Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Harusi ya Sugu ilivyowafanya viongozi kusahau tofauti zao

Video Archive
Thu, 5 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila usiku wa Jumamosi aliungana na viongozi wengine kwenye sherehe ya harusi ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Happness Msonga iliyofanyika katika hoteli ya Desderia iliyopo Uzunguni jijini hapa, na kuipambana sherehe hiyo kwa kuonesha umahiri wake katika kucheza muziki.

Jumamosi iliyopita, Sugu alifunga ndoa ya kikatoliki na Happness katika Kanisa Katoliki la Roho Mtakatifu, Parokia ya Ruanda Jimbo Kuu la Mbeya, na kufuatiwa na sherehe iliyofanyika nyumbani kwa marehemu mama yake eneo la Sai hadi saa 12:00 jioni, kisha aliandaa hafla fupi kwa wageni waliofika kumsindikiza iliyofanyika usiku kwenye hoteli yaake ya Desderia.

Wageni mbalimbali wakiwamo wabunge, viongozi wa kisiasa wakiwamo wa CCM, Chadema na wa Serikali walianza kumiminika hotelini saa 1:00 jioni, na Chalamila akiwa ameambatana na mke wake alifika katika viwanja hivyo saa 2:40 usiku na kupokewa na wabunge wakiongozwa na Joseph Selasini na meya wa Jiji la Mbeya, Mchungaji David Mwashilindi.

Baada ya muda mfupi, mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, katibu mkuu wake, Dk Vicent Mashinji, na naibu katibu mkuu-Zanzibar, Salum Mwalimu waliingia eneo la tukio na kuamsha shangwe kutoka kwa watu waliokuwa wakiendelea kuburudika na muziki.

Viongozi hao walisalimiana kwa furaha na shangwe na wageni wengine akiwamo Chalamila na kuleta utani wa hapa na pale. Pia aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya kabla ya kutimikia CCM, Wakili Shambwee Shitambala ambaye alipambana na Sugu kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ubunge wa Mbeya Mjini mwaka 2015, alikuwa miongoni mwa watu maarufu waliohudhuria.

Baadae Sugu na mkewe Happness waliingia kwenye viwanja hivyo na kuamsha shangwe kutoka kwa waalikwa wote waliokuwa wamesimama ikiwa ni ishara ya kuwapokea maharusi hao.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Muda huo huo, wakaingia Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Mary Mwanjelwa na Mbunge wa Songwe, Philip Mulugo ambao nao waliliungana kucheza muziki.

Hapo ndipo Chalamila alipoinuka na kujichanganya na watu wengine kucheza muziki ambapo alionekana kutia fora kutokana na ustadi wake wa kusakata muziki huku akiwa ni mwenye furaha, akikumbatiana na kumpongeza Sugu.

Alichosema Sugu

Baada ya burudani, Sugu alipewa kipaza sauti ili aweze kufanya utambulisho na kuwakaribisha wageni na kuwashukuru wote waliohudhuria sherehe hiyo, ambapo alisema kutokana na mchanganyiko wa wageni waliofika alipenda sherehe yake iitwe ‘Wedding Diplomacy’.

“Niwashukuru sana ndugu zangu kwa ‘support’ yenu tangu asubuhi kanisani hadi usiku huu. Nimepewa jukumu nitambulishe ndugu na jamaa, lakini leo nilimuomba hata MC (mshereheshaji) kwamba sitaki ile ‘high table’ (meza kuu). Nilisema leo ni ‘kuji-mix’ (kujichanganya) kitu cha nyama, pweza, samaki, kitu cha whisk, bia, juisi na kila mmoja hapa anavyotaka kufurahia.

“Hapa namuona hata mwenyekiti wangu (Mbowe) pale amekaa na Masala kutoka Pemba sijui kutoka chama gani, namuona Mheshimiwa ‘My Friend’ (Rafiki yangu) Albert (Chalamila) yupo karibu na katibu mkuu mstaafu wa wizara, Mama Mollery (Lucy), yupo na Silinde (David) wana ‘share’ (wanashirikiana) glasi.

“Ningependa tuiite hii sherehe ‘wedding Diplomacy’ ili kuweka mambo sawa kule tunakokwenda mbele, Mbeya haki ya Mungu napenda sana ushirikiano wenu kwetu,” alisema.

