Msanii Rich Mavoko amefikisha malalamiko yake serikalini kwa kutoridhishwa na mkataba aliopewa na uongozi wake wa WCB.
Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mngereza alipozungumza na MCL Digital kufafanua kuhusu madai ya mwanamuziki huyo kwa lebo hiyo inayoongozwa na Diamond Platnumz.
Mavoko ameonekana katika ofisi za Basata leo Agosti 9.
Kuhusu tukio la yeye kuonekana katika ofisi hizo, Mngereza amesema alikwenda kwa ajili ya kujisajili kwani hakuwa amepitia utaratibu huo.
"Naomba ieleweke kwamba hakuna kesi yoyote tuliyoletewa na Rich na alichokuja leo ofisini kwetu ni kwa ajili ya kujisajili,” amesema.
Akifafanua kuhusu suala la mgogoro wake na WCB Mngereza amesema,
“Tunachokijua hadi sasa kuna malalamiko alishayaleta kuhusu kutoridhika na mkataba alioingia na WCB na tayari tumepeleka kwa kamati iliyoundwa na Waziri ya kufuatilia mikataba hiyo.”
Akizungumzia madai hayo mmoja wa viongozi wa lebo ya WCB, Babu Tale amesema hayupo katika nafasi ya kumzungumzia Rich Mavoko akitaka waulizwe Basata.
“Mimi siwezi kulizungumzia hilo waulizeni Basata,” amejibu kwa kifupi.
Soma zaidi: