Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

ANTI BETTIE: Ameniambia hatanioa, lakini haachi tabia ya kunionea wivu

69790 Anti+bettie

Mon, 5 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nina mpenzi na ameshaniambia hawezi kunioa, lakini ninashangaa ananionea wivu, nikitoka ananifuatilia, akikuta namba hazielewi kwenye simu yangu ananipiga.

Je, huyu ni mwanaume wa aina gani?

Jiulize wewe ni mwanamke wa aina gani? Unaishi na mwanaume ambaye ameshakuambia hawezi kukuoa na bado unaruhusu akuonee wivu, unakuwa umelenga nini?

Mwanamke unatakiwa uheshimu utu wako, unakubali vipi kuishi na mwanaume asiyekuwa na malengo na wewe, anakuonea wivu kwa sababu anakuona ni wa gharama nafuu na unaweza kumuacha yeye ukaenda kwa mwingine.

Yaani huo wivu ni wa kuhofia udhaifu wa uelewa wako, kama umekubali kuwa na yeye aliyekuambia kabisa hatakuoa, kuna uwezekano mkubwa kumkubali yeyote awaye.

Zinduka usingizini , jijali, jiheshimu, linda utu wako, mwanamke ni wa thamani siku zote.

Pia Soma

Tukikorofishana kidogo ananifukuza

Mume wangu ni kama hanitaki, kila tunapotofautiana kidogo ananifukuza, kisha anakuja nyumbani kuniomba msamaha, ananichukua kiasi nimechoka.

Je, ananipenda kweli?

Usikubali hiyo hali iendelee. Baadhi ya wanaume wakiwa na mchepuko mpya au wanapotaka kukutana na wa zamani kwa kutumia siku moja au mbili hufanya visa ili watimize azma hiyo.

Sisemi huyo wako anataka kufanya hivyo, lakini nina wasiwasi na tabia hiyo ya kukufukuza kisha kuja kukuchukua baada ya muda. Kataa mnapokorofishana akikufukuza mwambie akurudishe nyumbani kwenu ili akitaka kukuchukua kikaliwe kikao rasmi cha familia na ueleze kukerwa na tabia yake ya kukufukuza, kama familia mfikie makubaliano ya kuacha tabia hiyo ya unyanyasaji na kukushushia hadhi. Muhimu na wewe jishushe unapomuona anakuja juu, inawezekana huwa unampandisha hasira mkipishana, unataka kuwa juu, huyo ni mumeo kuna namna ya kuzungumza naye, kujibizana naye.

Ninaishi naye kwa sababu alinisomesha

Nimeolewa hivi karibuni na mwanaume ambaye kiukweli simpendi, nimelazimika kufunga naye ndoa kwa sababu tu ndiye aliyenisomesha. Akiniomba unyumba ananiudhi kwa sababu hapo ndiyo ananikera zaidi.

Nifanyeje?

Hivi alivyokuwa anakusomesha mlikubaliana nini, kama ulikuwa unajibebisha ili akulipie ada bila kuweka wazi kuwa humpendi, pambana na hali yako.

Naamini angekusomesha pasi na kumuaminisha kuwa unampenda, sidhani kama angekung’ang’ania kukuoa.Kama ulijilazimisha kumpenda ili akusomeshe, tumia mbinu zile zile kujilazimisha kumpenda ili aendelee kuwa mumeo kwa sababu utakuwa umemdhulumu, umemuaminisha unampenda kumbe ulikuwa unapenda alichokuwa anakitoa na si yeye. Pole sana kwa kutokuwa mwaminifu hata kwa nafsi yako, chukua hatua kukabiliana na hali hiyo. Ukiamua kumpenda mtapendana tu hakuna namna.

Columnist: mwananchi.co.tz