Hivi unaona mambo yanavyokwenda pale klabu ya Yanga?Hali inasikitisha sana mambo hayako sawa kabisa sio tu nje hata ndani ya mamlaka inayoongoza klabu hiyo kwasasa.
Taratibu naanza kuiona Ynaga kama basi ambalo linatoka katika njia kuu na kuanza kutafuta pori na kupotea njia hakuna kinachonyooka kwasasa.
Uongozi hauna utulivu tofauti na wakati walivyoingia madarakani Mei 6,2019 ukiwa ni uongozi uliobeba matumaini makubwa kwa mashabiki na wanachama wake.
Nyuso za kila mdau wa klabu hiyo sasa hauna furaha hasa wakiangalia maisha yao lakini hatua mbaya Zaidi wakitazama maisha ya majirani zao yanavyokwenda kwa utulivu mithili ya mtu anayekunywa mtori mtamu, ndiyo, Simba wanakwenda kwa utulivu.
Hatua mbaya Zaidi klabu hiz mbili zinaishi maisha kama majirani wa kizamani katika nyumba za kupanga kwamba kama jirani anapika nyama leo lazima na mwenzake naye atafute kitu cha namna hiyo.
Juzi nimemsikia Dk Mshindo Msolla akitoka hadharani na kueleza anguko la kiuchumi la klabu hiyo akitoa maelezo marefu juu ya hali ya kifedha aliyoikuta ndani ya klabu hiyo.
Inawezekana ni ufafanuzi mzuri ambao ulihitajika kwa wadau wa Yanga kujua hali ilivyo na jinsi alivyoikuta lakini nikajiuliza sqali moja hivi ni nani ni mshauri mkuu wa Dk Msolla ndani ya Yanga?
Sioni kama Dk Msolla anamshauri mzuri ambaye anapaswa bado kuendelea kumsikiliza. Sitaki kukubali haraka eti kamati ya utendaji ya Yanga hasa wajumbe wake ndio wanamshauri kiasi hiki mwenyekiti wao.
Ukimsikiliza Dk Msolla ni wazi kwamba hakuwa anajua ndani ya uongozi ambao alikuwa akiomba ataingia na kukutana na changamoto za aina gani.
Napata wasiwasi pengine Dk Msolla alidhani kuna urahisi sana katika kuongoza klabu kama Yanga na kwamba waliomtangulia hawakuwa wanajua jinsi ya kuibadilisha klabu hiyo.
Nikifika hapo naanza kumtafuta mtu aliyekuwa nyuma ya Dk Msolla katika kutafuta nafasi hiyo hivi ni mtu aliyekuwa anaijua Yanga kwa undani kweli au alikuwa anaijua Yanga kupitia jezi ya njano na kijani ambazo wanazivaa.
Nikajiuliza hivi yule swahiba wake mkuu ambaye aliivuruga hata Ndanda akidhani ataisaidia kisha akakimbia ndiyo yuleyule amekuja na huku na kuendelea kuwa nyuma ya Msolla?
Najiuliza maswali haya kwa kuwa halikuwa suala la kificho kwamba Yanga ilihitaji kuongozwa na mtu ambaye hata kama hana fedha basi alihitaji kuwa na akili ya kutosha katika kujua jisni gani ataikomboa klabu hiyo katika hali ngumu ya fedha ambayo ipo sasa.
Hiakuwa siri kwamba Yanga ilikuwa na madeni mengi kuanzia kwa wachezaji mpaka katika taasisi mbalimbali ambazo ilikuwa ikifanya nazo kazi.
Sio jambo jipya kwa uongozi wa Dk Msolla eti kukabiliana na madeni na kifupi ni kwamba uongozi wowote kurithi madeni au hata kurithi mapato ya fedha katika akaunti lakini kwa hali ilivyokuwa ndani ya miaka miwili ya nyuma hutarajii kukuta mambo mazuri ya kiunchumi ndani ya klabu hiyo.
Inawezekana Dk Msolla hakulijua hili na bahati mbaya zaidi wale aliotarajia kumsaidia nao wakawa hawana ubora w ahata kumsaidia kimawazo.
Sidhani kama mashabiki wa Yanga wanahitaji kuendelea kusikia kwamba klabu yao ina ugumu wa maisha kiasi gani kwani hizi ni kelele walizosikia saba nyuma kiasi cha wao kuingia kazini kufanya usajili mkubwa tena wakichanga wenyewe sasa ni wakati wao kusikia uongozi mpya umekuja na akili gani juu ya kukabiliana zaidi nan a hali ngumu hiyo sio tena kuendelea kusomewa madeni ambayo hajalipwa huku bado klabu ikiwa na hali ngumu.
Ushauri wangu kwa Dk Msolla sasa ni kwamba aachane na mshauri wake mkuu ambaye sioni kama anamsaidia na kujikita katika mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji.
Vinginevyo wakati wowote kwa hali ilivyo sasa sitashangaa kusikia anaachana na haya majukumu kwa kuwa kabla ya muda endapo presha kubwa itaibuka kutoka kwa wanachama, hatasita kuachana na uongozi.
Haitakuwa rahisi kwa mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuvumilia endapo watasikia hata wachezaji wanaoamini watawasaidia wanaondoka taratibu.