Kwa kawaida safari ya kutoka Dar es Salaam mpaka Tanga huchukua kati ya saa sita mpaka nane, lakini ya kusafirisha mwili wa nguli wa maigizo nchini, Mzee Majuto ilichukua takribani saa 10 baada ya msafara wake kuwa unasimamishwa njiani na mashabiki wake.
Mwili wa muigizaji huyo ambaye jina lake halisi ni Amri Athumani uliwasili nyumbani kwake katika Mtaa wa Donge juzi saa 7.05 usiku baada ya kusimamishwa katika vijiji 16 na mashabiki wakitaka kutoa heshima ya mwisho.
Safari ya kwenda Tanga kwa ajili ya mazishi ilianza saa 10.00 jioni baada ya kumuaga katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam.
Magari ya waombolezaji yaliongozana kupitia Barabara ya Bagamoyo na kituo cha kwanza kusimamishwa na wananchi kilikuwa Kijiji cha Mkata ambako mamia ya wananchi wa eneo hilo walisimama kando ya barabara wakisubiri kushuhudia msafara huo.
Vijiji vingine ambavyo msafara huo ulisimamishwa ni Kabuku, Kwedizinga, Michugwani, Hale, Maguzoni, Kwabastola na Kibanda.
Vijiji vingine ambavyo wananchi walikesha barabarani wakisubiri kuushudia msafara huo ni Muheza, Lusanga, Mkanyageni, Pongwe, Majani Mapana, Mwamboni, Kwa Minchi na Mabanda ya Papa.
Kila msafara huo uliposimama wananchi hao walisikika wakimuombea kwa dini zote huku wengine wakilia kwa uchungu. Wapo waliokuwa wakilia huku wakiita Baba na na wengine Babu.
“Huyu ni mzee wetu jamani, tuko hapa toka saa 12 tukisubiri tumuone tu, yaani namkumbuka sana marehemu kwa sababu alikuwa ni mchekeshaji ambaye tulikuwa tunajivunia katika kijiji chetu cha Kibanda,” alisema mmoja wa waombolezaji kijijini hapo
“Usituone tuko hapa, sisi Mzee Majuto kwetu ni kama almasi, alikuwa anatujali sana, maana alikuwa akitoka Dar es Salaam lazima ashuke hapa Muheza kutusalimia, yaani alikuwa sio mtu wa majivuno,” alisema mkazi wa Muheza aliyejitambulisha kwa jina la Ally.
Katika muda wa saa nane shughuli mbalimbali zilisimama katika Jiji la Tanga baada ya umati wa watu kuelekea msibani.
Barabara ya Tanga Beach mpaka Duga Mwembeni ilifungwa ili kuwapa nafasi watembea kwa miguu waliokuwa wakimiminika kuelekea nyumbani kwa Mzee Majuto
Mwandishi wa Mwananchi, Burhan Yakub alisema hajawahi kushuhudia umati mkubwa wa watu katika eneo moja katika Jiji la Tanga kama huo.
“Mtu alitembea umbali wa kilomita mbili akijivuta katikati ya umati wa watu waliosimama kutoka ilipo nyumba ya Mzee Majuto,” alisema.
Mbali na umati kuwa mkubwa, ilikuwa fursa kwa wasafirishaji kwani daladala, teksi, bajaji na bodaboda zote zilifanya safari kuelekea Donge.
Daladala zote zilisitisha ruti zake na kufanya moja inayoelekea huko kwa kuwa asilimia kubwa ya wakazi wa jiji hilo walikuwa wakielekea msibani.
Wasanii wawa kivutio
Moja kati ya matukio yaliyovuta watu katika msiba huo ni uwepo wa wasanii maarufu nchini kama Mhogo Mchungu, Shamsa Ford, Cloud 112, Harmonize, Riyama Ally, Steve Nyerere, Simon Mwakifamba, Baba Haji na wengine wengi.
Baadhi ya waombolezaji walifanya kazi ya ziada wakitaka kuwashika mikono na kupiga picha na wasanii hao ambao wengi wamewahi kufanya kazi na Mzee Majuto.
Kuanzia saa 5.45 mchana, ibada ya mazishi ilifanyika katika msikiti wa Nuruguda uliopo karibu na nyumbani kwake na kuzikwa kijiji cha Kiruku yalipo mashamba yake nje kidogo cha jiji la Tanga.
Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela waliongoza mamia ya waombolezaji waliofika kumsindikiza Mzee Majuto katika safari yake ya mwisho.
Kwa upande wa dini, Sheikh wa Mkoa wa Tanga, Juma Luwuchu alisoma dua katika Msikiti wa Nur ul Huda uliopo katika Mtaa wa Donge kabla ya safari ya kuelekea Kiruku kuanza.
Wakazi wa jiji la Tanga walijipanga barabarani kuanzia Donge mpaka stendi ya zamani ya Ngamiani wakiupungia msafara ulipita katika miji ya Amboni na Mabokweni ambako kote watu walijazana barabarani.
Tanga wamlilia
Sheikh Rahim wa Msikiti wa Nurulhuda, alisema Mzee Majuto alikuwa mtu wa kusaidia wakazi wa Tanga na vitongoji vyake hasa katika masuala ya dini.
Alisema Mzee Majuto amechangia kiasi kikubwa katika ujenzi wa msikiti anaouongoza uliopo Donge karibu na nyumbani kwake na pia ni mwanzilishi wa madrasa akichangia ujenzi wa vyumba viwili.
Alisema katika Kijiji cha Mabokweni Kiruku ambako amezikwa, Mzee Majuto alitoa eneo lake moja la shamba na kujenga msikiti kwa ajili ya wanakijiji.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Waziri Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amewataka wasanii kuhakikisha wanawekeza ili kuweza kuandaa kesho yao kwa kufanya mema badala ya kuendelea kufanya starehe pekee.
Waziri Mwalimu ambaye ni mbunge viti maalumu mkuu wa Tanga, alitoa wito huo jana alipofika kuifariji familia ya marehemu King Majuto.
Alisema kuwa ni vyema wasanii wakaitumia sanaa kama ajira ili fedha wanazozipata wakazitumia katika mambo mema yatakayo mpendeza mwenyezi Mungu pamoja na kuacha alama wanapoondoka duniani.
Alisema ni wakati wa wasanii kuiga maisha aliyokuwa akiishi Mzee Majuto kwani amefanya mengi atayoweza kukumbuka na Watanzania na Dunia kwa Ujumla.
“Mzee Majuto amefanya mengi ikiwemo kujenga madrasa na msikiti katika eneo la Kiruku ambalo ndiko aliko zikiwa,” alisema Waziri Huyo.
Wakati huo Waziri Ummy alisema Kifo cha Mzee Majuto kimewaachia pengo kubwa wao kama wakazi wa Tanga na Tanzania kwa ujumla.
Alisema kuwa kama Serikali walijitahidi kutoa fedha za matibabu za kumpeleka Hospitali ya Muhimbili na India lakini juhudi za madaktari hazikuzaa matunda .
Mara ya mwisho walikutana siku chache kabla ya kwenda nchini India kwa matibabu ambapo alivyokutana naye alimpa Moyo na kumtakia safari njema .