WAKATI mtu mweusi alipozidisha harakati za kujikomboa kutoka kwa makucha ya Makaburu pale Afrika Kusini mwishoni mwa miaka ya 1980, Makaburu walisoma alama za nyakati.
Waliamua kukubali kwa hiari yao nyakati zilikuwa zimefika mwisho kwao na lazima wawaachie watu weusi nchi yao. Hivyo walianza kujiandaa mapema.
Katika kujiandaa na utawala wa mtu mweusi, Makaburu walichagua eneo moja lililo kilimani kidogo katika Jiji la Johannesburg na kujenga mji wa kifahari kwa ajili ya maisha yao binafsi. Mji uliitwa Sandton. Ni eneo la kifahari zaidi katika Jiji la Johannesburg.
Kama Chris Brown au Prince William watahitaji usingizi mzuri Johannesburg watafikia katika hoteli moja iliyopo Sandton. Miezi michache iliyopita, Arnold Schwarzenegger alionekana akizurura katika mitaa jiyo ya Sandton. Ni kitu cha kawaida.
Katika mtaa wa Alice Lane, eneo la Sandton, Hoteli ya Sandton Sun, Jumamosi moja ya mwezi huu, eneo la baa nilikutana na mwanamke anayeitwa Zarina Hassan. Kwa Watanzania mwanamke huyu anafahamika zaidi kwa jina la Zari. Kwa yeye mwenyewe na hisia zake, anapenda kujiita Zari TheBossylady.
Akiwa na mavazi ya kifahari katika mwili wake, vito vya kifahari katika mikono yake na hisia kali katika tabasamu lake, hapa nakutana na mwanamke ambaye miezi michache iliyopita alikuwa ameandika sentensi ya mwisho katika hadithi yake ya kusisimua ya mapenzi na mwimbaji maarufu wa kizazi kipya wa Tanzania, Nassib Abdul ‘Diamond Platnumz’.
Zari, mzuri kama alivyo ananitambulisha kwa Meneja wake, Beatrice huku akiwa ameambatana na rafiki zake wawili ambao siwafahamu. Bahati iliyoje. Akiwa na shinikizo la furaha isiyojulikana ilikotokea, huku akiwa na Mvinyo wa bei ghali, Backberg uliotengenezwa tangu 1916 nchini Afrika Kusini, Zari anayafungua maisha yake katika namna ambavyo hajayafungua kwa watu wengi wanaomfuatilia katika mitandao ya kijamii. Ana wafuasi zaidi ya milioni nne katika mtandao wa Instagram.
“Kaka watu wengi hawamfahamu Zari. Tanzania watu wengi hawamfahamu Zari kama ambavyo wanajisingizia kumfahamu. Huwa nawatazama tu, lakini maisha yangu halisi sio haya ambayo Watanzania wanayazungumza mitandaoni na kwingineko,” anasema Zari kwa hisia kali.
“Hiki ndicho kinanisikitisha sana. Kila siku kuna umbea mwingi mitandaoni kuhusu mimi. Umbea mwingi unahusu maisha yangu ya uhusiano na Nassib (Diamond), lakini watu hawawezi kuyajua maisha halisi ya Zari,” anasema Zari.
Akinyanyua glasi yake na kugonga mvinyo kwa furaha, Zari anaonekana mchangamfu zaidi kuliko yule ambaye anaonekana kutulia katika picha za Instagram pamoja na zile ambazo zinamwonyesha katika mihangaiko ya kimaisha.
“Hauwezi kumwambia kila mtu jinsi ulivyo, lakini mwanamke anahitaji kujitegemea na kujielewa. Ni tofauti na wanawake ambao naona nalinganishwa nao mitandaoni na kwingineko. Mimi ni Zari na nitabakia kuwa Zari.
PENZI NA BABA TIFFAH
Haiwezi kuvutia kumzungumzia Zari bila ya kuzungumzia uhusiano wake wa muda mrefu na Diamond Platinumz. Zari hataki sana kuzama ndani kuhusu jambo hilo, lakini anatumia akili kubwa kujilinda mwenyewe na kumlinda Diamond katika uhusiano wao.
Kuna mambo mengi hataki kuyaweka hadharani lakini anakumbuka kila kitu kuhusu mwanzo wa uhusiano wake na Diamond na jinsi ambavyo alianza naye na kufika naye mbali katika maisha. Katika kila sentensi ambayo inamhusu Diamond anaitumia kumwita jina la Nasib au Baba Tiffah. Tiffah ni jina la mtoto wake wa kwanza aliyezaa na Diamond kabla ya kupatikana kwa mwingine aliyejulikana kwa jina la Nillan.
