Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Amani endelevu ni msingi wa maendeleo ya uchumi imara

13520 Joseph+alphonce TanzaniaWeb

Fri, 24 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nchi yeyote inahitaji amani na utulivu ili wananchi wake waweze kufanya shughuli za maendeleo. Bila amani na utulivu wafanyabiashara, wafanyakazi, wakulima na wanafunzi hawawezi kujitimiza majukumu yao.

Amani ni miongoni rasilimali muhimu zinazohitajika kufanikisha chochote ambacho familia au jamii inakiwaza kwa lengo la kubadilisha hali iliyopo.

Achana na mchango wa ardhi, mtaji wa fedha taslimu na rasilimaliwatu kwenye utekelezaji wa miradi ya kiuchumi, pasipo na amani haya yote hayana tija.

Pamoja na vitu vingine unavyovihitaji kutekeleza mradi wa ndoto yako kwa manufaa ya jamii inayokuzunguka, unahitaji amani ya kweli.

Utafiti unaonyesha uwapo wa uhusiano kati ya amani na maendeleo katika ujenzi wa taifa bora na lenye uchumi imara. Kwa tafsiri ya kawaida maendeleo ni kupiga hatua kutoka hali dhaifu kwenda bora au ya juu.

Popote pale, maendeleo yanatajwa kuwa na umuhimu wake kwa maisha ya wananchi. Mosi ni kuongeza thamani ya mwanadamu. Hili hufanyika kwa kuheshimu utu na maamuzi yake bila kujali kipato, rangi, chama, kabila au dini.

Ikumbukwe, kila mwandamu ana thamani sawa na mwingine mbele ya sheria za nchi. Bila kujali ushawishi wako kwenye jamii, ni vyema kufahamu suala hili la msingi.

Uhuru wa kuchagua na kujiamria mambo bila kuingiliwa na mtu mwingine ni umuhimu mwingine wa maendeleo. Uhuru wa kukusanyika, kutoa maoni, kuabudu katika dini yoyote, kwenda popote na kujiunga na chama chochote ni mambo ya msingi kw akila mtu.

Kuna uhuru wa kuchaguliwa na kuchagua kwa misingi ya demokrasia. Pamoja na uhuru unaotajwa lazima uendane na misingi ya sheria, kanuni na utaratibu uliowekwa ili kutovunja haki za wengine ama kwa kukusudia au kutokusudia kwani hakuna uhuru usiokuwa na mipaka.

Tatu, kupatikana kwa mahitaji muhimu ya mwanadamu kikiweamo chakula, malazi, mavazi, huduma stahiki za afya, elimu bora na ulinzi na usalama. Dhana ya maendeleo inakamilika pale ambapo mwanadamu anaheshimika, yupo huru na anapata mahitaji muhimu ya kila siku.

Watafiti wa masuala ya uchumi na kijamii wanaeleza kuna uhusiano mdogo kati ya amani na vita. Haitoshi tu kusema palipo na amani hakuna vita na palipo na vita hakuna amani.

Kuna mchambuzi anatoa tafsiri ya amani, pamoja na kutokuwepo vita, anasema usiwepo umasikini, magojwa, ujinga, upendeleo na ukandwamizaji wa haki za wananchi wananchi.

Amani inaelezwa kuwa ni uwapo wa haki sawa katika jamii kunakosimamiwa na Serikali. Pamoja na tafsiri hizo, amani haijakamilika bila kuwapo kwa hali nzuri ya kiuchumi hususan kipato cha uhakika kuanzia ngazi ya familia, jamii na taifa kwa ujumla.

Nitaeleza kwa ufupi aina za amani kwa mujibu wa watafiti mbalimbali duniani. Kuna aina mbili za ammani, mosi ni amani chanya (positive peace) ambayo mara nyingi hupatikana pale ambapo hakuna umasikini, njaa, upendeleo, unyanyasaji, ukiukwaji wa haki, usawa na ubaguzi wa rangi.

Pili ni amani hasi (negative peace) hii hupatikana pale ambapo hakuna mashambulizi kwa raia, migomo, vita na matendo ya ugaidi.

Bila kujali nchi zilizoendelea au zinazoendelea, kila moja inahitaji aina zote mbili za amani ili wananchi wake wawe na maendeleo. Wakati tunaendelea na mapambano dhidi ya umasikini, ujinga na maradhi wakati huo huo tunahitaji kuzuia vita, ugaidi, upendeleo na ubaguzi wa aina yoyote kwa maendeleo ya kweli.

Zipo jitihada kadhaa zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali tangu uhuru hadi sasa kuhakikisha Tanzania linakuwa taifa bora na lenye uchumi imara. Kwa kipindi hicho, Tanzania ina dira kuu tatu za maendeleo hadi sasa.

Kwanza ni kujenga misingi imara ya kisiasa itakayowajumuisha wananchi wote baada ya kupata uhuru huo kutoka kwa wakoloni mwaka 1961.

Baada ya hapo lilikuja Azimio la Arusha mwaka 1967 na baadaye dira ya Taifa 2025. Dira ya Taifa 2025 ina malengo makuu matano ambayo yote yanaelekeza kuwa na Taifa bora na lenye uchumi imara.

Kati ya malengo hayo, lipo la kuwa na uchumi imara ambao ni shindani kwa mataifa mengine vilevile. Hili linaenda sambamba na kuwa na amani, utulivu na umoja wa kitaifa usioruhusu hila za namna yoyote kuleta mpasuko.

Kuelekea uchumi wa kati unaotegemea viwanda, tunahitaji kuwa na amani kuhakikisha maendeleo endelevu na yenye tija kwa watu wote.

Umuhimu wa maendeleo haya utadhihirika zaidi endapo wananchi wengi watanufaika nayo. Maendeleo yenye matabaka yanayoruhusu tofauti kubwa ya kipato kati ya masikini na matajiri mara nyingi hayawi endelevu.

Wakati Serikali inajenga miundombinu tofauti kwa kutumia kodi za wananchi wote, manufaa yake pia yanapaswa kumgusa kila mmoja kwa namna moja au nyingine.

Kufanikisha haya yote, hakuna njia fupi zaidi ya kuhakikisha kunakuwa na amani itakayomruhusu kila mmoja kushiriki kwenye shughuli za maendeleo kulingana na nafasi yake.

Mwandishi ni mtakwimu katika Ofisi ya Rais-Tamisemi.

Columnist: mwananchi.co.tz