Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

Yusuf Manji; Kielelezo cha “Malaika waliogeuzwa shetani”

Manji.jpeg Yusuf Manji.

Wed, 3 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Februari 8, 2017, ilikuwa Jumatano. Paul Makonda, wakati huo akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alitaja orodha ya aliowatuhumu kuwa vigogo wa biashara ya dawa za kulevya Tanzania.

Ilikuwa kutaja majina zigzaga. Taifa likazizima. Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima ndani. Halafu, Uchaguzi Mkuu 2020, Gwajima alipitishwa na CCM kugombea ubunge Kawe. Makonda, mtaja majina ya wauza unga, alienguliwa na CCM Kigamboni. Gwajima, mtuhumiwa wa dawa za kulevya ni mbunge leo.

Waruke wengine, kisha mlete Yusuf Mehbub Manji, tycoon wa Quality Group. “Niliowataja Ijumaa waripoti central,” Makonda alitoa amri. Kama mzaha, huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mwisho wa bilionea Manji. Kijana aliyepata kuwa na “miguvu” mingi Afrika Mashariki. Miguvu ya pesa.

Alipofika central Manji hakutoka. Yakaanza maisha ya mahabusu. Safari ya kwa mkemia mkuu kupimwa mkojo. Ooh, majibu ni chanya. Ukafuata mchuano wa fedha na mamlaka. Bonge la mechi. Sijui nani alishinda!

Vuta nikuvute mahakamani; madaktari wakatoa uthibitisho kuwa ile chanya ya mkonjo wa Manji wala si mihadarati, bali dawa mfululizo ambazo bilionea huyo alikuwa akitumia kutokana na maradhi aliyokuwa nayo. Fedha ni mfalme wa kila rasilimali. Ikiwemo rasilimali watu.

Mawakili wa nchi hadi nchi nyuma ya Manji dhidi ya wale wa Serikali. Halafu, mahabusu akawa hakai, muda mwingi ripoti za madaktari zilielekeza apewe uangalizi hospitali. Akapelekwa Aga Khan Hospital, Dar es Salaam. Wodi ya kitajiri. Ukiisogelea muda wote inanukia moshi wa sigara. Bingwa alikuwa zake ndani anachoma, hakuwa na wasi!

Ikapenyezwa kuwa hata polisi waliomlinda Manji hospitalini sababu alikuwa mahabusu, nao walineemeka. Posho Sh150,000 kila siku. Kila ofisa wa polisi alitamani kupangiwa zamu ya kumlinda mahabusu Manji, alipokuwa “akipatiwa matibabu” Aga Khan. Wenye mamlaka walitaka ateseke. Fedha ikatumika kugeuza mchezo.

Ikanyunyizwa na ikadhihirika, Makonda alikuwa rimoti tu. Mwenye rimoti alikuwa Mkuu wa Nchi, Jibaba Dk John Pombe Magufuli. “Ni vita ya kisasi”, ndivyo ilinong’onwa. Eti, enzi hizo Magufuli akiwa Waziri, alimkabili Manji, ambaye alimjibu: “Siongei na mbwa, naongea na mwenye mbwa.”

Wakati huo, Rais madarakani alikuwa Jakaya Kikwete. Ndiye alikuwa mwenye mbwa siyo? Novemba 5, 2015, aliyeambiwa “siongei na mbwa”, akageuka mwenye mbwa. Akaanza kutuma “mbwa wake” wamng’ate Manji. Hawakumbakisha salama.

Kesi mfululizo za uhujumu uchumi, faini za mabilioni ya fedha kwa ukwepaji kodi, malimbikizo ya kodi, kumiliki hati za kusafiri za nchi zaidi ya moja, halafu akakamatwa kwa kukutwa na sare za jeshi. Eti, alishinda zabuni ya kusambaza sare za Jeshi la Wananchi, kisha akakamatwa kwa kosa la kukutwa na sare za jeshi!

Manji wa sopsop, akageuka Manji madevu. Maisha ya mahabusu hakuzoea. Mtoto wa kitajiri, akaanzisha safari ya utajiri wake binafsi akiwa na umri wa miaka 20, akageuka bilionea mkubwa. Maisha nyuma ya nondo kwenye jela ya Keko, ilikuwa kumwonjesha jehanamu kabla ya mauti.

