Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

ACT-Wazalendo wana haki kuilaumu Chadema maridhiano na Serikali

90238 Chadema+pic ACT-Wazalendo wana haki kuilaumu Chadema maridhiano na Serikali

Mon, 30 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ili kuhakikisha naeleweka vizuri, naomba kwanza nifafanue maneno mawili – haki na usahihi. Unaweza kuwa na haki ya kuzungumza lakini hapohapo ikawa si sahihi kusema.

Mtoto anayo haki ya kuwalaumu wazazi wake kwa kutompeleka shule yenye mazingira na vifaa bora zaidi vya kusomea. Hapohapo anaweza akawa hayupo sahihi, ikiwa wazazi hawana na uwezo huo, bali wanajikuna wanapofikia.

Mfanyakazi anaweza kuwa na haki ya kudai ongezeko la masilahi lakini kutokana na mazingira ya kiuchumi ya mwajiri, ikawa si sahihi kudai hiyo nyongeza.

Chadema ni chama kikuu cha upinzani. Chenyewe ndicho kina sauti kubwa kuliko vyama vingine vyote. Kwa hivyo, agenda ya Chadema dhidi ya CCM au Serikali, huwa na nguvu kuliko ya vyama vingine.

Kwa muktadha huo, vyama vya upinzani vikiwa na agenda yenye kusimamiwa au kuungwa mkono na Chadema, nguvu yake inakuwa kubwa zaidi. Hivyo, wakati wowote Chadema haitakiwi kusahau nafasi yao kwenye upinzani wa nchi.

Linapokuja suala la kuunganisha nguvu za upinzani, kama Chadema wanakuwapo kwenye huo muungano, bila shaka ndio wataongoza. Haitarajiwi Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe kuongoza umoja wa wapinzani, mbele ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Hii ni kwa sababu Chadema wana msuli mkubwa wa wabunge, madiwani na hata wanachama. Chadema wanatakiwa kulizingatia hilo. Si kwa kiburi na kuona fahari, bali kwa wajibu, wakitambua dhima ambayo wamebeba kwa nchi kama chama kikuu mbadala.

Mwisho kila chama kina sera, agenda, falsafa na vipaumbele vyake. Hivyo, hakuna chama ambacho kinaweza kusema kinawadai Chadema kwa mambo kadha wa kadha. Na hapo ndipo linapokuja suala la haki na usahihi.

Lipo eneo vyama vya upinzani vyenye nguvu ndogo vinaweza kuwa na haki ya kuwalaumu Chadema, ingawa lawama zao zinaweza kuwa si sahihi. Nitaeleza!

Kama sarafu ilivyo na pande mbili, vivyo hivyo chama chochote cha siasa hukaa upande mmoja wa sarafu. Chukulia sarafu ya Sh100 kama mfano. Upande mmoja kuna kichwa cha Mwalimu Julius Nyerere na wa pili ni swala.

Tuamue kuwa upande wa Nyerere ndio kwenye dola na swala ni kiwakilishi cha upinzani. Hivyo, chama cha siasa huwa upande mmoja wa sarafu. Ama kwenye dola au upinzani.

CCM wapo upande wa dola. Ndio wanaongoza Serikali. Chadema, ACT, CUF, NCCR-Mageuzi, TLP, UDP, UPDP na vingine, wao wanaunda upinzani.

Kila chama katika upande wa sarafu ambao kipo, huwa na shabaha mbili za kimasilahi. Ya kwanza ni kulinda masilahi yake kama chama, pili ni kupigania au kutetea masilahi ya upande wa sarafu ambao kipo.

Tuizungumzie CCM; wana malengo ya kupigania masilahi yao kama chama, kuendelea kushika dola, kupata wabunge wengi ili kupata ruzuku zaidi na kupitisha agenda zao kwa nchi. Shabaha ya pili ni kupigania na kutetea upande ambao wao wapo, yaani utawala.

Tuiweke katika lugha rahisi zaidi; CCM wana wajibu wa kupigania chama chao, vilevile utawala. Kwa mantiki hiyo, hakuna namna unaweza kushambulia utawala pasipo kuigusa CCM.

Chadema kama walivyo ACT na vyama vingine vya upinzani, jukumu namba moja ni kupigania masilahi ya chama. Kuhakikisha wanahamia upande wa pili wa sarafu ili waongoze dola; vilevile kuongeza wabunge na kura za ubunge ili wapate ruzuku nyingi na kupitisha agenda au kukwamisha.

