Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

ATCL isichekelee ujio wa ndege, ijipange

36495 Pic+atcl ATCL isichekelee ujio wa ndege, ijipange

Sun, 13 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni wazi kuwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) linafufuka kwa kasi kubwa. Huku ni kupata uhai kwa taasisi ambayo iliendeshwa vibaya, ikaliwa, ikadhoofika kwa sababu mbalimbali na kufa.

Shirika linafufuka kwa sababu nchi inaye kiongozi mwenye visheni katika masuala ya msingi, unaweza kumsema Rais JPM na kumlaumu kwa masuala kadha wa kadha ndani ya nchi lakini kiukweli huyu ni Rais ambaye hadi anaondoka madarakani taifa letu litakuwa na masuala kadhaa muhimu, makubwa na ya kihistoria ya kujivunia na yatakayochochea maendeleo ya nchi kwa kizizi kijacho.

Ukuaji sekta zingine

Ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Umeme (SGR) ni kichocheo cha kipekee cha uchumi wa nchi masikini kama Tanzania ambayo imekuwa na changamoto za watu kutumia saa nyingi barabarani bila usafiri wa uhakika. Reli hii ikikamilika itasaidia kwenye eneo la ongezeko la kasi ya biashara kati ya jiji kuu la biashara la Dar es Salaam na mikoa yote ya katikati na pembezoni mwa Tanzania hasa Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi, maeneo ambayo yana malighafi nyingi huku yakihitaji bidhaa nyingi za kisasa, hapo hatujazungumzia uwezekano wa kupungua kwa bei za usafiri na usafirishaji hata kama jambo hili litachukua miaka mingi baada ya SGR kuanza kazi.

Mradi wa uzalishaji umeme wa Stiegler’s Gorge ambao utaliwezesha taifa kupata jumla ya megawati 2100 za umeme ni uti wa mgongo wa uchumi wa viwanda. Mradi huu ukikamilika kazi ya Tanesco itakuwa ni kuwekeza kwenye uhuishaji na uimarishaji wa miundombinu ya kusambaza na kutunza umeme, suala la mjadala iwapo nchi ina uwezo wa kiumeme halitakuwepo.

Mradi huu wa umeme utakuwa ni chachu ya kipekee kwa wajasiriamali wadogo na wafanyabiashara wakubwa, utakuwa ni msingi wa kuchochea kilimo cha kisasa hadi vijijini ambako wakulima wanaweza kuvuta maji na kufanya kilimo cha umwagiliaji kuwa cha uhakika.

ATCL inasubiriwa sana

Wakati nchi itakapokuwa na umeme wa uhakika na kwa hiyo uzalishaji wa uhakika, ATCL nayo itakuwa na changamoto ya kubuni mikakati mingi sana itakayokimbizana na kasi ya uzalishaji na mahitaji ya watu kusafiri kwa nauli ambazo zimekaa kistratejia na huduma ambazo zimefaulu viwango vya uridhikaji wa abiria na wasafiri.

Kwa hiyo, katika mabadiliko yanayotokea kwa kasi na ongezeko la idadi ya watu wenye kipato cha kati na masuala mengine kadhaa, ATCL inayo kazi ya ziada ya kufanya ambayo itapekea ukuaji wa sekta zingine kuwa fursa kwa shirika hili muhimu.

Sote tunajua ATCL ilikufa kwa sababu iligeuzwa kuwa shamba la bibi na sote tunajua kuwa ATCL inafufuka kwa sababu tumekataa isiendelee kuwa kichwa cha kujifunzia kunyoa, lakini Rais anafanya hivi kwa sababu anajua kuwa taifa la kizazi kijacho ni muhimu kuliko malalamiko ya sasa.

JPM si mkurugenzi wa ATCL

Rais wa nchi anapofanya juhudi za kufufua taasisi zenye tija ambazo ziliuawa kipindi cha nyuma, wajibu wake unaishia kwenye eneo la kusukuma na kuhamasisha usimamizi mpya na wa kisasa uliojaa tija kwa shirika hilo.

Si kazi ya Rais tena kuanza kuisimamia ATCL, anayo mangapi ya kufanya? Na hata hivyo, JPM hatadumu madarakani. Utafika wakati ataondoka, atakuja Rais mwingine ambaye atapaswa kuwa na msukumo wa kisiasa wa kuipeleka mbele ATCL, lakini Rais huyo mpya hatakuwa na uwezo wa kwenda kuishi ofisi za ATCL ili aiongoze.

Sababu za kiubinafsi ambazo ziliiua ATCL zinafahamika, na walioiua ni sisi wenyewe, wataalamu wetu, menejimenti zetu, tabia zetu na kutojipanga kwetu. Ni aibu ya karne ikiwa ATCL itayumba siku za mbele kwa sababu yoyote ile, ya zamani au mpya.

Nina uhakika, pamoja na kwamba biashara ya usafiri wa anga ni ngumu, taifa letu na wataalamu wetu walau tayari wanao uzoefu wa kutosha wa namna ilivyokufa ATCL ya zamani, na kwa kiasi kikubwa sababu za namna hiyo ndizo huua mashirika mengi ya ndege, zinaepukika na kudhibitika.

Jambo la msingi ni menejimenti ya ATCL kujitoa kufa na kupona kusimamia shirika hili kwa weledi mkubwa na bila kumsubiri Rais Magufuli ambaye ana majukumu mengine mengi ya kitaifa.

Sherehe kiwanjani

Tukishapokea ndege hizi saba ambazo JPM aliahidi kuzinunua na ametekeleza, kujifunga vibwebwe na ngoma na furaha na hamasa ya sherehe kwa upande wa menejimenti viishie uwanjani. Wananchi waendelee kusherehekea matunda ya kodi zao majumbani lakini menejimenti ya ATCL ikajifungie ijipange.

Kuendesha shirika la ndege si jambo lelemama, mashirika mengi yanazo ndege lakini yanajiendesha kwa hasara kubwa, siyo malengo ya Rais kununua ndege ili baadaye ATCL ijiendeshe kwa hasara, na siyo lengo la Watanzania kuona kodi zao zinatumika kununua ndege ambazo zitaendeshwa hovyo na kwa hasara.

ATCL inahitaji ubunifu wa kila namna, kujitolea kwa kila namna, uzalendo wa kila namna na uwajibikaji usiomithilika ili kutufanya tuwe na shirika imara, wataalamu tunao wa kutosha, ndege tunazo za kutosha, abiria wa ndani na nje ya nchi wapo wa kutosha. Tunapaswa kuwa na mikakati ya uhakika ya kuwahamasisha na kuwavutia kwetu, kazi hiyo siyo ya JPM ni ya menejimenti ya ATCL.

Ndiyo maana nimesisitiza, sherehe za mapokezi ya ndege tuachiwe wananchi majumbani, ATCL ikajifungie ituletee matokeo.

Julius Mtatiro ni mchambuzi wa mfuatiliaji wautendaji wa Serikali barani Afrika; ni mtaalamu mshauri wa miradi, utawala na sera na ni mtafiti, mfasiri, na mwanasheria. Simu; 0787536759; [email protected])



Columnist: mwananchi.co.tz