Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Adui wa Chadema, ACT-Wazalendo ni “nongwa zisizoisha”

76630 Siasapic

Sat, 21 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2002, vigogo wakubwa wa kilichokuwa chama tawala – Kenya African National Union (Kanu) waligawanyika. Walimsusa Uhuru Kenyatta aliyepigiwa chapuo kugombea urais na Rais aliyekuwa anamaliza muda wake, Daniel Arap Moi.

Majina makubwa kama Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, George Saitoti, Joseph Kamotho na wengine walimuasi Moi na kuamua kwenda kupambana na Kanu pamoja na Uhuru wake.

Mwanasiasa kijana, William Ruto alisimama bega kwa bega na Uhuru akimuunga mkono kama mgombea urais wa Kanu kuhakikisha mipango ya Moi inatimizwa.

Upande wa pili akina Raila walikwenda kuanzisha muungano wa National Rainbow Coalition (Narc), ikimjumuisha Kibaki wa Liberal Democratic Party (LDP).

Narc walimsimamisha Kibaki kuwa mgombea urais, kwa hiyo alikwenda kuchuana na Uhuru wa Kanu. Matokeo ya mwisho Kibaki alishinda, hivyo kuhitimisha utawala wa Kanu iliyokaa madarakani kwa miaka 39 tangu uhuru wa nchi hiyo.

Hapo ni kuonyesha kuwa Uhuru na Ruto kama vijana, walishikamana kipindi cha mtikisiko wa Kanu kukimbiwa na vigogo. Wakionyesha uaminifu mkubwa kwenye chama pasipo kumwangusha mzee Moi ambaye aliamini nchi ingekuwa salama zaidi kama angeiacha mikononi mwa Uhuru.

Pia Soma

Advertisement
Hata hivyo, mwaka 2003, Ruto alikwenda kujiunga na Raila aliyekuwa ameanzisha chama cha Orange Democratic Movement (ODM), hivyo kumwacha Uhuru peke yake Kanu. Mwaka 2006 Ruto alitangaza angegombea urais kupitia ODM lakini uchaguzi wa chama ulipofanyika alizidiwa kura na Raila.

Uhuru na Ruto waliingia kwenye joto kali la uhasama wa kisiasa kwenye Uchaguzi Mkuu Kenya mwaka 2007. Ruto baada ya kuzidiwa kura na Raila aliamua kumuunga mkono, wakati Uhuru alisimama na Kibaki aliyekuwa anatetea kiti chake cha urais kwa muhula wa pili.

Baada ya matokeo yenye utata kutangazwa yaliyompa ushindi Kibaki dhidi ya Raila aliyeonekana kuongoza kwa idadi ya kura kwa muda mrefu, vurugu kubwa zilitokea. Ruto na Uhuru walitajwa kama vinara wa machafuko hayo.

Uhuru aliongoza mapambano kuulinda ushindi wa Kibaki, wakati Ruto alikuwa mstari wa mbele kushinikiza Kibaki aachie ngazi na Raila aapishwe kuwa Rais wa Kenya. Vuta nikuvute hiyo ilisababisha mapigano na mauaji ya kikabila.

Raila alikuwa akiungwa mkono zaidi na Wajaluo pamoja na Wakalenjin. Raila ni Mjaluo na Ruto ni Mkalenjin. Wakati huo Wakikuyu walimpigania Kibaki, maana Uhuru na Kibaki wote ni Wakikuyu. Hivyo mapambano yakawa kati ya Wakikuyu dhidi ya Wajaluo na Wakalenjin.

Kati ya Januari na Februari 2008, Nairobi ilikuwa kimya, mitaa ikawa haina watu, biashara zilifungwa. Watu zaidi ya 1,000 waliripotiwa kuuawa, huku maelfu zaidi wakitajwa kupotea. Chuki ilikuwa kubwa na hatari ilikuwa ya kiwango cha juu.

Historia hiyo ndiyo ambayo huwaonyesha Uhuru na Ruto kama watu wenye historia za kushangaza, kama marafiki na ndugu kwa maslahi yao katika madaraka, vilevile kama maadui wenye kuwindana kwa sababu ya madaraka.

