Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwana FA alivyomfungulia Dunia Marco Chali

Chali 3547070 Mwana FA alivyomfungulia Dunia Marco Chali

Sat, 24 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Akiwa kama mtayarishaji muziki, mhandisi wa sauti na mtunzi, Marco Chali amefanikiwa kuinua wasanii wengi Bongo tangu akifanya kazi katika studio ya Kama Kawa Records hadi MJ Records alikodumu kwa kipindi kirefu.

Marco amefanya kazi na wasanii wakubwa wa ndani na nje, ameshinda tuzo za muziki Tanzania (TMA) 2008 kama Mtayarishaji Bora wa Mwaka na kutoa albamu moja, Ona (2021). Fahamu zaidi;

1. Wimbo wa Mwana FA 'Binamu' ndio ulimtambulisha Marco Chali katika Bongofleva, kipindi hicho Marco alikuwa anafanya kazi katika studio ya Kama Kawa Records ndipo baadaye akapata nafasi pale MJ Records kwa Master J.

Hata hivyo, Mwana FA, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa sasa, tayari alikuwa asharekodi wimbo huo miaka mingi nyuma na ulikuwapo katika albamu yake ya pili, Toleo Lijalo (2003).

2. Tayari Maua Sama alikuwa amesharekodi wimbo wake 'So Crazy' huko nyumbani kwao Moshi ila alipoenda Dar es Salaam na kukutana na Mwana FA aliamua kwenda kuurudia kwa Marco Chali na ulipotoka ukamtambulisha vizuri.

3. Mbali na kutayarisha muziki, Marco pia anaimba akiwa amesikika kwenye nyimbo kama 'Kamili Gado' wa Professor Jay, 'Party Zone' wa AY, 'My Life' wa Quick Rocka, 'King Zilla' & 'Nataka' zake Godzilla n.k.

Ukiachana na Marco Chali, watayarishaji muziki wengine Bongo ambao nao wanaimba ni pamoja na Nahreel, S2kizzy, Mr. T Touch, Mocco Genius, Lollipop (Goodluck Gozbert), Abbah, Mesen Selekta, P-Funk Majani n.k.

4. Kundi la Wakali Kwanza linaloundwa na Joslin, Makamua na Q Jay ndio walitakiwa kusikika katika wimbo wa Fid Q 'Usinikubali Haraka' ila Matonya alipousikika akaupenda wimbo huo na kurekodi, hivyo Marco Chali akaona alichofanya kinatosha.

5. Marco Chali ni miongoni mwa watayarishaji muziki watatu walioshiriki kutengeneza mdundo wa wimbo wa AY, 'Zigo', wengine ni Nahreel na Hermy B. Na hadi sasa huo ndio wimbo wa AY uliotazamwa zaidi YouTube kwa muda wote ukiwa na 'views' milioni 22.

Ikumbukwe wimbo wa Mwana FA 'Kama Zamani' akiwashirikisha Mandojo, Domokaya na Kilimanjaro Band (Njenje) ulirekodiwa kwa watayarishaji muziki watatu pia, kwa Marco Chali, Bob Manecky na P-Funk Majani ambaye toleo lake ndilo liliachiwa.

6. Kabla ya kusaini mkataba wa lebo, MJ Records, Quick Rocka alipewa nafasi ya kurekodi nyimbo tatu za majaribio, wimbo wa kwanza kurekodi ulikuwa ni 'Bullet' ambao ulifanya vizuri sana ila aliyeurekodi ni Marco Chali na Master J.

Licha kutengenezwa na Marco Chali ndani ya MJ Records, mtayarishaji muziki wa kwanza kusikia vesi za wimbo huo alikuwa ni Bifu Chaa ambaye alizikubali sana na kumuita Marco na ndipo 'Bullet' ikarekodiwa.

7. Wimbo wa kundi la Top Band linaloundwa na Q Chief na TID 'Nilikataa' wakimshirikisha Mr. Blue, ulirekodiwa na Marco Chali ila mixing na mastering alifanya Master J.

8. Saa tatu asubuhi Q Jay alipokea simu kutoka kwa Marco Chali na kumuita studio MJ Records, alipofika akakuta mdundo wa wimbo 'Lonely' upo tayari, unaambiwa walitumia takribani saa mbili pekee kurekodi wimbo huo na kukamilisha.

Ni wimbo uliofanya vizuri hadi kuteuliwa kuwania tuzo ya TMA 2009 kama Wimbo Bora wa RnB ila hakufanikiwa kushinda.

9. Wimbo maarufu wa kundi la Wakali Kwanza 'Natamani' uliotengenezwa na Marco Chali ndio uliowapatia tuzo yao ya kwanza ya TMA kama Wimbo Bora wa RnB 2009 ikiwa ni mwaka mmoja baada ya Marco naye kushinda tuzo hiyo. 

10. Mdundo wa wimbo wa Godzilla 'Salasala', awali Marco Chali alikuwa umeuandaa kwa ajili ya Jay Moe ila baadaye akaona Zilla anaweza kuutendea haki na ndio uliokuja kumtoa rapa huyo kimuziki.

Hiyo ni sawa na P-Funk Majani, kwake mdundo wa wimbo wa D Knob 'Sauti ya Gharama' aliuandaa kwa ajili ya kutumika kwenye wimbo wa Mh. Temba 'Nampenda Yeye' ila baadaye akaamua nyimbo hizo zibadilishane midundo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live