Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Balozi Mpungwe: Nyerere alinihimiza kuleta wawekezaji wa Afrika Kusini

57093 Pic+balozi

Mon, 13 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Ami Mpungwe amesema Rais wa Awamu ya Kwanza, Julius Nyerere ndiye aliyemhimiza kuleta wawekezaji kutoka Afrika Kusini.

Amesema kutokana na hilo hakutetereka kwa maneno ya watu waliosema kwamba alikuwa anauza nchi kwa makaburu.

Mpungwe alisema hayo Ijumaa iliyopita katika mahojiano maalumu na Mwananchi alipotembelea ofisi za kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) zilizopo Tabata Relini jijini Dar es Salaam.

Alisema aliteuliwa kuwa balozi wakati ambao nchi ilikuwa inatoka katika ujamaa na kuelekea katika uchumi wa soko na kuanza kuvutia uwekezaji. Alitumia uzoefu wake wa kuhudumu katika nafasi mbalimbali ndani ya Serikali ikiwamo ya mshauri wa Rais (Ali Hassan Mwinyi) kujua mwelekeo wa nchi na mahitaji yake.

“Wakati ule nchi ilikuwa inafanya ubinafsishaji na kiliundwa chombo maalumu cha kufanya hivyo (PSRC) ndiyo maana hata waliokuwa wanasema nauza nchi niliwashangaa maana mimi sikuwa chombo hicho. Nilileta wawekezaji wengi, wengine walikataliwa.

“Kama kuna mtu alikuwa ananitia moyo kuleta wawekezaji basi ni Mwalimu Nyerere. Kila nilipokuwa nikipata utata nilikwenda kwake... nikamwambia watu wanalalamika eti nauza nchi kwa makaburu, akaniamba wapuuze. Hata nilipokuwa nikisikia maneno mengine nilisema watu hawajui kama nilikuwa nimetumwa na viongozi wangu,” alisema.

Pia Soma

Alisema anashangaa waliokuwa wakisema anauza nchi wakati alishiriki binafsi katika mapambano ya ukombozi na kuweka rehani uhai wake hivyo kusema alikuwa mzalendo pengine kuliko hao waliokuwa wakisema anauza nchi.

Alisema kwa kuwa alifanya kazi za kisera na za ukombozi kwa muda mrefu, alipofika Afrika Kusini aliona ni vyema kubadili uhusiano baina ya nchi hizo mbili kutoka ule wa kiukombozi kuwa wa kiuchumi na alikuwa na marafiki wengi akiwamo Rais wa kwanza mweusi wa nchi hiyo, Nelson Mandela na aliyemfuatia, Thabo Mbeki.

Alisema kwa kuwa na marafiki hao, alipata uungwaji mkono kwa kiasi kikubwa katika kutafuta wawekezaji kazi ambayo alisema alijikita zaidi huku akimwachia naibu balozi majumu mengine.

Alisema licha ya kuleta wawekezaji wengi ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika kiuchumi, wapo waliokataliwa kutokana na kelele nyingi.

Alisema wawekezaji waliokataliwa walikuwa wa nyama pia kutoka Afrika Kusini ambao walitaka kuanzisha viwanda vya nyama na kukichukua kiwanda cha Tanganyika Packers kwa ajili ya kuzalisha nyama na ngozi.

“Walikuja wakafanya utafiti wakasema wamefurahi sana wakasema balozi, tunaweza kutengeneza kiwanda chenye hadhi ya kuzalisha bidhaa za kimataifa wakasema kwa kushirikiana na kampuni ya utengezeaji wa magari, wataanzisha kiwanda cha viti vya magari ya ngozi, lakini walikataliwa,” alisema Mpungwe ambaye sasa ni mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda cha Sukari cha Kilombero.

Alisema kilichokwamisha na kelele nyingi kutoka kwa baadhi ya watu wakiwamo wabunge ambao walidai kuwa Balozi amehongwa.

“Mimi kwa sababu ni balozi sikuwa na sauti kwenye bunge wakati huo waziri wangu (wa Mambo ya Nje) alikuwa (Jakaya) Kikwete nikamwambia mbona nashambuliwa huko haunitetei,” alisema.

Alisema anajivunia kuwa balozi ambaye ameleta wawekezaji wengi kuliko wote na kwamba wote aliowaleta, biashara zao zimeshamiri akitolea mfano wa Vodacom, Kilombero Sukari na Benki ya NBC.

