Habari. Nina mpenzi anaweza kukaa hadi siku tatu hajakutumia ujumbe wala kukupigia hadi umtafute.
Hali hiyo haitokei mara moja wala mbili ni kawaida yake tangu nianze mahusiano naye.
Hujasema kama unataka kufunga naye ndoa, umesema mpenzi sasa sijui unapita au unataka kuweka kambi ndiyo maana ninapata ukakasi wa aina ya jibu.
Ila kwa akili ya kawaida mwanamke kama anakupenda hawezi kupitisha siku hajakutafuta, kama anakaa hadi siku tatu kuna shida mahali. Kumbuka kuna baadhi ya wanawake wanapenda sana kubembelezwa, sasa kama hajakutafuta wewe unasubiri nini hadi zinapita siku tatu? Unaonaje ukaanzisha utaratibu wa kumtafuta yeye?
Hii itapendeza, mzoeshe kwa kufanya hivyo mara nyingi, akishazoea atakuwa teja wa kutafuta na siku ukikaa kimya haitafika saa mbili asubuhi atakupigia kutaka kujua kulikoni leo kimya. Pia inawezekana hakutafuti kwa sababu haelewi upo naye kwa ajili gani, yaani amekuona hueleweki unaelekea kuwa mpenzi sugu usiyekuwa na wazo hata chembe la kumuoa muwe mwili mmoja.
Nina imani akikuelewa unataka nini kwake mbali na mwili wake tu, atakutafuta kila mara ili mtu mwingine asizibe nafasi yake.
Kuna jambo lingine hujaliweka wazi pia unaweza kulalamika hajakutafuta kumbe hata vocha humuwekei, jipambanue kiume kama hutimizi majukumu usidai haki.
Mwisho na muhimu muulize kwa nini anakuwa na tabia hiyo ili ujue chanzo cha tabia hiyo na jinsi ya kuimaliza.
Shikamoo Anti. Nina miaka 16, sipendi kukutana kimwili, mpenzi wangu ananisisitiza tufanye mara kwa mara akidai kuwa ni afya.
Je, ni kweli?
Wewe mtoto huna haya kuniuliza swali kama hilo katika umri uliokuwa nao. Unajua kisheria hupaswi kuzungumzia mapenzi kwa mtindo huu, kwa sababu kisheria unatambulika bado mtoto hadi utakapofikisha miaka 18. Nafasi yako ya kuzungumzia mapenzi ni katika elimu ya uzazi salama na kujikinga na magonjwa ya kuambukiza ikiwamo Ukimwi na ni kwa makundi ya vijana tofauti na hapo utakuwa huna adabu.
Huyo mwanaume anatumia uchanga wako kukuhadaa ili akutumie, hata kama ni afya ni mumeo huyo hadi akuambie muwe mnafanya mara kwa mara?
Bahati yako nimeamka vizuri, tofauti na hapo sikuwa na sababu ya kukujibu kwani hatuwezi kuelewana, umri wako hauendani na unachotaka kukijua. Siku nyingine jifunze kuheshimu watu wakubwa na subiri muda wako ufike hayo mambo yapo utayakuta.
na utayachoka.