Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Anatory Amani, mwanasiasa anayeanguka na kusimama

10841 Pic+antony TanzaniaWeb

Wed, 8 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Imewakuta wengi ndani ya CCM walioshinda kura za maoni wakati wa uchaguzi lakini wakaenguliwa na kutangazwa wagombea wengine mbadala.

Baadhi yao hukubaliana na uamuzi huo na kusubiri wakati wao au kupoteza moja kwa moja walichokusudia, lakini kwa wengine huamua kutafuta fursa nyingine kwenye vyama vingine – Huku nako baadhi hushinda na wengine hukwama kabisa.

Ndivyo ilivyokuwa kwa Dk Anatory Amani ambaye baada ya kushinda kura za maoni katika Kata ya Kagondo, Manispaa ya Bukoba katika nafasi ya udiwani mwaka 2015, jina lake lilienguliwa katika vikao vya chama.

Huo ndio ulikuwa mwanzo wa mwanasiasa huyo mkongwe na kada wa CCM aliyepita katika milima na mabonde, kushindwa uvumilivu. Aliamua kuhamia kambi ya upinzani akijiunga na NCCR-Mageuzi iliyokuwa ndani ya Ukawa na kufanikiwa kushinda kiti hicho akimwangusha mgombea wa CCM.

Muungano wa Ukawa ulimrahisishia ushindi kwa kuwa vyama vingine katika umoja huo havikusimamisha wagombea, badala yake vikaunganisha nguvu na mashambulizi ya kumwangusha mgombea wa CCM.

Mgombea huyo hakushuhudia utangazaji wa matokea yaliyompa ushindi kwa kuwa alikuwa anashikiliwa katika Kituo cha Polisi kwa tuhuma za kuwafanyia fujo wasimamizi wa uchaguzi.

Hata hivyo, alitangazwa kuwa diwani akiwa mahabusu.

Huyu ndiye Amani ambaye ametangaza juzi kurejea CCM na kujivua nyadhifa za ujumbe wa vikao vya chama chake alizokuwa amepewa. Amekitelekeza chama kilichomvusha na kumpatia udiwani aliokuwa amenyang’anywa kwa maamuzi ya chama.

Ni meya wa zamani wa Manispaa ya Bukoba katika uongozi uliokuwa na vuta nikuvute nyingine na mgogoro wa muda mrefu uliowagawa madiwani katika pande mbili. Huyu pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Bukoba.

Ametaja sababu za kurejea CCM, kama ambavyo wengi wanasema, kuwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano na kwamba anaona ni eneo sahihi ambalo anaweza kusaidia utekelezaji wa ilani kuliko huko alipokuwa kwenye kambi ya upinzani.

Alivyowang’oa madiwani nane

Meya huyo wa zamani amerejea CCM na kwenda kukaa meza moja na baadhi ya madiwani ambao alipambana nao mahakamani akitaka mahakama iwafutie nafasi zao kwa kushindwa kuhudhuria vikao alivyokuwa anaitisha kwa mujibu wa sheria.

Kabla ya madiwani hao kutimuliwa na mahakama, CCM ilikuwa imeingilia kati na kuwatimua kupitia vikao vya ngazi ya mkoa kwa madai kuwa walikuwa wameendelea kuchochea mgogoro, pamoja na Mwenyekiti wa CCM wakati huo, Jakaya Kikwete kutoa maelekezo.

Ni Dokta Anatory Amani yuleyule aliyeitwa na viongozi wa kitaifa wa chama mjini Dodoma mbele ya Kikwete na kuonywa kuhusu mpambano wake na Kagasheki na kuagizwa watulie.

Madiwani waliotimuliwa ni Yusuph Ngaiza aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba na diwani wa Kashai, Samwel Ruhangisa (Kitendagulo), Robert Katunzi (Hamugembe), Deus Mutakyahwa (Nyanga), Richard Gasper (Miembeni), Mulungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda (Buhembe), aliyekuwa Naibu Meya na Dauda Kalumuna aliyekuwa Diwani wa Ijuganyondo.

Aliyekuwa Katibu wa CCM wa Mkoa wa Kagera, Averin Mushi alisema uamuzi wa kuwatimua madiwani hao ulifikiwa na halmashauri kuu ya CCM ya Mkoa kwa kile alichosema ni kwa ajili ya maslahi ya chama na wananchi wa Bukoba.

Hata hivyo, uamuzi wa halmashauri kuu ya CCM mkoa ulizimwa na vikao vya Halmashauri Kuu ya Taifa ambayo ilibatilisha uamuzi huo na kuwarejeshea uanachama wao.

Meya akaza kamba

Meya huyo hakurudi nyuma alifanikiwa kuwatimua madiwani hao kupitia mlango wa mahakama ambayo ilithibitisha kuwa walikuwa wamepoteza sifa za kuendelea kuwa katika nafasi hizo kwa kutohudhuria vikao halali vilivyoitishwa na meya.

