Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ajali hazitaondolewa nchini kwa haya matambiko wala maombi

Sun, 15 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwaka 1973 timu ya taifa ya Zaire (Sasa DRC) ilifuzu kushiriki fainali za Kombe la Dunia. Zaire ndiyo iliyokuwa nchi ya kwanza kutoka ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara kupata nafasi hiyo. Fainali hizo zilifanyikia Ujerumani Magharibi.

Rais wa Zaire, Mobutu Seseseko akawakusanya wachawi na waganga nguli wa Zaire kutoka maeneo yote ya nchi yake, kisha akawasafirisha wote kwenda Ujerumani Magharibi. Kazi kuu ya waganga na wachawi ilikuwa ni ‘kuwaroga’ wazungu na kufanya kila aina ya matambiko ili kuhakikisha timu ya Zaire inazifunga timu itakazokutana nazo na hatimaye inaleta kombe la dunia Afrika. Mobutu alikuwa na imani kali kwenye masuala ya uchawi na uganga.

Zaire ilipocheza mechi ya kwanza ikafungwa 2-0 na Scotland, mechi ya pili ikafungwa 9-0 na Yugoslavia na mechi ya tatu ikafungwa 3 – 0 na Brazil.

Zaire ya Mobutu, wachawi wake na waganga wake pamoja na uchawi wao na matambiko yao wakafunga virago kurudi Afrika wakiwa na magoli 12 – 0 kwenye mikoba yao.

Imani dhidi ya uhalisia

Uko uwezekano kwamba makala ya aina hii itawagusa baadhi ya watu hasa kwa sababu ya misimamo yao ya kiimani, kwa maana ya imani za kimila na imani za kidini, hao watanisamehe sana.

Mimi pia nina imani za kidini na nina mila za kwetu, lakini siku zote siruhusu mambo hayo mawili yawe na nguvu ya ghafla kuliko utashi niliopewa na Mungu.

Kwa mfano, mchungaji hawezi kuniambia jiue ili uende mbinguni, vivyo hivyo shehe hawezi kuniambia nilambe vidole ili nipate thawabu, padri hawezi kuniambia tumbukia kwenye shimo la maji marefu kisha kwa muujiza utaibuka.

Ndiyo. Hayo hayawezi kutokea kwa sababu pamoja na ukuu wa nguvu za Mungu ambazo mimi naziamini, na pia nguvu za matambiko ya wanadamu kwa wale wanaoziamini, bado utashi wangu ndiye kiongozi wa maisha yangu.

Faida ya utashi ni kuwa unaongozwa na hali halisi zaidi kuliko imani za juu. Mathalan, utashi unamfanya mtu ajue kuwa ukifanya mapenzi hovyo hovyo utapata Ukimwi na utakufa, wakati imani zinaweza kumfanya mtu aamini kuwa anaweza kupata Ukimwi na akaponeshwa kwa njia za kimiujiza. Ni kuamua unataka kuwa upande upi.

Ndiyo maana alipotokea Babu wa Loliondo, watu wengi sana na wengine wakiwa ni viongozi waliongozwa na imani zao kwenda kunywa kikombe cha dawa ili kutibu maradhi yao. Wagonjwa wengi walitolewa hospitalini kwa ajili hiyo, wengi wao wakafa kwa kukosa huduma za kisayansi na kiuhalisia kuliko zile za kiimani.

Mambo haya ninayoyaeleza yanatukumbusha jukumu muhimu la kutengeneza uwiano mzuri kati ya imani zetu na utashi wetu. Mungu hakukosea kutupatia akili na utashi, hakukosea pia alipoweka imani.

Bara la ajabu

Bara la Afrika linaendelea kuweka rekodi mbalimbali za mambo ya ajabu sana. Wakati Waafrika wanaendelea kuanguka kwenye lindi kubwa la umasikini, ongezeko kubwa la watu ambao watafikia bilioni 2.4 mwaka 2050, ukosefu wa usalama ndani ya Afrika, miundombinu mibovu, huduma dhaifu za kijamii na mambo mengine mengi yanayokera, viongozi wa Afrika wanaendelea na tabia ya kukwepa majukumu yao ya msingi ya kuwatoa raia kwenye lindi la matatizo.

Viongozi wanafanya hivyo kwa kuwekeza nguvu kwenye masuala ya imani potofu ambazo haziwezi kushindana na hali halisi.

Tukio la Mbeya

Wiki hii mkoani Mbeya kumefanyika matukio mawili makubwa, kwanza kumekuwa na maombi ya jumla ya kuzuia ajali ambayo yamefanywa na mamlaka za kiserikali za mkoa kwa kushirikiana na viongozi wa dini, halafu kukafanyika tukio la pili ambalo ni kukusanya watu waliotwa wataalamu wa mila ambao walivaa mavazi meusi na vitu mbalimbali kama vile ngozi, manyoya, vibuyu na vingine vingi. Kundi hili la pili likiwa na viongozi mbalimbali lilienda kufanya matambiko kwenye eneo ambalo panatokea ajali nyingi mkoani humo, matambiko hayo yana lengo la kuzuia ajali zisitokee.

Nikitafakari visa hivi vya Mbeya Tanzania na vile vya Zaire ya Mobutu na timu yake, ndipo nahitimisha kuwa Afrika ni bara la kipekee ambalo bado limezama kwenye lindi la ujinga na uhangaikaji. Ni bara ambalo bado linahitaji mabadiliko makubwa ya kifikra yatakayoambatana na kukubali mapungufu, wajibu na majukumu ya serikali za barani humu.

