Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ahadi za wabunge na akili za wapiga kura

25281 Ahadi+pic TanzaniaWeb

Sun, 4 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Unapotazama maamuzi ya Serikali wakati mwingine inashangaza sana. Ukisikiliza kauli za wanasiasa inashitua mno. Lakini, kubwa kuliko na kinachonyong’onyesha akili, mifupa, mapafu na nyoyo ni mitazamo, fikra, upeo na kila kitu kutoka kwa raia au kwa maana nyingine wapiga kura wenyewe.

Yawezekana kwa aina ya tawala za Kiafrika, Watanzania ndiyo watu pekee ambao ni rahisi kuwaongoza. Yaani kuwaongoza Watanzania ni rahisi kuliko kufanya mazungumzo ya faragha na mkeo. Lakini, ukitembea ndani ya taifa hili unagundua kuwa ni taifa gumu sana kuliongoza na kufikia malengo.

Utawaongoza ndiyo, lakini kuna faida gani kuongoza watu ambao hawakuelewi kiongozi wao unataka nini, na kibaya zaidi wao wenyewe hawajui wanataka nini. Mwelewa anataka umuongoze katika jambo analoliamini. Asiyemuelewa anataka umuongoze tu ili mradi naye kaongozwa.

Niwapo nje ya Dar es Salaam (mikoani) napenda kujichanganya na watu ili kuwasoma fikra na mtazamo wao. Na zaidi kupata taswira halisi ya maisha ya Mtanzania. Ndiko kwenye uhalisia wa kile tunachoambiwa na watawala, wanahabari na mshirika ya umma na binafsi.

Wiki iliyopita nilikuwa katika moja ya mikoa ya katikati ya nchi. Licha ya kutumia wikiendi yangu kwa kukaa maeneo ya watu wenye nafuu ya maisha na elimu vichwani. Lakini picha niliyoondoka nayo nimegundua kuwa tatizo la nchi hii siyo viongozi wala wanasiasa. Inatosha kusema tuna matatizo.

Wamekaa wanamsifia mbunge wao kuwa kawajengea barabara ya kilometa kadhaa. Mtu unajiuliza mbunge gani wa kujenga barabara hata ya kilometa moja jimboni?

Wao wanasifia kwa maana ya kwamba mbunge ndiye aliyejenga barabara. Huku wakimponda mbunge aliyetangulia kabla, kwamba hakuwahi kujenga hata choo cha shule. Kinachotokea ni kwamba wabunge wengi wanabebeshwa mzigo usio wao, kwa sababu ya wao wenyewe kutoa ahadi ya kufanya mambo ambayo siyo jukumu lao.

Wawakilishi wa wananchi

Wabunge wanaingia kwenye kampeni kama mapedeshee kwa kutoa ahadi kibwege bwege tu. Na wananchi nao kwa sababu wapo kwa akili ya kusikia mambo mazuri tu wanaingia mkenge. Wanamchagua. Kwa sababu raia hawapendi kuahidiwa mipango wanataka kuahidiwa vitu.

Kwenye kampeni waambie ukiwa mbunge utawaletea ndege ya kuwapeleka kanisani na misikitini na sokoni. Utachaguliwa kwa kura zote. Lakini ukiwaambia kuwa ukiwa mbunge utashirikiana na wananchi ili kuhakikisha ndege zinanunuliwa. Aiseee utapigiwa kura na mkeo tu kama siyo mume. Mshirikiane tena?

Watanzania wengi tupo hivyo. Tunataka kufanyiwa kila kitu siyo kushirikishwa kufanya kitu. Mgombea bora kwenye masikio ya Watanzania ni yule muongo muongo, anayeahidi kufanya jambo yeye kama yeye na siyo kwa kushirikiana na wananchi wake. Tunapenda sana kudanganywa na tunajivunia hilo.

Wananchi wengi hawajui kabisa kuwa ahadi za wabunge wakati wa uchaguzi huwa zinatekelezwa vipi?

Kwa kutumia pesa zao wenyewe? Ruzuku kutoka ndani ya chama anachotoka mgombea? Au kutokana na bajeti ya Serikali? Wengi hapa huamini kuwa ahadi za mbunge zinatekelezwa kwa pesa ya mfukoni mwake.

Hebu tuwekane sawa hapa, kuwa kazi ya mbunge ni uwakilishi wa wananchi. Kuwakilisha matatizo ya kimaendeleo ya wananchi serikalini ili yaweze kupatiwa ufumbuzi. Mbunge kama mtu binafsi hana uwezo wa kuwaletea wananchi maendeleo endelevu kwa kutumia pesa zake binafsi.

Anaweza kujenga shule kwa watoto wa jimbo lake wakasoma, lakini kamwe hawezi kuinua uchumi wa kila mwananchi kwa juhudi zake binafsi. Ni Serikali inayotakiwa kutekeleza ahadi za mbunge kwa wananchi. Ndio maana kuna wabunge masikini ambao hawawezi kujenga hata choo cha shule, lakini wanachofanya ni kuwakilisha wananchi.

