Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Barua ndefu kwa CCM: Changamoto, maboresho na mbadala viti maalumu

60951 Ccm+pic

Mon, 3 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Waheshimiwa viongozi, Ilani ya CCM kupitia kifungu namba 167(a) inasema ‘Katika kipindi cha utekelezaji wa Ilani ya 2015 – 2020, Chama kitaielekeza Serikali kuendelea kuweka utaratibu wa kikatiba na kisheria utakaowawezesha wanawake kushika nafasi sawa (50/50) za uongozi katika vyombo vya maamuzi katika ngazi zote.’

Kifungu hiki kinaweka wazi nia ya CCM kuchukua hatua muhimu kuhakikisha wanawake na wanaume wanashiriki kikamilifu katika ngazi za kutoa maamuzi. Bunge kama chombo kikubwa cha maamuzi lina uwakilishi wa wanawake upatao asilimia 37, asilimia 30 ni wale waliopatikana kwa utaratibu wa viti maalumu na asilimia 7 wakitokea majimboni.

Hii ina maana kwamba kuna upungufu wa wanawake kwa asilimia 13 ndani ya Bunge ili kufikia 50/50 Ilani ya CCM.

Kati ya madiwani wapatao 4,000 nchini Tanzania, wanawake madiwani waliochaguliwa kutoka kwenye kata ni takribani 240 ni sawa na asilimia 5 tu.

Tasnifu yangu ya Shahada ya Uzamivu inaangazia kwa undani masuala ya sheria zinazowawezesha au kuwakwamisha wanawake kushiriki katika ngazi za maamuzi. Baada ya kuonana na wanawake wanasiasa wakiwamo madiwani na wabunge, nimebaini kuwa utekelezaji wa viti maalumu japokuwa umetuletea baadhi ya mafanikio, haufuati malengo ya kuanzishwa kwake.

Changamoto za Viti Maalumu

Pia Soma

Mosi, ni kuhusu hadhi ya viti maalumu. Kuna kanuni na miongozo inayozuia madiwani viti maalumu kuwa wajumbe katika kamati za maadili katika kata. Katika Halmashauri nyingine kuna mazoea ya kutowaruhusu madiwani viti maalumu kuwa wajumbe wa kamati za fedha.

Hata kwenye zile Kamati ambao wanawake viti maalumu ni wajumbe mfano kamati za Ukimwi, Huduma za Jamii, na Mipango Miji, wanawake hawa hawaruhusiwi kuwa wenyeviti.

Pia kuna sheria zinazowanyima fursa madiwani viti maalumu kuwa meya, naibu meya, wenyeviti wa halmashauri za majiji, miji na wilaya. Madiwani viti maalumu hawaruhusiwi hata kukaimu uenyekiti wa kamati ya maendeleo ya kata ikiwa diwani wa kuchaguliwa ana udhuru.

Kuna baadhi ya kata ni bora kwa mwenyekiti wa Kijiji ama mtaa kukaimu uwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya kata, kuliko diwani viti maalumu. Katika hili tukumbuke kuwa wabunge viti maalumu nao ni madiwani katika kata zao.

Kwa upande wa Bunge, ile kanuni ya kutoruhusu wabunge viti maalumu kupata fedha za maendeleo, na kifungu cha Katiba kinachowanyima fursa kuteuliwa kuwa waziri mkuu vinawaweka wanawake viti maalumu katika hadhi ya chini.

Kimsingi, sheria, kanuni na mazoea yanayowanyima wanawake viti maalumu fursa uongozi katika halmashauri na Bunge, zinatoa taswira kuwa kama taifa tumewaweka wanawake viti maalumu katika hadhi ya chini, na tumeshaweka hitimisho hawana uwezo wa kuongoza au kuwa sehemu ya maamuzi fulani.

Hii ni kinyume na kifungu namba 4 cha Mkataba wa Kuondoa aina zote za Ubaguzi dhidi ya wanawake wa mwaka 1979 ambapo Tanzania imeridhia.

Mkataba huu unatambua viti maalumu kama hatua za mpito ambazo hazitakiwi kukumbatia ama kuleta unyanyasaji na unyanyapaa kwa wanawake.

Pili, viti maalumu vimekuwa vikiwanufaisha wanawake wachache licha ya lengo lake la kuwajengea uwezo na uzoefu wanawake wengi, ili waende kwenye siasa za majimbo.

Tangu kuanzishwa kwa viti maalumu takribani miaka 34 iliyopita, mpaka sasa Tanzania ina wanawake asilimia 7 tu kutoka majimboni. Hivyo, kwa miongo takribani mitatu na ushee, na ikiwa vikifutwa leo, viti maalumu vitakuwa vimefikia lengo lake kwa asilimia 7 tu.

Moja kati ya mizizi ya tatizo hili ni kutokuwepo kwa ukomo wa muda kwa mwanamke mmoja kuwa mwakilishi kupitia viti maalumu. Ukomo wa uwakilishi wa viti maalumu, kama ungekuwa vipindi viwili tu, ungewezesha wanawake wengi kwenda kushindana majimboni/katani, na kutoa fursa ya kada nyingine ya wanawake kupata uzoefu wa kisiasa.

Mpangilio huu ungesaidia kupiga hatua za msingi na za haraka katika kufikia 50/50.

Kuna hoja kuwa wabunge ni wabunge na madiwani ni madiwani, hivyo kama mbunge wa jimbo/diwani wa kata hana ukomo pia mbunge/diwani wa viti maalumu asiwe na ukomo ikiwa tu ataendelea kushinda kura za wale wanaowapigia kura.

Tukumbuke kuwa wanawake viti maalumu japokuwa wana majukumu ya kibunge/kidiwani pia wanatumikia lengo la nyongeza. Wako katika viti hivyo ili kupata uzoefu utakaowawezesha kushiriki katika siasa za ushindani, kwa hiyo wanawake wengi zaidi inabidi wapate fursa ya kupata uzoefu huo. Kuwekwa kwa ukomo wa kuwa mbunge wa kiti maalum kutaendana na malengo ya kuanzishwa vitu maalum ili kurekebisha changamoto ambazo zimekuwa zikiwakwamisha wanawake kushiriki kikamilifu katika vyombo vya maamuzi.

Kutokuwa na ukomo wa kisheria ama kikanuni kunawapa wanawake walio katika viti maalumu faida ya ziada katika kuendelea kuhodhi viti hivyo, kwa kuwa wana mtandao mkubwa katika chama na katika mabaraza ya wanawake ya vyama, faida ambayo wanawake wanaowania viti maalumu kwa mara ya kwanza hawana.

Hili suala la uhodhi wa viti maalumu ni la vyama vyote, lakini kwa kutumia nafasi yake kama chama tawala CCM ina wajibu wa kutenda kwa mfano, ili kuhakikisha viti maalumu vinatekelezwa kwa namna inayokidhi madhumuni ya kuanzishwa kwake hususani kuwapa wanawake wengi fursa ya kupata uzoefu wa kisiasa kuelekea majimboni.

Itaendelea Jumatano

Victoria Lihiru ni Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu Chuo Kikuu Cape Town, Afrika Kusini. [email protected], +255 713085139.

Columnist: mwananchi.co.tz