Haijulikani alikubaliana nini na wenye mamlaka. Ghafla, baada ya msoto mrefu, taarifa ya Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma (DPP), ikaeleza nia ya kuendelea na mashitaka dhidi ya Manji haikuwepo tena. Akaachiwa. Huyooo, akasafiri kwenda Marekani. Biashara zake akahamisha.

Kabla ya zama za mwenye visasi, ungefika jengo la Quality Plaza, Nyerere Road, ofisi zilikuwa nadhifu. Yale mazuria sakafuni na sanaa kubwa iliyotumika kusanifu mwonekano wa jengo kwa ndani, ungejua kuwa pesa nyingi ilikuwepo ndani yake. Quality Plaza siku hizi limekuwa jengo la PSSSF.

Namkumbuka Manji kwenye nyakati zake za heri. Alimshusha Raila Odinga kutoka Kenya, kuzindua Quality Centre Mall. Ilikuwa sehemu ambayo ungepata kila kitu. Siku hizi Quality Centre limebaki kuwa jengo la kumbukumbu za kihistoria.

Zama kabla ya mwenye visasi, ungemwona Manji ziarani na Rais Kikwete. Alikuwa alama ya sekta binafsi Tanzania. Manji alipata kuwa fahari ya nchi katika uwekezaji, hasa barani Afrika.

Magufuli, kiongozi aliyehisi watu wanamdharau au walimdharau alipokuwa waziri, hata hotuba zake ziliashiria kuwa kifua chake kilibeba visasi. “Wale waliokuwa wanaishi kama malaika, wataishi kama Shetani,” alitamka waziwazi Rais Magufuli.

Yaliyompata Manji, ndiyo tafsiri ya wengi kuwa alikuwa akiishi kama malaika kabla, akapewa msoto uliomfanya aishi mithili ya Shetani. Manji, maisha yake yalivyobadilika, ni kielelezo cha utawala wa Magufuli, jinsi alivyobomoa jumuiya ya kibiashara na kuwaning’iniza wengi “msalabani”.

Kesi nyingi za uhujumu uchumi kwa wafanyabishara, walipoambiwa watengeneze mwafaka nje ya mahakama (plea deal), fedha walizolipa, kumbe zikapelekwa kufichwa China. Dhuluma kwa wafanyabishara wa Bureau de Change na wengine. Manji alishushiwa ankara zenye zaidi ya Sh12.3 bilioni. Akalipa!

Jambo la kusikitisha, si Manji wala Magufuli aliye hai leo. Magufuli alifumba macho tangu Machi 2021 na taifa likatangaziwa kifo Machi 17, 2021. Manji, naye aliingia usingizini Juni 29, 2024. Wenye ukweli kamili wa hadithi ya “mbwa na mwenye mbwa”, wote wameshalala usingizi wa mauti. Pengine, maisha baada ya kifo yatawakutanisha na wataombana msamaha. Mungu ndiye anajua.

Ameondoka Manji, kwa familia yake alikuwa baba, kaka na mtoto, kwa taifa la Tanzania, alikuwa raia aliyejenga athari chanya kwenye maisha ya wengi. Kupitia biashara zake, aliajiri maelfu ya Watanzania. Kadhalika mamia ya Wahindi walioshushwa kutoka India.

Katika soka, Manji alipata kuwa oksijeni ya Yanga. Alianza na udhamini wa mchezo wa kubahatisha wa Lotto Kitita, baadaye akawa mfadhili mkuu, kisha Mwenyekiti wa Klabu. Kipindi chake, Yanga ilipata mafanikio makubwa uwanjani kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, misimu mitatu mfululizo (2014-2015, 2015-2016 na 2016-2017).

Manji jeuri sana; Juni 28, 2016, Yanga ilicheza mechi ya Kombe la Shirikisho (Caf), dhidi ya TP Mazembe, hatua ya makundi. Mechi ilichezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Kwa kuwa Yanga walikuwa wenyeji na kwa sababu Manji alikuwa na mvutano dhidi ya uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), aliagiza mashabiki waingie bure ili TFF wakose mapato. Halafu upande wa Yanga, alibeba gharama zote yeye mwenyewe.