Kuhusu sera ya viwanda na mabalozi wa sasa alisema kazi ya balozi ni kutumwa kutafuta wawekezaji lakini kufanikisha uwekezaji huo ni suala la mamlaka za ndani.

“Mabalozi wanaweza kujitahidi na mimi naamini wanajitahidi lakini vyombo vya ndani vinapaswa kuwa katika namna ya kuwapokea wawekezaji hao kwa mtazamo chanya. Mazingia ya biashara yalikuwa changamoto hata wakati huo lakini wawekezaji wanavutiwa zaidi na utajiri wa asili, sera za nchi na soko, mambo mengine sio kivutio kikubwa,” alisema.

Kustaafu akiwa na miaka 48

Balozi Mpungwe, ambaye alizaliwa Februari 1951 huko Ifakara mkoani Morogoro, alistaafu kwa hiari akiwa na umri wa miaka 48 kazi yake ya mwisho serikalini ikiwa hiyo ya Balozi wa Tanzania Afrika Kusini na hiyo ilikuwa mwaka 1999.

Alisema tangu akiwa mdogo alipewa majukumu makubwa ya uongozi. Alisema akiwa na miaka 34 , alikuwa mshauri wa Rais... “na hapo ndipo ujana wangu ulikoma,” anasema huku akicheka.

“Mwaka 1998 nilimfuata Rais (Benjamin) Mkapa nikimuomba kustaafu mapema nikiwa na miaka 47, alinikubalia lakini akaniambia nikae mwaka mmoja kwanza ndipo nikaja kustaafu nikiwa na miaka 48. Nilitaka kupumzika”

Mpunge ambaye ana Shahada ya Sayansi ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema hakufaidi kabisa ujana wake kwani alitumia muda wake mwingi katika harakati za ukombozi katika mataifa mbalimbali yakiwemo Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe na baadaye migogoro ya Rwanda.

“Nilikuwa kiongozi katika harakati za ukombozi wa Afrika Kusini, kuiona nchi hiyo ikiwa huru na Mandela akiwa huru kwangu lilikuwa ni jambo kubwa sana katika maisha yangu nikaona hakuna jambo lingine linaweza kunifurahisha katika maisha yangu hata ungenipeleka Marekani, Tokyo, Japan au London Uingereza,” alisema Mpunge akielezea sababu yake ya pili ya kustaafu mapema.

Alisema jambo la tatu ni kuona fursa katika biashara. Pamoja na kuchoka, wakati akifanya kampeni za kukuza uwekezaji kati ya Tanzania na Afrika Kusini aliona fursa katika biashara eneo ambalo aliamua kuhamia.

Kuhusu uchumi

Balozi Mpungwe alisema jambo la msingi katika kukuza uchumi ni kuangalia tulipoanguka wakati wa harakati akisema si tu kwamba viwanda vilikosa usimamizi, bali kulikuwa na mambo mengine kama kubadilika kwa mifumo ya kiuchumi ya dunia.

“Uwezo wa kuzalisha sasa inabidi uwe wa kiushindani, leo kiwanda kinachozalisha matairi 100 kwa siku hakiwezi kushindana na kile kinachozalisha matairi milioni mbili kwa siku, kama uzalishaji ni mdogo bei inakuwa kubwa kama uzalishaji ni mkubwa bei inapungua ndiyo maana leo nguo zinazotoka China na India ni bei nafuu kuliko zinazotengenezwa hapa,” alisema balozi huyo mstaafu mwenye hisa katika kampuni ya DSTV nchini.

Alisema kutokana na mabadiliko ya mambo mbalimbali hivi sasa, anatumia muda wake mwingi kuandika historia yake na kujifunza mambo ya baadaye.

“Wakati sisi tunakua, tulikuwa tunatafuta kazi, tunakoelekea kazi itamtafuta mtu. Itakuwa ni nani mwenye uwezo wa kufanya kitu fulani.”

Alisema kuna haja ya kuwa na mjadala juu ya mfumo wetu wa elimu kwa kuwa una changamoto nyingi ambazo zinatakiwa kutatuliwa ili ziendane na mabadiliko yanayoendelea duniani.

Columnist: mwananchi.co.tz