Baada ya mwafaka kupatikana na utulivu kurejea Aprili 2008 na Raila kukubali kuapishwa kuwa Waziri Mkuu Aprili 17, 2008, Uhuru na Ruto walishika nafasi tofauti kwenye Baraza la Mawaziri. Mwaka 2010, walishtakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), iliyopo The Hague, Uholanzi.

Ni kipindi ambacho Uhuru na Ruto walijipanga na kuondoa tofauti na makovu yote ya nyuma kisha kuunganisha nguvu kushinda kesi, vilevile kushinda urais kwenye Uchaguzi Mkuu 2013.

Mwaka 2012 Uhuru aliondoka Kanu na kujiunga na chama cha The National Alliance (TNA). Mwaka huohuo Ruto naye alijiunga na chama United Republican Party (URP). Baada ya hapo wakaunganisha vyama kupitia umoja wa Jubilee na kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu Kenya 2013. Uhuru akawa Rais, Ruto Naibu Rais.

Kutoka kwenye maisha ya Uhuru na Ruto, unapata darasa kuhusu siasa, uongozi, uhusiano na maisha kwa jumla. Darasa hilo linajenga maarifa katika kulinda na kustawisha uhusiano wa kisiasa, vilevile linafundisha subira na namna wakati gani wa kuamua nini katika maisha ya kisiasa.

Darasa hilo litakuwezesha kutambua na kuzingatia kuwa kwenye siasa hakuna rafiki wa kudumu, ila yapo masilahi ya kudumu.

Muhimu ni kwamba siasa huwa hazitaki “nongwa zisizoisha”. Mnatofautiana mitazamo leo au mnapingana kwa sababu ya jambo fulani, wakati mwingine ukijiri mnakubaliana kwa ajili ya maslahi mengine.

Chadema na ACT

Kumekuwa na jitihada za mitandaoni kuliko vikao vya viongozi wa vyama, kuunganisha nguvu ya Chadema na ACT-Wazalendo kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020.

Mashambulizi hayo yamefuata baada ya Zitto Kabwe kumtembelea Tundu Lissu, mwanasheria mkuu wa Chadema, Brussels, Ubelgiji, anakoendelea kutibiwa. Zitto ‘aliposti’ picha mnato na video akiwa na Lissu, kisha akaandika maneno kuwa ushirika (coalition) wa upinzani ndio dawa ya CCM 2020.

Kwa kauli hiyo, baadhi ya wafuasi wa Chadema, wanamshambulia Zitto kuwa anataka kumchonganisha Lissu na chama chao. Zaidi, wanakumbusha mambo ya nyuma ya Uchaguzi Mkuu 2015. Kwamba ACT haikumuunga mkono mgombea Urais wa Ukawa, pia Zitto alitimuliwa Chadema kwa usaliti.

Hizi ndio “nongwa zisizoisha”. Wanasiasa hutazama wakati ujao na mazingira yake, si kupigana vita ya zamani. Mwaka 2015, mgombea wa Ukawa alikuwa Edward Lowassa, ambaye sasa ni CCM. Iweje Chadema na ACT washutumiane kwa kutoungana kumpeleka Lowassa Ikulu?

Kuungana au kutoungana kwa Chadema na ACT katika uchaguzi ujao, kunategemea mahitaji ya kimazingira. Je, mazingira yanataka wapinzani waungane au kila chama kijitegemee? Sio kubeba nongwa za kale. Ruto na Uhuru wangeziishi, wasingekuwa Rais na Naibu Rais leo. Maana walitaka kuuana baada ya Uchaguzi Mkuu Kenya 2007.

Zitto alitimuliwa Chadema kwa sababu ya waraka ulioandikwa na waliokuwa maswahiba wake, Profesa Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba. Wote hao sasa ni CCM. Maisha ni tofauti kabisa.

Mtangazaji wa Marekani, Dave Ramsey, aliwahi kutoa andiko aliloliita “Maadui Watano wa Ushirikiano”. 1. Kukosekana mawasiliano 2. Kutokuwa na sababu ya pamoja 3. Majungu 4. Kukosa mwafaka wa mifarakano na 5. Kukosa uwiano. Yote yanajionyesha katika hili.

Columnist: mwananchi.co.tz