Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NO AGENDA: Hivi Kanumba, Ngwair, King Majuto ndio wamekufa kiukweli?

92383 Pic+majuto NO AGENDA: Hivi Kanumba, Ngwair, King Majuto ndio wamekufa kiukweli?

Mon, 20 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

STEVEN Kanumba ‘The Great’ amekufa. Ndiyo amekufa jumla. Sasa hivi wanasimuliana “Kanumba alikuwa fundi Bongo Movie”, tunasimuliana tu!

Kizazi cha sasa kitapotea na Kanumba atasahaulika jumla. Msanii kusahaulika ni kosa la jinai. Msanii huwa hafi, kwa hiyo haiwezekani asahaulike. Msanii hupokea wito wa kuagana na dunia kwa sababu ni agizo la Mungu kuwa binadamu lazima arejee mavumbini!

Msanii kwa kazi zake huendelea kuishi kila siku. Msanii huwa hafi jumla. Hapa Tanzania kwetu kina Marijan Rajab pamoja na ujabali wake wa muziki lakini ameondoka jumla. Tatizo siyo yeye, ni Tanzania yetu na mwamko mdogo wa sanaa.

Mbaraka Mwishehe, mpaka leo watu wanaimba Mtaa wa Saba. Matunda hayapo, kama nchi tuliamua aondoke na sanaa yake. Mara moja moja ndiyo nyimbo zake zinachezwa baa, “Shida haikosekani hata siku ya harusi”, kisha walevi wanagonga glasi na kusema: “Mzee alikuwa fundi.”

Mzee Kassim Mapili emeondoka hivi karibuni, hata akiwa hai thamani yake haikuonekana pamoja na Rangi Yake ya Chungwa! Hivi kaondoka, basi ndiyo kabisa. Unamuuaje jumla Mzee Mapili?

TX Moshi William na uhodari wake wa kutunga pamoja na sauti yake nzuri, wapi alipo leo. Kifo kilipomchukua na bendi yake ya Msondo nayo ikapoteza hadhi.

Pia Soma

Advertisement
Msondo ilimbakiza Kamanda Maalim Muhidin Gurumo ambaye TX Moshi alipofikwa na mauti yeye alibaki mgonjwa. Siku ikawadia Maalim Gurumo akaipa kisogo dunia. Wito wa Mungu haukwepeki!

Unawezaje kuwasahau Gurumo na TX Moshi? Tanzania tumekuwa na uthubutu wa ajabu mno. Eti hatuna mbinu bora za kuwafanya watu hawa adhimu waendelee kuishi hata baada ya kuingia kaburini.

Juma Kilowoko ‘Sajuki’ amesahaulika mapema pamoja na kuwepo kwa simulizi ya kuumiza kuhusu maradhi yake mpaka kifo.

Adam Kuambiana hata wasanii wenzake wanamtaja kwa kuvizia, tena pale wanapokuwa wamekwama maeneo fulani ya kikazi ndiyo wanasema: “Angekuwepo Kuambiana hapa hili lisingekuwa tatizo!”

Hakika inauma mno kumkumbuka Sharo Millionea na ubitozi wake. Aliitenda sanaa yake ya comedy vizuri kwa kuigiza usharobaro. Alitokea kuwa mashuhuri. Alizikwa kwa kishindo na kweli alizikwa jumla. Hakumbukwi tena!

Acha nishike tama! Eti hata Albert Mangweha ‘Ngwair’, naye ameondoka kimoja. Inakuwaje tena Mfalme wa Freestyle katika Bongo Rap?

Maskini Ngwair mwenye kichwa kama mgodi wa Tanzanite, kutokana na ufundi mkubwa aliokuwa nao wa kutunga na kurap, kweli imekosekana njia ya kumfanya aendelee kuishi?

Ifike mahali tuwe na aibu, yaani Ramadhan Masanja ‘Banza Stone’, yuleyule Mwalimu wa Walimu apotee jumla na tusimkumbuke kabisa? Vizazi vijavyo visiwe na taarifa ardhi ya Tanzania ilipatwa kukanyagwa na mwanafasihi huyu?

Familia zina wajibu wa kuwafanya ndugu zao wasanii waliofikwa na mauti kuendelea kuishi.

Ni kwa vipi Tupac Shakur ‘Makaveli’, Christopher Wallace ‘Notorious BIG’, Elvis Presley ‘King of Rock’, Michael Jackson ‘King of Pop’, Marvin Gaye, Whitney Houston, Big Punisher, Ella Fitzgerald ‘Queen of Jazzy’ na wengineo wanaendelea kuishi?

Inakuwaje Kanumba, Ngwair, Gurumo, TX Moshi William, Sajuki, Kuambiana, Banza, Marijan Rajab, Mbaraka Mwishehe, Suleiman Mbwembwe, Hemedi Maneti, King Majuto na wengine wamekufa jumla?

Hapa nifafanue kuishi kwa msanii haina maana ya nyimbo zake kusikika mara mojamoja redioni, kutazamwa kwenye video, kuwarusha watu klabu na maeneo mengine ya starehe, la hasha!

Kuishi kwa msanii ni kule kuondoka kwake lakini nyuma yake anawaacha watu wakiendelea kuwa ‘bize’, yaani jina lake linaendelea kutengeneza shughuli na matukio ya kila siku yenye kuingiza fedha.

Unaweza kujiuliza ni kwa nini mpaka leo, Flora Mtegoa ambaye ni mama yake Kanumba, hajaweza kufungua kituo cha kumbukumbu za mwanaye.

