Wasanii zaidi ya 20 waeelezwa kufika wilayani Chato Mkoani Geita kwa ajili ya kushiriki shughuli za kumuaga aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli. Hayo yameelezwa leo na Alhamisi, Machi 25 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hasaan Abbasi, katika shughuli hizo zinazoendelea katika viwanja vya Magufuli wilayani humo. Dk Abbassi alisema katika uhai wake kama kuna kitu Hayati Magufuli alikipigania na kukipangia kukipigania zaidi kikue zaidi ni sekta ya Sanaa na ni katika kumuenzi mpaka kufika leo tayari wasanii zaidi ya 25 wako wilayani Chato kushiriki shughuli mbalimbali za kuaga mwili wa kiongozi huyo.
"Leo hatuko naye mtu huyu John Pombe Magufuli, bingwa katika kuipigania sekta ya sanaa, anapaswa kuimbiwa, nyimbo za maombolezo, nyimbo za kumwombea pumziko la amani na la milele.
"Hivyo leo kuanzia saa 10 kamili jioni hadi saa moja katika uwanja wa Magufuli hapa Chato tumewapa nafasi wasanii wote watakaoweza kufika na waliokwishafika kumuimbia Magufuli kwa nyimbo mbalimbali za maombolezo walizozitunga mmoja mmoja na kama makundi," alisema Dk Abbasi.