Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

Taasisi ya Dk Mengi inavyoendelea ‘kuwabeba’ wenye ulemavu nchini

9c854c85f230b01959827a290c973703 Taasisi ya Dk Mengi inavyoendelea ‘kuwabeba’ wenye ulemavu nchini

Tue, 26 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KWA mujibu wa Shirika la Afya duniani (WHO) inakadiria kuwa ifikapo mwaka 2030, kutakuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wenye matatizo ya akili na kisaikolojia sanjari na idadi ya juu ya waathirika wengine kupitia aina nyingine za ulemavu.

Kutokana na hali hiyo, inatajwa kuwa gharama za matibabu pamoja na gharama za kiuchumi kwa dunia itakuwa kubwa na hivyo kuleta changamoto kwa jami ikiwemo ya Watanzania ambao wengi wao bado wanaishi wakiwa na kipato cha wastani wa chini ya ya dola moja kwa siku.

Katika kuihamasisha jamii kutambua changamoto zinazowakumba watu wenye ulemavu nchini na kutoa msaada wa matibabu, Taasisi inayoshughulika na malezi kwa watu wenye ulemavu ya ‘‘Dr Reginald Mengi Persons with Disabilities Foundation” (DRMF), hivi karibuni iliandaa matembezi jumuishi kwa lengo la kuongeza uelewa wa magonjwa na ulemavu wa afya ya akili, kisaikilojia na usonji yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam na kuudhuriwa na watu mbalimbali.

Kimsingi kupitia matembezi hayo yaliyokuwa yamebeba kauli mbiu ya Umoja wa Mataifa (UN) ya siku ya mtu mwenye ulemavu Duniani ya mwaka 2020, inayosema “Sio Kila Ulemavu Unaonekana” taasisi hiyo iliandaa matembezi hayo maalumu kwa lengo la kuchangia matibabu ya magonjwa ya afya ya akili.

Aidha kwa mujibu wa WHO, usonji tatizo la kibaiolojia analopata mtoto anapokuwa tumboni mwa mama yake, humpata mtoto mmoja kati ya kila watoto 160 duniani na zaidi dalili zake huonekana kuanzia umri wa miaka mitatu na kuendelea.

Kabla ya hapo wataalamu wanasema ni aghalabu kuona dalili hizo ambapo zinapojitokeza mtoto hukosa mbinu za uhusiano, anashindwa kuzungumza na wakati mwingine kurukaruka na hata kujing’ata, ripoti hiyo inasema watoto wenye tatizo hilo wengine hutekelezwa na jamii na kunyimwa haki zao za msingi ikiwemo kuishi, kuendelezwa, kulindwa na kushirikishwa.

Hata hivyo katika siku ya kimataifa ya usonji duniani inayoadhimishwa Aprili 2 kila mwaka, UN imetaka elimu zaidi ili jamii ibadili mtazamo kwani watoto wenye usonji wakipatiwa huduma mapema wanaweza kushiriki vyema katika jamii zao kwani wana uelewa wa hali ya juu.

Katika matembezi hayo yaliyoandaliwa na DRMF, na kuwashirikisha pia watu wenye ulemavu, mbali na dhima ya kukusanya fedha hizo kwa ajili ya kusaidia matibabu ya watu wenye ulemavu wa akili, pia yalilenga kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na tatizo la usonji ili kuondoa ubaguzi kwa waathirika wa tatizo hilo lakini pia jamii inayowalea.

“Dhumuni kubwa ni kutoa hamasa kwa jamii yote kuona umuhimu wa kuchangia fedha kwa ajili ya matibabu hayo lakini pia kujenga uelewa katika jamii pamoja na wadau mbalimbali waweze kuutambua ulemavu huo na kufahamu changamoto zinazohusu aina za ulemavu na kushirikiana kwa pamoja katika kutoa huduma zinazohitajika kwa watu wenye matatizo hayo” anasema Mkurugenzi wa DRMF, Shimimana Ntuyabaliwe.

Anasema waliona ni muhimu kuihamasisha jamii kuchangia gharama za matibabu hayo kwa watu wenye matatizo hayo kutokana na kuwa dawa wanazopaswa kutumia kwa kila mwezi ni ghali na zina umuhimu sana katika kulinda na kujenga afya ya akili Ntuyabaliwe anasema kwa kushirikiana na wataalamu wa afya ya akili wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), taasisi hiyo inakusudia kuendesha kambi mkoba za afya ili kutoa elimu pamoja na huduma ya uchunguzi kwa walengwa ikiwa ni pamoja na kwa watoto wenye usonji katika mikoa ambayo ina matukio mengi ya watu wenye ulemavu wa akili, ulemavu wa kisaikolojia pamoja na usonji ikiwemo Dar es Salaam, Kilimanjaro, Iringa na Singida.

Anasema hayo ndiyo malengo ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 2018 chini ya muasisi wake marehemu Dk Reginald Mengi ambaye katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita amekuwa mhimili mkubwa kwa watu wenye ulemavu kwa kusaidia katika nyanja mbalimbali kuwajengea ustawi bora wa maisha bila ya kuwabagua kwa kigezo chochote.

Anasema katika kulisimamia hilo na kulitekeleza, Dk Mengi enzi za uhai wake mbali na kutoa misaada ya moja kwa moja ikiwemo matibabu na mengineyo kwa watu wenye ulemavu, pia aliweka utaratibu wa kukutana na watu hao kila mwaka kupitia hafla maalumu ambayo mara nyingi ilikuwa ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Lengo maalumu ya hafla hiyo ilikuwa ni kuwakutanisha pamoja watu wenye ulemavu na kufurahi nao kwa chakula na vinywaji ili kuondoa dhana ya ubaguzi iliyotawala miongoni wana jamii ya kuwa watu wenye ulemavu ni tegemezi, suala ambalo mara nyingi Dk Mengi alikuwa akipingana nalo na kusisitiza kuwa watu hao ‘wakiwezeshwa wanaweza’

Anasema kama hiyo haitoshi, ili kuwahamasisha kundi hilo la wetu wenye ulemavu kushiriki shughuli mbalimbali katika jamii, DRMF iliweka utaratibu wa kutambua mchango wao katika nyanja mbalimbali kwa kuandaa tuzo maalumu za ‘I CAN’ zilizokuwa zikishindanishwa miongoni mwao na kuwapata wale bora kupitia utaratibu wa mashindano hayo.

Ntuyabaliwe anasema taasisi hiyo ya DRMF chini ya ukurugenzi wake imeendelea kubeba pamoja na mambo mengine jukumu kubwa la kulinda na kuenzi ‘legacy’ ya muasisi wake Dk Mengi (marehemu) kwa kuendeleza kazi aliyoifanya kwa zaidi ya miongo mitatu ya kuwahudumia watu wenye ulemavu nchini.

Chanzo: habarileo.co.tz