Je, hata wasanii wenzake wameshindwa kumsaidia mawazo Flora kutambua kiasi cha fedha ambazo anaweza kutengeneza kupitia kituo cha kumbukumbu za Kanumba?

Hapa Tanzania hakuna kituo cha Marijan Rajab wala Mbaraka Mwishehe, hakipo cha Gurumo wala hakijafikiriwa cha TX Moshi William.

Wasanii kwa kawaida wanakuwa na vitu vingi vya kuenziwa. Jamii inanyimwa kuvijua kwa undani wake, hivyo kusababisha wasahaulike na wakati huohuo, familia zinakosa fedha.

Hapa haina maana ya kufa kufaana, hapana! Ila ni ukweli kuwa wasanii wengi wanapoondoka huacha fedha nyingi nyuma yao lakini hazikamatiki kwa sababu ya familia zao kukosa ubunifu.

Lazima kuwafanya watu watoke kona mbalimbali za ndani na nje ya nchi kisha kutembelea vituo vya wasanii wao.

Mathalan, siku ya kuzaliwa na ile aliyokufa msanii, katika kituo cha kumbukumbu za msanii husika, kunakuwa na shughuli nyingi. Watu wanalipa fedha!

Muhimu ni jinsi ya kukifanya kituo kuwa na hadhi kwa kukitangaza na kuhakikisha mtu akifika hachushwi.

Hivi Maalim Gurumo yakipata simulizi nzuri na yenye ufasaha, ikatengenezwa documentary, nani ambaye asingependa kuitazama au kuisikiliza?

Waza pia kuhusu TX Moshi, maisha yake, ubishoo wake, ukuu wake kimuziki, ustaa wake, alivyokuwa mtu pendwa kwenye jamii kisha afya yake ilipoanza kutetereka baada ya ajali na hatimaye kifo!

Nyimbo zake zinasikika zikisindikiza simulizi nzuri yenye mengi ambayo jamii haijapata kuambiwa na mengine yaleyale yaliyofahamika lakini yanawekwa pamoja.

Je, familia haioni kama hizo ni fedha na zipo nje-nje?

Leo hii James Dandu ‘Mtoto wa Dandu’ au ‘Cool James’ hata hakumbukwi. Ni wachache wenye kutambua kuwa alikuwa mwanamuziki mkubwa nchini na ndiye mwanzilishi wa Tuzo za Muziki Tanzania.

Tatizo ndugu wengi wa wasanii waliofariki dunia wakiulizwa, utasikia wanalalamika kuwa serikali haiwasaidii. Dah, kudadadeki! Yaani hata kubuni njia ya kutengeneza fedha kupitia jina la ndugu yako unataka usaidiwe na serikali?

Wewe andaa mpango mzuri, kisha utaona mwenyewe jinsi serikali inavyoweza kuwa karibu na wewe. Itajileta tu, si itataka kodi yake?

Voleta Wallace ni mama wa BIG, ukimfuatilia utagundua ana utajiri unaokadiriwa kuwa dola milioni 40, zaidi ya shilingi bilioni 80. Moja ya vitu ambavyo vimempa fedha nyingi Voleta ni documentary kuelezea maisha ya BIG.

Ni suala la kuiandaa vizuri na kuitengenezea njia bora za masoko.

Mtaji mmoja mkubwa ni lile jina ambalo msanii husika anakuwa ameliacha.

Maisha ya msanii yakiwekwa vizuri katika kitabu kizuri, watu watapenda kusoma. Itasaidia kumfanya msanii aendelee kuishi na familia kutengeneza fedha.

Wasanii wengi huwa na vitu ambavyo havijulikani, na watu wenye uwezo wa kuvisimulia kwa ufasaha ni ndugu zake. Mathalan, mama yake Ngwair, anayo mengi ya kusimulia kuhusu mwanaye, na watu wangeyapenda.

Yapi hasa maisha ya Ngwair tangu akiwa mtoto? Vitabia vyake vya utotoni, alipoanza kuisumbua familia wakati akiwa na kiu kubwa ya kufanikiwa kimuziki. Kunakuwa na simulizi kutoka kwa marafiki zake kuhusu maisha yao ya ghetto.

Nakala za vitabu zinapelekwa Maktaba ya Taifa ili vizazi na vizazi, wakienda kujisomea, wanapata pia fursa ya kusoma maisha ya wasanii ambao kwa hakika wanastahili kuitwa mashujaa wa sanaa.

Vitabu vina maana kubwa. Pattie Mallete ni mama yake Justin Bieber, yeye alipoona mwanaye ana jina kubwa, aliandika kitabu kuhusu maisha yake ya kumlea Bieber kinachoitwa Nowhere but Up (The Story of Justin Bieber’s Mom).

Pattie aliweza kuuza kitabu hicho nakala nyingi na kumpatia fedha zaidi ya Dola 10 milioni ambazo ni zaidi ya Sh20 bilioni.

Hata mama yake Diamond Platnumz, anaweza kuandika kitabu cha jinsi alivyomlea kwa tabu mwanaye na kutengeneza fedha nyingi kipindi hiki ambacho mwanaye anang’ara kila kona. Ni fursa!

Mimi mwenyewe ningependa sana kusoma kitabu kinachoeleza kwa ufasaha maisha ya Shem Kalenga lakini hakipo. Nahitaji mno kumsoma Dk. Remmy Ongala, sina pa kupata undani wa maisha yake.

Chanzo: mwananchi.co.tz