Wajibu vs matambiko na uganga

Ajali za magari ni jambo halisi, siyo imani wala uganga. Ajali hazina uhusiano na uchawi, matambiko, ugagula, utamaduni wala mambo kama hayo. Ajali hazina uhusiano na Ukristo, Uislamu, Ubudha wala imani nyinginezo. Ajali ni tendo halisi linalotokea na linaweza kuzuiwa kwa njia halisi, ndipo baadaye asingiziwe Mungu.

Wajibu wa mwanadamu, serikali, mamlaka, wamiliki wa magari, watumiaji wa njia na barabara unakuja mwanzoni kwanza kabla ya kumkabidhi Mungu na hata labda hao miungu wengine wa mitaani, ambao wanaaminiwa kwenye matambiko.

Wamiliki wa magari wana wajibu wa kuhakikisha magari yao ni mazima muda wote, yamekaguliwa kila wakati ukifika na kila ikihisiwa kunaweza kuwa na tatizo, na wana jukumu la kufuatilia mienendo ya magari yao hata yanapokuwa mbali nao.

Madereva wa magari wanalo jukumu la kufuata sheria zote za usalama barabarani kwa umakini na ukamilifu ikiwa ni pamoja na kuendesha magari kwa tahadhari hata katika maeneo ambayo wana uzoefu nayo. Madereva wanapaswa kujenga nidhamu kubwa na kuhofia kila jambo dogo wanaloliona kwenye gari au barabara maana mambo yanayodhaniwa kuwa madogo hukua haraka ikiwa gari liko kwenye mwendo na huweza kuleta madhara makubwa.

Serikali inao wajibu wa kuhakikisha inajenga miundombinu ya uhakika kwenye maeneo yote hatarishi na yenye viashiria au uwezekano wa kutokea ajali, bila kujali kuwa maeneo hayo kumewahi kutokea ajali au hakukuwahi kutokea ajali.

Jukumu la ujenzi wa miundombinu na teknolojia zote za usalama wa barabara iko kwa serikali.

Vyombo vya ulinzi na usalama na hasa polisi wa usalama barabarani wanapaswa kufanya kazi yao kufa na kupona na kuhakikisha wanachukua hatua stahiki za kiushauri na kisheria kwa wamiliki wa magari, madereva na abiria au watumia barabara wote kila wanapoonyesha vitendo vya kukiuka sheria za usalama barabarani.

Watembea kwa miguu, waendesha baiskeli na watumia barabara wengine wanapaswa kufundishwa njia salama za kutumia barabara, kunapaswa kuwa na kampeni kubwa ya kitaifa ya masuala ya matumizi ya barabara na alama za barabarani na elimu ya hatua za kuchukua kila jambo fulani linapotokea au linapotaka kutokea.

Hii itawasaidia watumiaji wengine wa barabara kuchukua maamuzi sahihi na ya tahadhari kila mara, ambayo yatawaepusha na ajali, wao na watu wengine.

Uhalisia na matambiko

Katika yote hayo niliyotaja hapo juu hakuna mahali ambapo nimetaja waganga, wachawi, makanisa, misikiti, wachungaji, maaskofu, mashehe, wachungaji na wengineo. Tusichanganye maisha halisi na usalama halisi wa watu wetu na taifa letu dhidi ya mambo ya imani ambapo kila mtu anaamini imani yake.

Haiwezekani ajali zinatokea sana mkoa fulani au eneo fulani halafu hatua zetu za kwanza za kuzuia zinakuwa ni kuitisha makongamano ya kidini na sala badala ya kutekeleza kwanza wajibu nilioutaja hapo juu, ambao unapaswa kuratibiwa kisasa ukiihusisha serikali, Jeshi la polisi, wamiliki wa magari, madereva na watumia barabara wote wakiwemo watembea kwa miguu.

Ajali haziwezi kuondolewa kwa maombi na matambiko. Ajali zitaondolewa kwa mikakati yenye uhalisia na inayoonekana inayojengwa na utashi wetu wa kimaamuzi katika kushughulika miundombinu, namna zetu za utumiaji wa barabara, namna ya usimamizi wa sheria zetu, namna ya umiliki na utengenezaji wa magari na namna ya uendeshaji wake.

Ni ujinga mkubwa kuendelea kuamini kuwa ajali ni mapenzi ya Mungu au ni kazi ya shetani. Huu ni ujinga mkubwa kama ule wa Mobutu wa kuamini kuwa Afrika inashindwa kuchukua kombe la dunia kwa sababu haijawaroga wazungu na timu zao. Haiwezekani ujinga wa Mobutu wa mwaka 1973 unarudiwa Tanzania mwaka 2018.

Ni lazima serikali yetu na wananchi wote tusimame na kusema hapana kwa ajali. Tuseme hapana hiyo kwa kurekebisha kasoro za kiuhalisia zinazopelekea ajali zisiishe. Tusikwepe wajibu wetu kwa kujificha nyuma ya maombi na matambiko.

Julius Mtatiro ni mchambuzi wa mfuatiliaji wa utendaji wa serikali barani Afrika; ni mtafiti, mwanasheria, mwanaharakati na ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF. Simu; +255787536759 [email protected])

Columnist: mwananchi.co.tz