Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Anna anatakiwa kujengwa kiimani kabla ya msaada wa kisaikolojia

85054 Anna+pic Anna anatakiwa kujengwa kiimani kabla ya msaada wa kisaikolojia

Fri, 22 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wataalamu wa saikolojia wamesema Anna Zambi, aliyepoteza wazazi na wadogo zake watatu katika mafuriko, anahitaji kujengwa kiimani kabla ya kuanza kupata msaada wa kisaikolojia.

Wameshauri viongozi wa dini kuwa karibu na binti huyo, ili ajue kwamba kila jambo linalotokea duniani hupangwa na Mungu.

Wazazi na wadogo zake watatu walisombwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua wakiwa kwenye gari eneo la Handeni wakati wakiwa safarini kwenda shuleni kuungana naye katika mahafali ya kidato cha nne.

Hata hivyo, Anna hakupewa taarifa za msiba huo ili kumuwezesha kufanya mitihani yake ya kumaliza elimu ya sekondari.

Akizungumza na Mwananchi jana, mtaalamu wa saikolojia kutoka Shirika la Msaada wa Kisaikolojia kwa Watoto (REPPSI), Edwick Mapalala alisema zipo hatua tano anazopitia mtu aliyepewa taarifa za huzuni.

Alisema kwa hatua aliyo nayo Anna hivi sasa, anapaswa kupewa msaada wa kiimani, ili wakati wanasaikolojia watakapokuwa wanamjenga iweze kumsaidia.

“Kwa hiyo viongozi wa dini wenye utaalamu wa kuzungumza na watoto, huu ndio wakati wao. Anna anawahitaji zaidi,” alisema Mapalala.

Alisema tukio alilokutana nalo limemuumiza kisaikolojia na limeivunja imani yake.

“Vitu vingi wanavyohangaika navyo watu kwa sasa kumhusu Anna havina msaada kabisa. Yeye haoni faida, wala fedha, mali wala chochote kile zaidi ya kujiuliza maswali mengi kuhusu familia yake,” alisema Mapalala.

Daktari wa Hospitali ya Temeke aliyekuwapo kwenye msiba huo, Fredrick Doya alitaja hatua ya kwanza anayokutana nayo mtu anayepata taarifa za huzuni ni kukataa.

“Anakataa kabisa kwamba haiwezekani hali hii initokee,” alisema Dk Doya.

Alisema hatua ya pili ni kupata hasira kuhusu ile taarifa.

“Akishapata hasira anaanza kubishia taarifa aliyopata kwamba haiwezekani kabisa, hiki nilichosikia sio kweli,” alisema Dk Doya.

Mapalala alitaja hatua nyingine ni kuwa njiapanda, hali ambayo Anna anapitia kwa sasa.

“Akiwa kwenye hatua hii anahitaji kujengwa hasa kiimani ili aingie hatua ya mwisho ya kukubaliana na hali halisi kwamba hivi ndivyo ilivyo,” alisema Mapalala.

Alisema ule utaratibu wa kiafrika wa kutoa heshima za mwisho huwa unasaidia pia watu kukubali tukio,” alisema Mapalala.

Alisema kama ilivyotokea kwa Anna, kuchagua kwenda kwa mama yake mdogo Isabela, jambo hilo linamsaada kisaikolojia kwa sababu aliamua kukaa na mtu anayempenda.

Columnist: mwananchi.co.tz