Dodoma. Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ametaja sababu za kuacha muziki na kuamua kujikita katika shughuli nyingine, akibainisha kuwa uamuzi wake huo utafikia tamati miaka mitatu ijayo.
Sugu ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 47 ametoa kauli hiyo juzi Jumatatu Juni 3, 2019 katika mahojiano maalum na Mwananchi jijini Dodoma akibainisha atajikita katika masuala mengine ikiwemo biashara lakini hana ndoto za kuacha siasa.
Amesema jambo hilo si la kuacha ghafla ni lazima lifanyike kwa utaratibu kulingana na ushauri wa wadau wa muziki na mashabiki wake.
Sugu ambaye aliandika uamuzi wake huo katika mitandao ya kijamii amesema, “Ndio maana tuliwashirikisha watu, pale nilikuwa nawaeleza watu wangu ili nipate mawazo yao, watu wamesema nitoe albamu ya kuaga wasanii, wengine wanasema nifanye tamasha na hivyo si vitu vya siku moja.”
“Kama wanataka albamu mie nitapanga nije na ipi na nimshirikishe nani. Mpaka napumzika itakuwa miaka mitatu.”
“Ndoto yangu kwa sasa ni kufanya mambo ambayo sikuwahi kuyafanya katika kipindi cha zaidi ya miaka 20 katika muziki. Nataka kuwashirikisha wakina Jay Z hata Nas katika albamu yangu ya mwisho.”
Pia Soma
- Sheikh awataka Waislamu kuyaendeleza mema ya Ramadhan
- Magufuli atoa maagizo kwa Ma-DAS, ofisa tarafa nchi nzima
- Rihanna ambwaga Beyonce kwa utajiri
Soma mahojiano zaidi katika Jarida la Starehe Jumamosi June 8, 2019