Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Bajeti itekelezwe ili itatue kero vijijini

Wed, 27 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bajeti ya serikali ya awamu ya tano ya mwaka 2018/19 imepita kama ambavyo ilitarajiwa.

Katika bajeti ya mwaka 2018/19 serikali imepanga kuwa na mapato na matumizi ya Sh32.4 trilioni. Kati ya hizo, Sh20.4 trilioni zinatarajiwa kutumika katika matumizi ya kawaida na Sh12 trilioni katika mipango ya maendeleo.

Pamoja na hoja zote zilizojitokeza wakati wa mjadala na nje ya Bunge, katika upigaji kura Bajeti hii imeungwa mkono. Kwa mantiki hiyo, Watanzania wengi kupitia wabunge wao walioipitisha, wana matumaini makubwa kuwa itakwenda kujibu kero zao na kuwaondola umaskini.

Hofu ya utekelezaji

Kwa bahati mbaya sana, tumezoea kuona bajeti inapitishwa kwa mbwembwe nyingi, lakini baadaye fedha zimekuwa hazipelekwi katika maeneo yaliyokusudiwa kwa wakati.

Katika bajeti ya mwaka 2017/18 tumeshuhudia fedha za maendeleo zilizotengwa karibu nusu hazikupelekwa katika maeneo yaliyokusudiwa.

Ingawa serikali, imeahidi kabla ya mwaka wa fedha kuisha fedha nyingi zitakuwa zimefikishwa sehemu ambazo zilipangwa lakini kwa kuchelewa huku ni wazi haziwezi kufika zote wala kufanya kazi zilizokusudiwa.

Hata hivyo, tunawapongeza baadhi ya wabunge kwa kutoa michango makini na mawaziri kwa kuwa wasikivu walipokuwa wakipokea maoni ya wabunge ili kuboresha bajeti za wizara zao.

Lakini, watambue kuwa kupitisha bajeti ni jambo moja na kuitekeleza ni jambo jingine.

Kama nilivyosema awali, imekuwa ni kawaida bajeti kupitishwa kwa mbwembwe, lakini baadaye utekelezaji wake unakuwa ni hafifu.

Miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakiathiri utekelezaji wa bajeti na kukosekana vipaumbele vichache ambavyo vikitekelezwa vitaweza kusisimua sekta nyingi.

Wachumi kadhaa, wamekuwa na maoni mbadala juu ya bajeti, kwa maelezo kuwa licha ya uchumi wa Taifa kuonekana unakua lakini uchumi huo siyo jumuishi na ndiyo sababu bado watu wengi ni masikini.

Hivyo, wamekuwa na ushauri kuwa ili uchumi ukue kugusa maisha ya mamilioni ya Watanzania ni lazima sekta zinazogusa watu wengi zipewe kipaumbele.

Miongoni mwa sekta ambazo zinapaswa kutazamwa ni sekta ya kilimo na utalii, ambazo zinaongoza kwa kutoa ajira nyingi na kuingiza mapato kwa taifa.

Watanzania asilimia zaidi ya 70 wanategemea kilimo, hivyo kama kilimo kikiboreshwa kwa maana ya kupatikana teknolojia za kisasa kwa gharama nafuu, ruzuku, pembejeo na masoko ni wazi Watanzania wengi watanufaika.

Hivyohivyo kwa sekta ya utalii, kwani kwa sasa ndio inaongoza kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni zaidi ya asilimia 25 lakini pia hata katika pato la taifa mchango wake ni zaidi ya asilimia 18 kwa sasa.

Endapo jitihada zingeongezwa katika utalii, ambao unaweza kutoa ajira kwa mamilioni ya Watanzania bila kujali viwango vya elimu, faida ingeonekana.

Hivyo katika bajeti, ilitarajiwa walau sekta hizi, zingepewa uzito mkubwa na kuongezwa fedha za miradi ya maendeleo na manufaa yangeonekana haraka zaidi.

Kwa utalii ilitarajiwa kuongezwa fedha za kuboresha miundombinu kurahisisha watalii kuvifikia vivutio lakini pia kuongezwa fedha za kutangaza vivutio vya utalii.

Hata hivyo, kwa kuwa tayari bajeti imepita kinachotakiwa ni kuhakikisha fedha za maendeleo zilizotengwa katika sekta mbalimbali zinatolewa kwa wakati ili zikatatue kero za wananchi.

Watanzania wengi bado wana imani kubwa na serikali yao, hivyo sasa ni muhimu watendaji wa serikali kuhakikisha bajeti inakwenda kujibu kero zao na hili litawezekana kama miradi ya maendeleo itatekelezwa.

Mussa Juma ni mwandishi Mwananchi mkoani Arusha. 0754296503

Columnist: mwananchi.co.tz