Wajibu mwingine ni kutetea au kupigania upande waliopo, yaani upinzani.

Sasa basi, ACT, Chadema, CUF, NCCR na vyama vingine vya upinzani, katika eneo la kwanza huchuana. Kila kimoja lengo mama ni kushika hatamu, kuwa na nguvu kubwa ya uwakilishi ndani ya Bunge, mabaraza ya madiwani na Serikali za Mitaa.

Katika eneo hilo, Chadema, ACT, CUF, NCCR na vyama vyote vya upinzani ni mahasimu. Hakuna wakati wowote ule Chaumma wanaweza kutamani NLD wapate, wao wakose. Masilahi ya chama kwanza. Ni kupitia kipengele hiki, ACT wakiwalaumu Chadema, litakuja jibu kwamba “mna chama chenu, nasi ni chetu, tusiingiliane”.

Eneo la pili ni ulinzi na utetezi wa upande wa sarafu. Chadema, ACT, CUF, NCCR na vyama vingine vyote, wapo upande wa upinzani. Hivyo, baada ya kupigania masilahi ya chama, lazima kuyavujia jasho masilahi ya upinzani.

Kama kuna haki ya upinzani inakuwa imenyimwa, waathirika ni vyama vyote upinzani. Mathalan, mazingira ya ufanyaji siasa kwa Tanzania hivi sasa, yanaathiri vyama vyote vya upinzani.

Ni eneo hili Chadema wanaweza kuchukia CUF wakiwa na migogoro au ACT kuwanyooshea kidole NCCR, maana hapo yanaangaliwa masilahi ya upande wa sarafu ambao vyama hivyo vyote vipo.

Kwa mantiki hiyo, ACT wana haki ya kuwalaumu Chadema au chama kingine cha upinzani, kama wanaona vitendo au matamshi yao, yanadidimiza masilahi ya upande wao wa sarafu.

Chadema walikwenda kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Desemba 9, mwaka huu katika maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika. Hoja iliyobebwa na Chadema ni maridhiano.

ACT walikosoa hatua hiyo kwamba haukuwa umepita hata mwezi, tangu vyama vyote vya upinzani vilie kuchezewa rafu na CCM kwa kutumia rungu la dola, katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019.

Ilikuwa imani ya ACT kuwa vyama vyote vya upinzani vilipaswa kuonyesha hasira yao dhidi ya CCM na dola kwa kila kilichotokea.

Mbunge wa Kawe na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee alisema kuwa ACT waliingilia mambo yao kama vile wanawadai.

Nakumbusha; katika suala la utetezi wa upande wa sarafu ya upinzani, ACT kama wanaona Chadema wanadidimiza masilahi ya upinzani, wanayo haki ya kulaumu.

Hata Chadema wakiona ACT au chama kingine cha upinzani kinacheza mchezo wa kuibeba CCM, wanayo haki ya kukilaumu. Ni kwa sababu ni chama mwenza katika upinzani.

Hivyo, ACT wanaweza kuwa na haki, lakini swali ni kuhusu usahihi. Je, Chadema hawakuwa na hoja ya msingi kujaribu kutengeneza daraja la maridhiano na Rais John Magufuli?

Na je, Chadema hawakuwa na masilahi yao kama chama ambayo waliyasimamia? Maswali hayo ndiyo yanajenga mantiki kuwa ACT hawakuwa sahihi, ingawa haki walikuwa nayo.

CUF na Ada Tadea walikuwapo Kirumba, sasa mbona Chadema pekee ndio walaumiwe? Jibu lake ni hili; Katika mkataba wa Munich mwaka 1938, Uingereza ililaumiwa zaidi kwamba ilimwendekeza mno Adolf Hitler.

Hata hivyo, Italia na Ufaransa pia zilisaini kumwacha Hitler ajitanue Ulaya ili kuepukana na vita, kukwepa yasijirudie ya Vita ya Kwanza ya Dunia. Lawama hazikuwa nyingi kwa Italia na Ufaransa.

Ni kwa sababu Uingereza ni taifa kinara. Msimamo wake ulionekana una athari kubwa. Chadema ni kinara. Misimamo yake ina athari kubwa. Wapinzani wanaitazama kama turufu ya uimara wa upinzani. Chadema wakilegalega, upinzani lazima udhoofike.

Columnist: mwananchi.co.tz