Hivi karibuni, kilio kikubwa cha taifa letu kimehamia kwenye ajali mfululizo za magari ya serikali au taasisi za umma. Si kwamba hii ni mara ya kwanza magari ya serikali kupata ajali, la hasha! Tofauti ya wakati huu na huko nyuma ni kwamba, ajali za magari ya serikali za mara hii zimekuwa mfululizo na inaonekana kama vyanzo vya ajali hizo zinafanana.
Ni wazi kwamba, vyanzo vya ajali hizi ni vilevile vyanzo vya ajali za magari mengine; mwendokasi, uchovu wa madereva kutokana na kuendesha magari umbali mrefu, ubovu wa miundombinu ya barabara zetu, uchakavu wa magari na madereva kutozingatia sheria za barabarani.
Tukizama ndani zaidi ya tatizo hili kwa kuzingatia vyanzo vya ajali nilivyovitaja tunagundua kwamba chanzo kimoja kwa sasa hakihusiki sana. Hiki ni cha uchakavu wa magari. Kwa watu ambao wanapishana na magari ya serikali barabarani, watagundua magari mengi kati ya hayo ni mapya na au ni ya kisasa na yenye nguvu na ufanisi mkubwa yawapo barabarani.
Kwa msingi huo tunabakia na hoja nne au vyanzo vinne ambavyo vikitibiwa na serikali tutakuwa na uhakika wa watumishi na viongozi wanaotumia magari hayo kuwa salama hadi mwisho wa safari zao.
Mwendokasi wa kuzimu
Nani hajui kuwa magari ya serikali yanakimbizwa utadhani ndege aina ya JET. Mahali ambapo kuna matuta magari haya yanapaa juu utadhani helikopta, kwenye kona yanapita na spidi ya kilometa 150 kwa saa, kwenye barabara ya kawaida yanatembea hadi kilometa 200 kwa saa. Muda wote yamewasha taa yakiashiria kwamba hakuna mzaha, hakuna kusimama na hakuna mwisho mwema.
Kwa kweli mwendo wa magari ya serikali kwenye barabara zetu ni safari za kuelekea kuzimu. Unapishana na gari ya serikali inakimbia utadhani waliomo wana miadi na Mungu kuwa wao hawawezi kupata ajali au kukosa mwelekeo.
Kwa kifupi, mwendo ambao magari ya serikali yanautumia barabarani haumithiliki na mwendo wenyewe tu ni ajali tosha. Tusipotafuta mbinu ya kudhibiti mwendo huo, watumishi wetu na viongozi wetu wataendelea kupoteza maisha.
Madereva wa magari ya serikali hawapumziki, wamegeuzwa kuwa kompyuta. Siku ina saa 24, mwanadamu anapaswa kutumia saa 8 tu kufanya kazi na labda akizidisha sana atahitaji saa 10 tu kufanya kazi. Kisha anahitaji saa 8 kulala na saa 6 – 8 kufanya masuala yanayochangamsha mwili wake kama vile mazoezi, kujumuika na wenzake kwa masuala mbalimbali n.k.
Dereva wa gari la serikali anaamshwa saa 10 alfajiri ili yeye na kiongozi au mtumishi wa serikali kwenda safari ya kilomita 800. Wanatumia saa 7 kufanya safari hiyo, wanafika mahali huko saa 5 asubuhi. Kiongozi au mtumishi anaingia kwenye majukumu huku dereva akiwa “standby” eneo la nje.
Ikifika saa 8 mchana mtumishi au kiongozi anarudi kwenye gari safari nyingine ya kilomita 1,000 inaanza, safari hii inatumia saa zingine 10, mtumishi au kiongozi analala muda huo wa saa 10 za safari mpya kwa kadri atakavyo, dereva yeye masikini anakalia usukani hadi saa 6 za usiku.
Alfajiri saa 10 dereva anaamshwa kwa majukumu mengine. Ukweli ni kuwa, hakuna ubongo wa binadamu unaoweza kufanya kazi namna hiyo. Tusipokomesha ratiba za namna hii, hasa kwa magari ya serikali kwa kuwa na madereva wawili ambao watakuwa wanapokezana gari, tutaendelea kupambana na vilio vya kuwapoteza ndugu zetu ambao tumewatengeneza kwa gharama kubwa za walipa kodi.
Miundombinu ya Tanzania haikidhi haja ya magari yanayohitaji kwenda spidi 180 kwa saa, barabara zetu nyingi ni zile ambazo magari yanayoenda na kurudi yanakutana, zinahitaji uendeshaji wenye nidhamu ya hali ya juu kwani kosa moja kidogo tu linaweza kusababisha gari kukosa mwelekeo au kugongana na gari jingine. Barabara zetu nyingi zina matuta yasiyotegemewa, kona za mara kwa mara na miteremko inayohitaji utulivu wa uendeshaji. Haijulikani ni sababu ipi inafanya magari ya serikali yanakimbizwa spidi za juu sana kwenye barabara zenye hali niliyoieleza hapo juu.
Kwa kifupi hoja hii inaungana na chanzo cha mwisho cha ajali ambacho nilikitaja, cha kutozingatia sheria za barabarani.
Madereva hawa wa magari ya serikali, ama kwa kutaka wao au kwa kulazimishwa na mabosi wao, hawafuati alama zozote za barabarani, mahali panapozuia gari lisilipite lingine wao hupita hata magari 10 bila kujali chochote.
Mahali ambapo kuna kona kali wao huendesha kwa spidi zilezile. Kwa kweli ukipanda gari ya serikali na mwendo wake, inakuwa kama umechukua tiketi ya kifo. Serikali inalo jukumu la kujenga mkakati shirikishi ili kuliokoa taifa letu na vifo vya viongozi na watumishi wa umma.
Julius Mtatiro ni mchambuzi wa mfuatiliaji wa utendaji wa Serikali barani Afrika; ni mtaalamu mshauri wa miradi, utawala na sera na ni mtafiti na mwanasheria, Simu; +255787536759 Barua Pepe; [email protected])