Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

‘Acheni kuwatishia wake zenu talaka’

28617 TALAKA+PIC TanzaniaWeb

Sun, 25 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Zanzibar. Wanaume wametakiwa kuacha tabia ya kuwatishia talaka wake zao kwani kufanya hivyo kunawapelekea wengi kukosa amani na utulivu kwenye ndoa zao .

Wito huo ulitolewa na mkuu wa idara ya wanawake na watoto Pemba, Mwanaisha Ali Massoud wakati akizungumza na wananchi wa shehia ya Tumbe Magharib mjini hapa juzi.

Alisema kwa hivi sasa kwenye jamii nyingi Zanzibar limekuwa jambo la kawaida baadhi ya wanaume kuwatishia wake zao kuwapa talaka jambo aliloeleza si jema na hata dini inakataza.

“Nafahamu kwamba kwenye ndoa kuna changamoto mbalimbali lakini isiwe sababu ya wanandoa kutoelewana na kutishana kupeana talaka au kuachana,” alisema.

Baadhi ya kina mama wa shehia hiyo walidai kumekuwa na vitendo vingi vya udhalilishaji katika ndoa.

Mmoja wa kina mama hao, Bidia Kombo Ali alisema miongoni mwa sababu zinazopelekea hali hiyo ni matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana ambao wengi wao ndiyo wahusika wa matendo hayo.

“Kwa mfano hivi karibuni mwanangu wa kiume miaka 17 alikamatwa na vijana wanaotumia dawa za kulevya kwa lengo la kutaka kumlawiti, lakini wakati anajihami walimpiga na kumkaba shingo, alikaa siku mbili tu akafariki kwani aliumia sana, ila kesi tulipoifuatilia polisi tuliambiwa tukasuluhishane,” alisema.

Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto, Mwanajuma Majid Abdallah aliwataka wanaume kuacha kuwatelekeza wanawake na watoto, kwani ndio chanzo kikuu cha kufanyiwa udhalilishaji.

Mwanasheria wa wizara hiyo, Shaame Farhan Khamis aliwataka wazazi kuripoti matukio hayo sehemu husika kwani Serikali imerekebisha sheria ambayo pamoja na mambo mengine inawanyima dhamana watuhumiwa wa kesi za ubakaji na ulawiti.



Columnist: mwananchi.co.tz