Madhara ya mapambano hilo yaliigharimu CCM ambapo katika uchaguzi mkuu uliopita ni madiwani wawili pekee katika kata zilizokuwa kwenye mgogoro waliofanikiwa kutetea nafasi zao na baadhi zilichukuliwa na upinzani kwa kutumia mtaji wa mgogoro ndani ya CCM na upepo uliovuma vizuri upande wa Ukawa.

Alivunja mfumo wa ‘nyarubanja’

Kuna wakazi asilia wa mji wa Bukoba wanaojuana kwa koo na majina na haikuwa rahisi kwa mgeni yeyote kugombea na kushinda nafasi ya juu ya uongozi wa kuchaguliwa na Dk Amani ndiye alivunja mwiko huo.

Kada huyo wa CCM alianzisha mwanzo mwema wa kuruhusu hata mawazo mapya kutoka nje ya Bukoba na hata upinzani aliokuwa anaupata ilikuwa ni matokeo ya kutaka kulazimisha mabadiliko kwenye mji mdogo wenye watu wanaofahamiana.

Hatua yake ya kushinikiza upimaji wa viwanja kwenye maeneo yaliyokaliwa na koo mbalimbali kwa kurithishana bila kuendelezwa, ulimuibulia tuhuma ya dhuluma ya viwanja vya wananchi wanyonge madai ambayo yametajwa na ripoti ya CAG.

Pamoja na kasoro zilizojitokeza katika harakati zake za kuvunja mfumo huo uliobatizwa ‘nyarubanja’ ulikuwa mwanzo wa kuvutia watu kutoka nje ya Bukoba kununua viwanja vilivyopimwa kwa ajili ya makazi na shughuli za uwekezaji.

Maeneo yenye viwanja vilivyopimwa yalianza kujengwa barabara za vumbi na kuwekewa miundombinu ya umeme na maji, juhudi ambazo zilianzishwa na CCM kupitia viongozi wake yenyewe na kuzihujumu kupitia mlango wa pili.

Kwa Manispaa ya Bukoba Dk Amani alionekana kama’ Bwana Mipango’ ambaye yuko tayari kutumia gharama ili kutekeleza kile anachokiamini na katika baadhi ya kata kama Kitendagulo alitimuliwa kwa mawe na wananchi waliokuwa wanapinga upimaji wa viwanja.

Fundo moyoni

Ndani ya vikao vya Baraza la Madiwani akiwa tu diwani, Dk Amani hakuonyesha uchangamfu wowote kama ilivyokuwa wakati akiwa meya na hata alivyokuwa anaendesha mikutano ya kuwanadi wagombea wa upinzani hakuwa na furaha.

Alionekana ni kama jembe lililoishiwa makali na pengine kama kiongozi aliyekuwa na fundo moyoni hasa baada ya uchaguzi Chief Karumuna kusimikwa kama mrithi wake, huku akitegemewa kumsaidia kusukuma ajenda alizoanzisha.

Ndoa ya Ukawa iliwahakikishia upinzani kuongoza Baraza la Madiwani la Manispaa ya Bukoba huku Chadema ikiwa na madiwani wengi zaidi. Awali ilifikiriwa kuwa Dk Amani kupitia mwavuli wa Ukawa angeweza kurejea kwenye kiti chake cha umeya.

Hata hivyo, haikuwa kama baadhi walivyotegemea badala yake Chadema ilimsimamisha Chief Karumuna diwani wa Kahororo kugombea kiti hicho na baada ya kushika usukani Dk Anatory Amani alionekana kama diwani asiyesomeka.

Atatosha CCM?

Sio jambo la ajabu kuwa Dk Amani amerejea katika chama alichokulia na kukitumikia tangu ujana na safari yake ya kujiunga na upinzani lilikuwa chaguo lake la pili baada ya jina lake kukataliwa lisipeperushe bendera ya chama hicho kwenye kiti cha udiwani.

Kwa vyovyote vile ndoto ya Dk Amani aliyewahi kuingia msukosuko na Uhamiaji katika masuala ya uraia, kisiasa haiwezi kuwa ni kuishia kwenye ngazi ya udiwani na tayari katika mchakato wa kura za maoni mwaka 2015 alijaribu kutikisa kiberiti kwa kushiriki kura za maoni za ubunge wa Bukoba Mjini.

Aliachwa kwa mbali sana na Balozi Kagasheki lakini hiyo haimaanishi kuwa hakubaliki na kurejea kwake CCM anawekwa moja kwa moja kwenye mzani wa kuwa na matarajio makubwa zaidi kisiasa.

Columnist: mwananchi.co.tz