Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Agizo la Rais litekelezwe bila upendeleo

41565 Magufulipic Agizo la Rais litekelezwe bila upendeleo

Thu, 14 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Rais John Magufuli, kiongozi mkuu wa nchi alipiga marufuku mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa na kuruhusu viongozi wa kuchaguliwa tu katika maeneo yao husika.

Rais alitoa agizo hilo mwaka juzi ili katika kipindi chake ajikite zaidi kutimiza ahadi zake kwa maendeleo ya Watanzania wote.

Hata hivyo, agizo hilo lilipigiwa kelele na vyama vya upinzani na wadau wa demokrasia nchini, lakini baadaye walilazimika kuliheshimu.

Mikutano ya hadhara iliyoruhusiwa ni ya wabunge katika majimbo yao ya uchaguzi na viongozi wa kitaifa wasiokuwa na majimbo wamejikuta njiapanda. Ilifika hatua hata mikutano ya ndani ikawa inavunjwa na polisi chini ya agizo hilo hilo.

Kwa kawaida kiongozi wa nchi anaposema jambo linatakiwa kutekelezwa. Inawezekana likawa ni agizo linaloonekana kuwa kinyume cha sheria, lakini kwa busara hutakiwa kutekelezwa na ndiyo maana hata vyombo vya dola vinalazimika kusimamia agizo hilo.

Baada ya agizo hilo baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa waliachana na mikutano ya hadhara na kuhamia katika mikutano ya ndani na wale ambao walijaribu kwenda kinyume na agizo hilo waliingia matatizoni.

Hata hivyo, katika siku za karibuni wameonekana baadhi ya wanasiasa hasa kutoka chama tawala, ambao wameanza kukiuka agizo la Rais na kufanya mikutano hadharani.

Hatua hii imeanza kuzua mjadala ni kwa jinsi gani viongozi hao wameamua kupuuza agizo hilo na hakuna hatua zinazochukuliwa tofauti na inapotokea upande wa pili.

Mfano mdogo tu ni kitendo cha Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kufanya mkutano wa hadhara mkoani Arusha mwishoni mwa wiki.

Ili kuliweka hilo sawa, ni vyema ungetolewa ufafanuzi na pengine ikafahamika kuwa inapozungumziwa mikutano ya ndani inamaanisha nini?

Ingawa kikatiba ni haki ya vyama kushiriki kufanya mikutano na kushiriki katika matukio mbalimbali ya kisiasa, ni vyema agizo linapotolewa liheshimiwe na pande zote, au kama kuna maagizo mengine yatolewe ufafanuzi.

Ni muhimu kuangalia haya mambo kwa umakini kwa kuwa kunaweza kuufanya upande mwingine kudhani haufanyiwi haki na kusababisha mvutano ambao hauna sababu yoyote katika siasa za nchi yetu.

Katika mazingira ya vyama vingi kama haya, jambo la msingi ni kuweka uwanja ulio sawa wa ushindani.

Jambo jingine la kuzingatia ni chama tawala kujenga mazingira ambayo yanamfanya Rais ambaye ndiye aliyetoa agizo hilo kuwa mtegoni kwa sababu yeye ndiye mwenyekiti wa chama.

Ni vyema ikafahamika kuwa kama agizo hilo limekuwa likiheshimiwa kwa miaka yote mitatu, basi liendelee kuheshimiwa hivyo hivyo mpaka wakati wa uchaguzi utakapowadia.

Ingawa ni haki ya vyama vya siasa kufanya mikutano yao kwa mujibu wa sheria, bado agizo hilo linapaswa kuheshimiwa na pande zote mbili; vyama vya upinzani na chama tawala.

Katika mazingira ya sasa ambayo maendeleo ndio suala la msingi zaidi, hakuna sababu ya kusababisha mvutano badala ya kuangalia jambo ambalo litafanya tusonge mbele.

Kama mikutano ya ndani imeruhusiwa, basi itumike kwa vyama vyote bila kuonekana dalili za upande mmoja kudhani unaonewa.

Tunaamini kuwa vyama vyote vya siasa vitatumia vizuri mikutano ya ndani bila kusababisha vurugu zozote.



Columnist: mwananchi.co.tz