ndugu zake mama nao walijibu mapigo, kwa kumlaani yule baba kwa ukatili wake. Kimila hatakiwi kumpiga mke wake na akitaka mambo yasawazishwe kimila, lazima atafute ng’ombe mweupe peee kama ishara ya kwamba amekosea na hatarudia tena.

Wakwe na mashemeji yalizidi kuja juu lakini yule mama hakusema kitu hadi mwisho alisimama na kusema kwa taabu kutokana na majeraha yake.

‘Kwa nini hatuangalii chanzo?’

Mashemeji walijifanya hawaelewi.

‘Unasema nini mwanamke mshenzi wewe.’

‘Nitukane mnavyopenda. Nipe majina yote mliyo nayo katika kapu lenu lakini ukweli unabaki palepale. Usingenipiga na kunikata na kisu hayo yote yasingetokea.’

Akaamka na kutoka huku akisema.

‘Nasubiri haki yangu!’

Watu wakabaki wanatumbuliana macho.



Columnist: mwananchi.co.tz