Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

ACT-Wazalendo, CUF, Maalim Seif wamepata au wamepatikana?

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

“Wakati ni huu, wakati ni sasa. Shusha tanga, pandisha tanga safari iendelee.” Ni tangazo la Maalim Seif Sharif Hamad kwa wanachama na wafuasi wake akiwaamuru washushe bendera za CUF na wapandishe za ACT-Wazalendo, chama alichohamia.

Uamuzi huo wa Maalim Seif aliobadili historia ya miaka 27 ndani ya CUF ulitokana na kushindwa kesi ya kulalamikia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kama mwenyekiti wa chama hicho.

Lipumba alijizulu uenyekiti wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 na mwaka mmoja baadaye akatengua uamuzi wake na kurudia nafasi hiyo.

Hatua hiyo ilipingwa na Seif na timu yake na wote wamehamia ACT-Wazalendo.

Kufuatia hatua hiyo, ACT imebadilika ghafla na kupata mafuriko ya wageni, hasa Zanzibar ambako haikuwa na wafuasi wengi.

Pamoja na hayo, suala muhimu linabaki je nani amenufaika na nani amepoteza nini katika tukio hilo zima?

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kwa hali ilipokuwa imefikia ilikuwa ni lazima Maalim aondoke CUF kwa kuwa mazingira yalikuwa hayaruhusu tena.

Wanasema kwa kuhamia ACT, Maalim amekinufaisha zaidi chama hicho huku akiacha maswali kuhusu wabunge 28 wanaomuunga mkono kwa kuwa mpaka sasa hawajatoa tamko lolote.

Waziri wa zamani Njelu Kasaka anasema uamuzi wa Maalim Seif una faida kwa pande zote; kwaza utamnufaisha yeye kuendelea kubakia katika medali za siasa nchini.

Kwa mujibu wa Kasaka, migogoro ndani ya CUF ilikuwa na lengo la kummaliza Maalim Seif kisiasa kwa kutumia dola, hivyo kwa vyovyote vile angeendelea kung’ang’ania kuwa ndani ya chama hicho mwisho wake ungekuwa mbaya.

“Ni uamuzi sahihi, unamwezesha aendelee kuwa hai katika medani za siasa kwa muda mrefu na waliokuwa wamepangia vinginevyo watakwama.”

Vilevile Kasaka anaongeza kuwa kujiunga kwa Seif ACT kutakiimarisha chama hicho hasa katika safu za uongozi.

“Maalim Seif ni mwanasiasa nguli, ana uzoefu wa kutosha na ushawishi wa hali ya juu, hivyo ACT hawawezi kumuacha katika safu yao uongozi. ACT pia itegemee kunyanyuka ghafla katika idadi ya wafuasi kwa kiwango kikubwa ambao haikuwa nao,” anasisitiza.

Anasema jambo lingine ni chama hicho kupata taswira ya kitaifa kama sheria ya vyama vya siasa inavyosisitiza kuwa na wanachama wapande zote.

“Sasa Maalim Seif amekipatia ACT taswira halisi ya kuwa chama cha kitaifa, sote tumeshuhudia jinsi kilivyosomba wanachama kutoka visiwani Zanzibar.”

Hata hivyo, Kasaka anasema kuna suala la ruzuku ambalo linategemea uamuzi wa Serikali kwa kuwa wabunge wanaomuunga mkono Maalim Seif ni wengi.

Kasaka anatoa mfano wa jinsi ya waliokuwa wabunge wa CUF walipofukuzwa kwa kugomea Bunge Serikali aliamua kutotangaza uchaguzi mdogo ikitoa sababu ya kupunguza gharama badala yake walibadili vifungu vya sheria.

“Kwa ujumla kuhama kwa Maalim kumeongeza nguvu kwa vyama vya upinzani kuendelea katika mapambano dhidi ya demokrasia. Msimamo wangu ni kuwa wasikubali kurudi katika mfumo wa chama kimoja,” anasisitiza Kasaka.

Kinyume na maoni ya Kasaka, Mkurugenzi wa habari wa CUF, Abdul Kambaya anasema kuondoka kwa Maalim Seif ni haki yake na hakuna madhara yoyote kwa chama hicho kwa kuwa.

Vilevile Kambaya anasema haoni kama uamuzi huo wa Maalim Seif utamjenga, badala yake utambomoa na kumuondoa katika medali za siasa wa muda mfupi.

“Tatizo ninaloliona wapinzani wanawajenga watu badala ya kutengeneza mfumo. Mifano ipo wazi yuko wapi sasa Augustino Mrema ambaye aliondoka kwa mbwembwe NCCR-Mageuzi na kuhamia TLP lakini kilichomtokea sasa kila mmoja anaona,” anasema.

Anasema Mrema hakwenda kujenga chama badala yake alijienga mwenyewe kama inavyotoka kwa Maalim.

“ACT wasishangalie kwani Maalim hajapeleka chama Pemba badala yake wamempokea yeye mwenyewe na wanathibitisha hili kwa kusema kwamba ulipo tupo. Watambue kilichompata ‘kibeku na ungo’ pia kitamkuta kwa kuwa wanaendelea kumtengeneza Maalim badala ya kutengeneza mifumo imara,” Anasema.

Lakini maoni ya Kambaya yanapingana na wachambuzi wengine, kama Mkazi wa Tabata, Karim Hosein anayesema kitendo cha Maalim kujiunga na ACT kinawanufaisha zaidi chama hicho kwakuwa kimepata mtu anayejua siasa, mzoefu na anayekubalika.

“Uamuzi wa Maalim utawezesha ACT kuvuna wabunge na madiwani wengi katika uchaguzi wa 2020 lakini si kwa nafasi ya urais,” anasema.

Maoni hayo hayatofautiani sana na ya Maria Kitosi, mkazi wa Temeke, ambaye anaona kuwa ACT ilishapoteza mvuto na imani kwa wananchi baada ya viongozi wake wakuu kuteuliwa na Rais katika nafasi mbalimbali lakini sasa kimelamba dume.



Columnist: mwananchi.co.tz