Baada ya kuwatambulisha ndugu kwa kusimama na kusalimia, Sugu alisema miongoni mwa watu ambao walitamani kuiona siku hiyo muhimu katika maisha ni marehemu mama yake Desderia Mbilinyi, hivyo aliwaomba watu wote kusimama na kukaa kimya kwa dakika moja ikiwa ni ishara ya kumkumbuka na kumuombea kwa Mola.

Alisema “ambaye nina-mmiss hapa ni mama na kwa heshima yake naomba tusimame kwa dakika moja kwa sababu najua alitamani sana hii siku kuiona…sahamani sana”.

Zawadi ya wabunge

Akizungumza kwa niaba ya wabunge, Selasini, alisema bila kujali tofauti za vyama vyao, Sugu anafanya kazi ya wananchi wa Mbeya kwa kushirikiana na wabunge wengine ndio maana hata sherehe hiyo imehudhuriwa na wabunge wa CCM, hivyo kwa pamoja walimuandalia zawadi ya picha 18 za watu maarufu dunia ambazo ziligawanywa katika makundi matatu yenye maana tofauti.

“Nazungumza hapa kwa niaba ya wabunge wenzangu kama mnavyotuona tulivyosimama, tupo hapa tunafanya kazi pamoja na mheshimiwa Sugu, na Sugu anashirikiana na wabunge wote ndio maana mnamuona mama Mwanjelwa (Mary) na Mheshimiwa Philip Mlugo wote wanatoka Chama Cha Mapinduzi,” alisema Selasini.

Alisema kwa umoja wao waliona zawadi nzuri ya kumkabidhi Sugu iwe kumbukumbu ya maisha yake, zawadi ya picha 18 za watu maarufu wakiwamo wanamuziki, wanasiana na viongozi wa kikatoliki.

Selasini alisema kundi la kwanza, ni picha za wasanii maarufu duniani na aliwataja baadhi yao ni Bob Marly, Lucky Dube, Jayz, mwanamasumbwi Mike Tyson, wakimwambia Sugu kwamba hakukosea hata kidogo kuwa msanii wa muziki na yeye mwenyewe (Sugu) anatambua kazi na wito wake kuwa msanii umechangia kwa kiwango kikubwa kumfikisha mahali alipo sasa, hivyo walimtaka kutoiacha kazi hiyo.

Alisema “na kwa sababu hiyo, tunataka tumuambia asiiache kazi hii (usanii wa muziki) na hata kama nguvu zitakapompungua basi awasaidie wadogo zake wasanii wachanga, awafunde ili waweze kufikia pale alipofikia yeye. Na hizi picha atakapozining’iniza popote atakapotaka zimkumbushe kwamba hawa watu ni ‘Model’ kwake na kila atakapoziangalia basi akumbuke kuendeleza kazi hii’.

Kundi la pili la picha ni za wanasiasa na wanaharakati, na miongoni aliowataja ni Hayati Nelson Mandela wa Afrika Kusini, hayati Julius Nyerere wa Tanzania, Martin Luther King, Patrice Lumumba wa Kenya, Nkwame Nkrumah, wa Ghana, Mahati Magandi wa India, na Mwanaharakati Che Guevara wa Cuba mwenyeasili ya Algentina.

Selasini alisema viongozi hao wamefanya mambo makubwa duniani hivyo wanamtakia Sugu akuwe katika siasa na afanane na watu hao na kumuaminisha kwamba hakukosea kuwa mwanasiasa na sasa amekuwa mkongwe katika ulingo huo.

Kundi la tatu, Selasini alisema kwa vile Sugu na mkewe Happness ni Wakatoliki, hivyo walimkabidhi picha mbili za viongozi wa dini hiyo akiwamo Baba Mtakatifu Yohane Paul II, huku akisema kiongozi huyo wa kiroho alihubiri zaidi upendo kwa mwanadamu.

Chalamila

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambaye ni kada wa CCM ambaye kabla ya kuteuliwa katika nafasi hiyo alikuwa mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Iringa, kwa muda wote alionekana kuwa karibu na Sugu katika hafla hiyo.

Mara kwa mara Chalamila ambaye katika majukwaa ya kisiasa amekuwa na upinzani mkali kwa Sugu, alionekana akiteta na mbunge huyo huku akiwa mchangamfu, mwanye furaha wala kutoonekana na hata chembe ya tofauti baina yake na Sugu.

Chanzo: mwananchi.co.tz