Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Agizo la Magufuli kwa maDC lina ujumbe mzito

39642 Pic+magufuli Agizo la Magufuli kwa maDC lina ujumbe mzito

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Jumatano iliyopita Rais John Magufuli aliwaonya wakuu wa wilaya kwa tabia yao ya kuwaweka watu mahabusu ovyo kwa saa 48. Alisema kuna mambo huhitaji maelekezo tu badala ya kutumia hiyo nguvu ya kuwaweka watu ndani.

Mambo mawili niliyapenda baada ya Rais Magufuli kuwaonya hao ma-DC. Mosi ni kwamba anajua kuwa wasaidizi wake wanatumia vibaya nafasi zao za uongozi. Pili, anajua kuwa wameshaonywa mara kadhaa lakini hawajaacha ndiyo maana aliamua na yeye kusema.

Namnukuu Rais Magufuli: “Siyo haki. Viongozi wengi wamezungumza kuhusu hili na mimi narudia. Kama una mamlaka ya kuweka watu ndani, mkuu wa mkoa wako naye akiamua akaweka watu ndani itakuwa ni vurugu.”

Nilitaka kugusa hapo tu kuwa viongozi wengi wameshazungumza. Ni kweli kabisa, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa walishaonya jambo hilo. Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo alishasema, Waziri wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Mkuchika na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu walishakemea tabia hiyo.

Wananchi mbalimbali wameshalalamika, wanasiasa, asasi za kiraia, viongozi wa dini, lakini tabia hiyo imeendelea mpaka Rais alipozungumza. Swali ni je, wataogopa kwa sababu Rais kasema au watakaidi na kuendelea? Na ukaidi huo ni kwa masilahi ya nani?

Ikiwa mpaka Makamu wa Rais alisema na hakusikilizwa mpaka Rais ameamua kusema, hiyo tafsiri yake ni nini? Je, walimkaidi Makamu wa Rais? Au walitaka kumsikia Rais mwenyewe akitoa tamko?

Ujumbe mzito

Ukijiuliza maswali kadhaa kuhusu sakata la wakuu wa wilaya kuwaweka watu mahabusu, unapata mambo matatu ambayo yote yanathibitisha kuwa kuna ombwe la uongozi nchini, yaani Taifa linakabiliwa na ukosefu wa viongozi.

Mosi; wananchi wanalalamika, vilevile viongozi wa dini na asasi za kiraia, lakini mkuu wa wilaya hasikii, anaendelea kufanya uamuzi unaolalamikiwa na wengi. Mtu wa aina hiyo si kiongozi anayetegemewa kuwaongoza watu. Uongozi ni kuongoza, si kuburuza.

Imeelezwa mara nyingi kuwa kiongozi mzuri ni yule msikivu. Rais wa 28 wa Marekani, Woodrow Wilson, alisema: “Sikio la kiongozi lazima lipige kengele kutokana na sauti za watu.”

Kitendo cha wananchi kulalamika lakini wakuu wa wilaya wakaendelea na yanayolalamikiwa, ni wazi hawana sikio la uongozi.

Pili; Viongozi wa juu wanaonya, mkuu wa wilaya anarudia yaleyale ambayo yameonywa. Hadi Makamu wa Rais? Ni dhahiri mkuu wa wilaya ambaye aliweka watu mahabusu baada ya onyo la Makamu wa Rais, huyo si kiongozi, maana ni mtovu wa nidhamu kwa mamlaka za juu yake. Mwanafalsafa wa zamani wa Ugiriki, Aristotle, alipata kusema: “Ambaye hawezi kuwa mfuasi mzuri, hawezi kuwa kiongozi mzuri.” Kwa maana hiyo, kama mkuu wa wilaya anaweza kukaidi maagizo ya mabosi wake, huyo anawezaje kuwaongoza wengine?

Profesa wa uongozi wa umma katika Chuo Kikuu cha Harvard, Marekani, Barbara Kellerman anafundisha kuwa watu wengi hujifunza kuwa viongozi wazuri kwa kuwa wafuasi wazuri. Hekima za Aristotle na Barbara wa Harvard, zinatwambia kuwa baadhi ya wakuu wa wilaya si wafuasi wazuri, maana walimkaidi mpaka Makamu wa Rais, kwa hiyo hawawezi kuwa viongozi wazuri.

Tatu; malalamiko yote yanaonyesha ni kiasi gani wakuu wa wilaya wengi wanavyopenda kuamrisha. Uongozi siyo amri. Mara nyingi amri humaanisha kutojiamini. Anaona haheshimiwi au haogopwi, kwa hiyo anaamrisha ili aogopwe. Mtu asiyejiamini hapaswi kuwa kiongozi.

Katibu Mkuu wa pili wa Umoja wa Mataifa, Dag Hammarskjold katikati ya Karne ya 20 alisema: “Nafasi yako haikupi haki ya kutoa amri. Inaweka shinikizo juu yako juu ya wajibu wa kuishi kwa namna ambayo watu wengine watapokea maagizo yako bila kujisikia wamefedheheshwa.”

Uongozi unataka kiongozi asifedheheshe wengine. Kuweka watu mahabusu ni kuwafedhehesha. Na kama alivyosema Rais Magufuli, mambo mengine yanahitaji mazungumzo na maelekezo lakini amri zinakuwa na nguvu kuliko busara.

Hili lifahamike

Sheria ya Tawala za Mikoa, sura ya 97, ambayo ndiyo imewapa mamlaka wakuu wa mikoa na wilaya kuwaweka watu mahabusu pale wanapoona kosa linafanyika mbele yao, lakini imekuwa ikitumika vibaya, maana ina masharti yake.

Kwanza wanasheria wamekuwa wakiikosoa kwamba inakwenda kinyume na Katiba, pili inafafanuliwa kwamba ilitungwa kipindi ambacho hakukuwa na mtandao mzuri wa jeshi la polisi. Mkuchika amepata kufafanua kuwa mkuu wa wilaya anaweza kumweka mtu mahabusu kwa saa 24 ili kuokoa maisha yake.

Hata hivyo, wakuu wa wilaya huwasweka mahabusu hata watu ambao hupishana nao kauli tu. Wanasiasa wengi wameshaonja joto la jiwe. Wengi wa upinzani lakini pia CCM. Mbunge wa Hanang (CCM), Mary Nagu aliwahi kuwekwa mahabusu na Sara Msafiri alipokuwa mkuu wa wilaya ya Hanang. Kwa sasa Sara ni mkuu wa wilaya ya Kigamboni.

Julai 3, mwaka jana, Rais Magufuli alikutana na viongozi wastaafu na kuomba wamshauri. Majaji wakuu wastaafu, Augustino Ramadhan na Barnabas Samatta walimshauri kuhusu haki na kauli za viongozi zenye kuvunja sheria hasa za wakuu wa wilaya.

Je, wakuu wa wilaya hawakuwasikiliza Samatta na Ramadhan? Mbona karibu miezi sita baadaye Rais ametoa onyo upya? Hizi ni dalili za wazi kwamba kuna tatizo la usikivu wa kiuongozi. Kuna tatizo la uongozi.



Columnist: mwananchi.co.tz