Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Baraka zingine zinaweza kuwa balaa wa balaa

58476 Pic+baraka

Mon, 20 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Waishiwa wenzangu,

Kweli nina mashaka na akili za watu wengine. Hebu angalia hiyo barua kutoka kwa mtu fulani. Ananikumbusha yule mfalme aliyekurupuka kujaribu kuzuia mawimbi kwa kuamini, akiamuru tu, mawimbi yatarudi nyuma. Lakini hebu nisiseme sana. Msome wenyewe.

Mwishiwa Makengeza,

Nakuandikia wewe, ingawa najua kichwa chako si kizuri maana kazi yako kukejeli tu, kukejeli tu wakati kazi yetu ni kuungana kujenga taifa basi. Lakini nashangaa kwamba wajenzi wenzangu hawajaona umuhimu wa hayo ambayo nataka kusema hivyo imebidi nikufuate wewe na ufyatu wako.

Suala ni hili. Mvua ni beberu. Au tuseme ni beberu mamboleo. Kwa nini tusiishtaki? Ndiyo, usicheke. Kulingana na sheria zetu mpya tukufu zilizopitishwa na bunge letu tukufu, mambo ya kuharibu utukufu na watukufu wa nchi yetu si tu ni marufuku bali ni kosa la jinai. Kwa misingi hii, hii mvua ya wiki jana tusemeje? Ilivyonyesha mfululizo, imeleta picha mbaya juu ya nchi yetu, na kuzuia jitihada zetu za maendeleo. Mabeberu walidai kwamba wanatuletea mema kumbe wao na vibaraka wao walileta majanga tu. Na mvua ni vivyohivo. Tumeimba miaka yote mvua ni baraka, sasa baraka iko wapi? Mvua imenunuliwa na mabeberu.

Lakini usinielewe vibaya Makengeza. Siongelei jinsi watu walivyokumbwa na mafuriko. Shauri yao. Wameambiwa wahame lakini kwa kuwa hawataki adha na ada za kusafiri kutoka mbali kutafuta kazi kila siku wamejibana hapohapo kwenye mafuriko. Ndiyo maana hujaona waheshimiwa wetu wa wilaya na mkoa wakihangaika kuwatembelea au kuwasaidia hawa waathirika wa mafuriko. Ingekuwa suala muhimu, tungewaona ukurasa wa mbele wa magazeti yote, kama katika masuala mengine hata madogomadogo kama umuhimu wa magari yao, maisha ya fahari n.k. Achana na hao. Walijitakia.

Pia Soma

Nazungumzia mambo mawili hasa. Mosi, hii si mara ya kwanza mvua kutuumbua sisi sote wenye nia njema ya kuleta maendeleo. Tena ninao uhakika kwamba mvua imejiunga rasmi na wale wafuasi wengine wa ubeberu mambo leo, yaani vyama vya wapinzani. Ikaleta mafuriko kwa mabasi yetu mara ya kwanza, hatukukemea wala hatukushtaki hiyo mvua, ndiyo maana wapinzani walitamba kwa kutukosoa kwa nini tuling’ang’ania kujenga pale. Ujinga mtupu. Kosa ni la mvua si la ujenzi. Na sasa, kwa kuwa mvua haikukemewa na kushtakiwa imerudia tena kuleta mafuriko na kutuumbua zaidi. Nakumbuka tulivyorukaruka na kutoa povu kutetea msimamo wetu wa kujenga pale, licha ya maoni ya wataalam na wananchi, sasa tunakula aibu na mkurupuko wetu wa kuleta maendeleo shauri ya hii mvua ya kishenzi.

Pili, Makengeza, umewahi kufikiria jinsi mvua inavyoharibu jitihada zetu za kupata fedha za maendeleo. Nimeona kwa siku hizi mbili za jua (MATAGA oyee kwa kushinda mvua na kuleta jua tena. Mvua iende huko shambani inapotakiwa) wauguzi wetu wa barabarani wanajimwaga kwa nguvu sana kutibu magari yetu kwa mashine zao muhimu za usalama barabarani. Risiti zao kwanza ni kielelezo halisi cha usalama, lakini pia wanajitahidi sana kujaza pengo la mapato lililojitokeza kwa zile siku za mvua. Mvua imezuia makusanyo ya mapato. Kwa nini isishtakiwe maana inarudisha nyuma jitihada zetu za kuwaletea wanyonge maendeleo?

Na si mapato ya taifa tu. Hata buti za hawa wauguzi hazing’ai tena kutokana na fedha ya kubrashi viatu vyao. Ndiyo maana wanahaha. Jana nilisimamishwa kwenye taa kule kwenye barabara ya Mandela eti nimeruka taa nyekundu huko nyuma. Alijuaje, eti mtu mmoja huko (hajasema mwuguzi mwenzie) amepiga simu kusema kwamba gari la aina yangu (hajasema namba za gari) liliruka taa nyekundu. Sasa tayari anataka nitoe pesa ingawa kwa kweli, sikuona kile kifaa muhimu kinachoonesha kwamba wanatujali na uendeshaji wetu. (Acha ujinga Bwana ee. Siongelei tochi! Naongelea mashine za EFD) Mikono mitupu.

Sasa unajua Makengeza, mimi niko tayari kulipa kodi na tozo zote, si kama hawa wafanyabiashara wengine wasio wazalendo ambao eti wanafunga biashara zao kwa kudai kwamba kodi na tozo zimezidi. Kwa hiyo nilikuwa tayari kabisa kutoa mchango wangu kwa ajili ya kodi ya taifa na ya viatu pia lakini niliudhika kutozwa kodi ambayo haikuwa sahihi. Naendesha kwa uangalifu mkubwa sana, iweje nidaiwe? Alipoona sikubali, kadai kwamba sijalipa bima ya gari, ikabidi nishuke na kumwonesha kwamba kweli nimelipa hadi mwisho wa mwaka huu. Akasikitika, akasononeka, akaangalia buti zake zisivyong’aa lakini mwisho ilibidi aniache niondoke.

Unaona Makengeza? Kutokana na hiyo mvua huyu dada ameshindwa kabisa kubrashi viatu vyake hadi analazimika kutafuta hata makosa ambayo hayapo. Hali hii inamdhalilisha yeye, pamoja na wenzake, pamoja na jitihada za serikali yetu tukufu kuongeza mapato yake kwa udi na ubani, kwa lila na fila, kwa hamu na ghamu kwa … si unajua mwenyewe. Yote hayo ni sababu ya mvua. Lazima mvua ikomeshwe kabla ya kuleta madhara zaidi katika muonekano wetu mbele ya umma. Mvua ishtakiwe kwa uchochezi. Imetumwa na mabeberu makusudi. Hawataki maendeleo yetu na wanafanya juuchini kukwamisha jitihada zetu.

Sisi twajua mvua ni baraka, iweje igeuke balaa kama hakuna mkono wa beberu hapa. Nimesema!

Columnist: mwananchi.co.tz