Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Azory anatukumbusha ya Vatican au Dk Mwakyembe ameteleza?

54924 Pic+azory

Wed, 1 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nimesikitishwa na matamshi ya Dk Harrison Mwakyembe, waziri wa Habari juu ya kupotea kwa Azory Gwanda.

La kusikitisha zaidi ni kwamba matamshi kama hayo yanatolewa na mtu ambaye angekuwa mstari wa mbele kuwatetea na kuwalinda waandishi wa habari lakini akatamka kwamba “sasa suala la Azory limefungwa, kama alikufa au amepotea ni kama wengine wengi waliokufa na kupotea kule Kibiti.”

Sote tunajua na dunia nzima inajua kwamba Azory, alikuwa mwandishi wa habari za uchunguzi, akiliandikia gazeti la Mwananchi, wakati yanamkuta ya kumkuta kulikuwa na hayo mauaji ya Kibiti naye aliandika habari kadhaa juu yake.

Kuna malalamiko mengi kwamba kuna watu wengi wasiokuwa na hatia walikufa kule Kibiti. Kusema tu bila ushahidi ni uchochezi. Azory hakutaka kufanya uchochezi, akaanza kazi yake ya kuwasemea wale wasiokuwa na sauti na kufikisha habari za uhakika kwenye vyombo vya habari na kwenye serikali.

Hakuna mwenye taarifa za Azory, kuwa kwenye kikundi cha ujambazi, ugaidi au kushiriki kwa namna yoyote ile kwenye mauaji. Hivyo matamshi kwamba na yeye atakuwa amekumbwa kwenye mkasa wa Kibiti, bila maelezo ya kina ni kuilazimisha jamii ya kuishi kwenye ukimya na kujenga utamaduni wa ukimya, kitu ambacho si kizuri kwa taifa linalojitangaza kuwa mstari wa mbele katika demokrasia na haki za binadamu.

Waziri Mwakyembe, anataka kutujengea utamaduni wa ukimya kwenye taifa letu. Tunataka tusitake siasa za ukimya ni hatari, iwe leo au vizazi vijavyo. Ina maana Azory kama aliyaona ya kuyaona angekaa kimya, kwa vile hakukaa kimya yamemkuta kama yalivyowakuta wengine wengi kule Kibiti.

Vyombo vya habari ni mhimili mkubwa katika jamii yetu, ukiachia mbali serikali, mahakama na Bunge. Hivyo wahariri wanaoviongoza vyombo hivi ni watu muhimu na wana ushawishi mkubwa katika jamii. Ni muhimu kabisa watu hawa kuwa na sauti ya pamoja ili mhimili huu muhimu uwe na nguvu za kutosha kutetea haki na kusimamia ukweli.

Inashangaza kwamba sauti hii ya pamoja, sauti ya kutetea haki sauti ya kupinga kunyanyaswa na kuonewa haijasikika kupinga kwa nguvu zote matamshi ya Mwakyembe, kwamba Azory, yalimkuta kama yalivyowakuta wengine wengi kule Kibiti.

Tulitegemea kuwaona wahariri wakitumia nguvu zao zote, magazeti yao, mikutano yao na hata maandamano ya amani kupinga matamshi hayo.

Bahati mbaya au nzuri wahariri wengi ni vijana. Na tujuavyo vijana mara nyingi wanakuwa mstari wa mbele kutetea haki na kutaka mabadiliko. Katika hali ya kawaida, bila kuzingatia itikadi yoyote ile kitendo cha kubeza tukio la kupotea kwa Azory, kingepigiwa kelele na wahariri hadi mbingu zikasikia.

Kimya hiki kinashangaza sana. Ukimya unahesabika katika sauti ya pamoja, sauti ya kutetea haki? Au wakati umefika kuamini kwamba wahariri wetu wamefungwa midomo? Au wanapata somo kama lile la Vatican? Au wanaamini kwamba waziri kateleza? Kesho ataomba msamaha au atawajika?



Columnist: mwananchi.co.tz