“Kwangu mimi Nassib anabakia kuwa baba watoto wangu. Tumeachana. Ninamheshimu sana kwa sababu ameniletea watoto wawili na nina furaha sana. Huyu Tiffah ananipa furaha sana kwa sababu ni mwanangu pekee wa kike. Tayari nina watoto wa kiume lakini sikuwahi kuwa na wa kike. Hata hivyo ukurasa wangu na Nassib umefungwa,” anasema kwa hisia kali.
WALIPOANZIA
Zari anashindwa kuficha hisia zake juu ya kuingia kwenye uhusiano na Diamond kwa kusema;
“Nilipoanza uhusiano na Nassib nilijishusha sana kwa sababu nilitaka kutulia na mwanamume huyu na kufanya maisha. Nilijua Nassib ni staa nami nilikuwa mwanamke wa kiwango cha juu, ila nikasema embu kwanza acha nijishushe nilitaka kuishi naye.”
“Katika uhusiano ni vizuri kumwacha mwanamume awe mwanamume na wewe mwanamke uwe mwanamke. Hauwezi kushindana na mwanamume. Nilipotoka nilikuwa mwanamume ambaye alikuwa ana kila kitu (Ivan Ssemwanga, mpenzi wake wa zamani ambaye kwa sasa ni marehemu) lakini nikasema acha nijishushe.”
MALAVIDAVI YAKE NA IVAN
Katika dunia ya Zari ambayo wengi hatuifahamu, Zari anafungua moyo wake na kukubali jinsi gani ambavyo Ivan alikuwa akimpenda sana, lakini penzi lao liliyumba kadri mpenziwe huyo alivyokuwa akimnyanyasa kiasi cha kufikia kumpiga.
“Ivan alikuwa ana pesa sana, sawa, lakini kuna wakati alikuwa ana tabia za ajabu, unajua alikuwa mtu wa makundi na kuna wakati maisha yake yote yalikuwa ya starehe tu. Pia alikuwa mkali kwangu kiasi cha kuanza kunipiga.”
Kufikia hapo Zari anafungua mkono wake wa kulia na kuonyesha alama aliyoachiwa na Ivan kutokana na ugomvi mmoja wa mapenzi baina yao. Katika maongezi yote, Zari anaonekana bado anampenda na kumkumbuka Ivan. Haonyeshi kuendelea kuwa na kinyongo chochote, lakini anaufungua moyo wake na kukiri udhaifu huu wa Ivan dhidi yake.
“Ilipofika hapo nikasema basi lazima ifike mwisho. Nikaachana na Ivan aendelee na maisha yake mengine nami niendelee na maisha yangu mengine. Sikujali sana kuhusu pesa kwa sababu nampenda mwanamume anayenijali mimi kama mwanamke na kunipa heshima yangu.”
Mkononi mpaka leo Zari ana pete ya uchumba ya Almasi aliyonunuliwa na Ivan. Kwa mujibu wake ina thamani ya Dola 20,000 za Marekani. Ana saa aina ya Rolex yenye thamani ya Dola 12,000, pia akiwa amevaa cheni ya mkononi yenye thamani ya Dola 5,000 za Marekani.
“Unaweza kwenda katika mitandao na kuangalia thamani ya vitu hivi. Unaweza kupiga picha na kutafuta link ya kujua hivi vitu vina thamani gani. Sina haja ya kujisifu,” anasema Zari huku akivua pete yake na kunikabidhi.
KWANINI HAKUOLEWA NAYE?
Kwa kusikiliza simulizi lake na mahaba yake na Ivan, nashawishika kumuuliza Zari; Kwa nini hakuolewa na Ivan licha ya kuvalishwa pete hiyo ya uchumba yenye thamani kubwa?
Zari haonekani kujutia uamuzi wake wa kutoendelea penzi lake na Ivan licha ya kwamba mambo hayakuenda sawa na Diamond Platinum.
“Hapana, ilifika wakati nikasema inatosha. Sikuona sababu ya kuolewa na Nigga Ivan. Unajua Ivan alikuwa anadhani kuninunulia magari ya kifahari au vito vya thamani au kunipa pesa nyingi kungeweza kunifanya niwe chini yake na kumsikiliza. Sio hivyo. Unaweza kunipa kila kitu lakini mwishowe nakutaka wewe hapo. Mwanamume anabakia kuwa mwanamume tu,” anasema Zari.
“Alikuwa na mambo mengi na hakunipa heshima iliyostahili. Mimi ni mwanamke ninayethamini zaidi utu na heshima. Mambo ya pesa, magari na dhahabu ni nyongeza tu, lakini kitu cha muhimu zaidi ni mapenzi.”
Je, mnajua kabla ya kutua kwa Diamond, Zari alishawahi kutoka na kidume kingine, tena cha kawaida? Itaendelea kesho Ijumaa...!