Hili suala ni la msingi sana, na wananchi wa kawaida wanapaswa kufahamu, ili waondoe fikra kwamba maendeleo yanaletwa na mbunge binafsi na si Serikali kupitia mbunge. Ahadi nyingi wanazotoa wakati mwingine ni kwa ajili ya kupata ubunge wenyewe kwa wengi wao. Wanapokosa sera zenye tija wanageuka kama wendawazimu kwa kuahidi hata yasiyowezekana.

Ahadi za wagombea

Mbunge anatoa ahadi kibao kuwa atafanya hili, atafanya lile ili mradi apate ubunge ila kwa hali halisi hakuna atakalofanya kupitia mifuko wake zaidi ya kuomba serikali kuu imfikirie kwenye bajeti yake. Kama Serikali haitakuwa na fungu la ahadi zilizotolewa na mbunge, ina maana kuwa hata hiyo miaka mitano pamoja na jimbo kuwa na rasilimali kibao likakosa maendeleo ya maana.

Kinachohitajika siyo ahadi nyingi, bali ubunifu wa mbunge kwenye miradi ambayo rasilimali zake zinapatikana jimbo kwake, na siyo kusubiri fungu kutoka serikalini ambalo halina uhakika. Kama wabunge hawawezi kutekeleza ahadi wanazotoa kwa wananchi, hilo ni kosa ambalo ni sawa na kughushi hati au taarifa ili kujipatia ajira.

Mfumo uliopo ni kama wabunge wanapiga ramli tu, hakuna mbunge mwenye uhakika wa kujengewa barabara na Serikali zaidi ya utashi wa serikali kuu yenyewe. Kila kitu kinapangwa juu kuhusu wapi kifanyike hiki na wapi kisifanyike hiki. Huu siyo mfumo rafiki wa kutoa ahadi kibwege bwege tu. Utaumia.

Bajeti ingepangwa na mikoa na siyo wizara kama ilivyo sasa, wabunge wangesimamia vizuri pesa zinazotolewa katika mikoa yao, tofauti na sasa ambapo bajeti inapangwa na wizara. Kuna mikoa mingi ambayo haina maji salama ya bomba lakini ina vyanzo vingi vya maji. Ni rahisi kutatua matatizo ya mkoa kuliko wizara.

Uchumi wa mikoa

Kuna mikoa ambayo ina rasilimali nyingi zinazozalisha pato ambalo kama kuna utaratibu unaoeleweka, ungekuwa mtaji mzuri wa kuinua pato la mtu mmoja mmoja kwa kila mkoa. Lakini pia halikuwa kosa kutoweka utaratibu huo maana kufanya hivyo kungeiumiza mikoa ambayo haina rasilimali za kutosha. Waliacha tugawane umasikini.

Hivi sasa kila mkoa hupangiwa bajeti na wizara husika. Hakuna linaloweza kufanyika bila bajeti kutolewa na wizara. Sasa tufike mahali tuwaulize wabunge wetu wanaoahidi kwenye kampeni kutoa hiki na kile kuwa hilo fungu la kufanyia yote hayo watapata wapi? Na siyo wao waahidi kisha raia na mbunge wao wote wategemee huruma ya serikali kuu.

Wakati wa kampeni wabunge badala ya kutoa ahadi nyingi wanatakiwa wawaambie wananchi kuwa, kwa kushirikiana nao, watawezesha kupatikana maendeleo, kwa sababu bajeti ya nchi kama yetu haiwezi kuhudumia kila sekta bila nguvu za wananchi. Lakini siyo masikini asiye na ajira anadanganya masikini wenzake kuwa atawaletea maendeleo kumbe naye anataka ajira ya miaka mitano.

Semeni ukweli kuwa bila ushiriki wa wananchi maendeleo ni ndoto. Wabunge wanaogopa suala la kuwaambia wananchi kuwa watawashirikisha kwa sababu wanajua wananchi watahisi wanataka kuchangishwa hivyo hawatawapa kura zao, kwani kila mtu anajua adha ya michango.

Ni kazi ya mbunge kubuni miradi mbalimbali katika jimbo lake na kutumia fursa na rasilimali zilizopo kuwaletea maendeleo wanajimbo lake, wala sio suala la kuiachia Serikali tu. Wabunge wengi wanaangalia namna watakavyofaidi mema ya nchi kwa faida zao, na si kwa faida ya wapiga kura wao.

Tatizo wabunge wengi sio wawazi kwa sisi wapiga kura. Nimehudhuria mikutano mingi ya kampeni, sijasikia mara nyingi wabunge wakiongelea suala hili la ubunifu wa miradi, zaidi ya kusifia sera za vyama vyao, ambazo hazileti mwanga wa maendeleo yanayoonekana. Ili kutumia rasilimali zetu kwa maendeleo ya majimbo yetu tunahitaji fursa tu kutoka serikalini.

Matokeo yake wananchi ukiwaambia wachangie jengo la shule wanasema hawawezi kufanya hivyo kwa kuwa mbunge aliahidi kutekeleza. Hii ndio sura halisi ya wabunge na wapiga kura walio wengi. Kuwa mbunge sio sera wala kumwaga blah blah jukwaani ila ni kutoa kile ambacho utawafanyia wananchi wako ukishapata kura zao.

Columnist: mwananchi.co.tz