Manji, nyakati zake za heri, alimpeleka puta mfanyabiashara gwiji Tanzania, Reginald Mengi. Waliendeshana kwenye vyombo vya habari hadi mahakamani. Halafu, Manji kwa jeuri ya fedha, aliwang’oa Original Comedy, East Africa TV, akawapeleka TBC. Yote kumkomoa Mengi. Manji, alikuwemo ndani ya orodha ya “Mafisadi Papa Tanzania”, iliyosomwa na Mengi.

Manji mtata sana; alimburuza Mengi mahakamani kwa kumchafulia jina, halafu akaomba fidia alipwe Shilingi Moja ya Tanzania. Hii ilimaanisha kuwa Manji hakutaka fedha za fidia, isipokuwa alitaka kumshughulisha Mengi. Inasikitisha kuwa leo, wote, Mengi na Manji hawapo duniani. Mengi alivuta pumzi ya mwisho Mei 2, 2019. Pengine maisha baada ya kifo yatawafanya Manji na Mengi kuwa marafiki. Nani anajua?

Manji ni mada nzito; mwaka 2000, akiwa kijana mwenye umri wa miaka 25, aliingia kwa kishindo kugombea ubunge, jimbo la Kigamboni. Fedha alizomwaga zilimtikisa aliyekuwa Mwenyekiti CCM, Rais Benjamin Mkapa, ambaye ilibidi aingilie kati kumdhibiti. Haitoshi, Mkapa amesimulia kuhusu Manji kwenye kitabu chake, “My Life, My Purpose” – “Maisha Yangu, Kusudi Langu.”

Manji, Uchaguzi Mkuu 2015, alishinda udiwani Mbagala Kuu, Dar es Salaam. Alitamani umeya wa Jiji la Dar es Salaam, alikwama baada ya Chadema na Cuf (Ukawa), kushinda viti vingi vya udiwani kuliko CCM. Halafu, Septemba 2017, akiwa katikati ya kesi nyingi zilizomkabili, alivuliwa udiwani kwa utoro.

Hakuna aliyejua kuwa mwisho wa Manji ungekuwa namna hii. Baada ya kuhamia Marekani, Julai 29, 2019, alifunguliwa mashitaka ya kuendesha gari akiwa na kilevi (Driving Under Influence “DUI”), kwenye jimbo la Florida. Mwaka 2021, baada ya Magufuli kufariki dunia, alirejea Tanzania akiwa na matumaini. Akawekwa mahabusu. Alipotoka, aliondoka zake.

Miaka 49 ya kuishi duniani, imetosha Manji kuhitimisha safari. Aliandika Franz Kafka, mwandishi wa Ujerumani: “The meaning of life is that it stops.” – “Mantiki ya maisha ni kwamba hukoma.” Ingekuwa uhai hauna mwisho, maisha yasingekuwa na maana yoyote. Nasadiki.

Shairi la faraja kutoka kwa mwandishi na mwinjilisti wa Marekani, Max Lucado, likujenge imani kuwa kifo si hasara: “We see a hearse; we think sorrow. We see a grave; we think despair. We hear of a death; we think of a loss. Not so in heaven. When heaven sees a breathless body, it sees the vacated cocoon & the liberated butterfly.”

Kiswahili: “Tunaona gari la maiti; tunajisikia majonzi. Tunaona kaburi; tunajisikia kukata tamaa. Tunasikia kuhusu kifo; tunajisikia kupoteza. Haipo hivyo mbinguni. Mbingu inapoona mwili usiopumua, huona kiumbe kilicho huru na kipepeo aliyekombolewa.”

Usiku mwema Yusuf Mehbub Manji. Kitabu changu “Kikwete Lowassa; Urafiki. Ndoa Yao ya Kisiasa. Uadui”, kinapatikana maduka ya vitabu; TPH Bookshop, House of Wisdom na Elite Bookstore. Unaweza kukinunua moja kwa moja kwa kupiga simu namba +255787616381 au +255713355717. Bei ni Sh75,000. Ndimi Luqman MALOTO

Chanzo: www.tanzaniaweb.live