Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Uwanja Sokoine Mbeya gumzo kila kona nchini

Video Archive
Sun, 29 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya/Dar. Wakati mchezo baina ya Prisons na Yanga ukihamishwa mkoani Mbeya, Uwanja wa Sokoine umeibua mjadala baada ya kuharibiwa katika tamasha la muziki.

Prisons na Yanga sasa zitacheza mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Samora Iringa. Awali ulipangwa kuchezwa Uwanja wa Sokoine.

Zikiwa zimebaki saa chache kabla ya mchezo huo kufanyika, Bodi ya Ligi ilitoa tamko la kuhamishia mchezo huo mkoani Iringa kutokana na ubovu wa eneo la kuchezea la Uwanja wa Sokoine.

Juzi wasanii Nassib Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’ walifanya tamasha la muziki katika uwanja huo jambo lililosababisha uharibifu kwenye sehemu ya kuchezea (pitch).

Mjadala mkubwa ulitawala jana katika mitandao ya kijamii wakihoji uamuzi wa uwanja huo unaomilikiwa na CCM kutumika kwa tamasha hilo zikiwa zimebaki saa chache kabla ya kuchezwa mechi.

Akizungumza jana, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Boniface Wambura alisema wameupeleka mchezo huo Iringa baada ya kuufungia kwa muda uwanja wa Sokoine.

“Bodi imezuia Uwanja wa Sokoine Mbeya kutumika kwa mechi za Ligi Kuu.Uamuzi huo umetokana na eneo la kuchezea (pitch) kuharibika vibaya kutokana na tamasha la muziki lililofanyika jana (juzi).

Klabu za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili ambazo timu zake zilikuwa zikitumia uwanja huo zimeelekezwa kutafuta viwanja mbadala,”ilisema taarifa kutoka Bodi ya Ligi.

Kauli ya CCM

Wakati mjadala mkali ukiibuka kuhusu matumizi ya uwanja huo, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Bashiru Madodi alisema kitendo cha kuruhusu tamasha lililosababisha kuharibu uwanja huo ni kashfa na aibu kwa viongozi wa CCM mkoa huo ambao wamepewa dhamana ya kusimamia mali za chama kutoka kwa wanachama wao.

Alisema viongozi wa CCM lazima wakutane kupata majibu ya mambo matatu ikiwemo kutaka kujua nani aliyekwenda kuomba uwanja huo utumike kwa tamasha hilo, mtu aliyetoa idhini na kujua ni kiasi gani cha fedha kilichotolewa kwa CCM ili kuruhusu tamasha hilo lifanyikie uwanjani hapo.

Prisons

Mwenyekiti wa Prisons, Enock Mwanguku alisema chama cha soka mkoa na wamiliki wa uwanja wanapaswa kujitafakari katika matumizi ya uwanja huo.

“Unapoleta tamasha la muziki kama hivi matokeo yake unaharibu soka la Tanzania, wameharibu uwanja ina maana wamevuruga mapato ya wananchi wa Mbeya kwasababu timu zinapokuja wanakodi gesti, magari na wananunua vyakula. Lakini ukishafungiwa watakosa mapato,”alisema Mwanguku.

Wadau walonga

Kocha wa Mwadui, Khalid Adam alisema suluhisho la jambo kama hilo ni timu kuwa na viwanja vyao na si kutegemea viwanja vya watu wengine.

“Lazima tujue viwanja ni vya nani na mwenye mamlaka ya viwanja vinavyotumika kwenye mpira ni nani.

“Viwanja sio vya timu na wenye mamlaka ya viwanja wana uhuru wa kufanya chochote wanachotaka. Hizo ni changamoto zinazotukabili lakini hatuna wa kumlaumu kwasababu klabu zetu hazina viwanja,”alisema Khalid.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila alisema kila timu inatakiwa kuwa na uwanja wake kama kanuni zinavyotaka.

“Vile viwanja vinamilikiwa na CCM ndio wanajua matumizi ya viwanja yakoje ikiwemo mpira na matamasha mengine. Klabu hazimiliki viwanja hapo ndipo tatizo linapoanzia.

“Wamiliki wa viwanja wanatakiwa kuwa na ukaribu na uhusiano mzuri na Bodi ya Ligi ili kupeana utararibu wa kuvitunza viwanja kwa matumizi mbalimbali ikiwemo mechi za ligi. Klabu zinatakiwa kujitahidi kuwa na viwanja vyao,”alisema Katwila.

Chanzo: mwananchi.co.tz